Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all 296 articles
Browse latest View live

Jinsi ya Kupunguza Matumizi ya Chumvi katika Ulaji wa Vyakula na mengineyo

$
0
0

Chumvi inapotumika kwa kiasi kidogo haina madhara. Miili yetu inahitaji chumvi kwa kiasi kidogo sana kwasababu chumvi huupatia mwili madini ya Sodium yanayohitajika kusafirisha taarifa za mfumo wa fahamu, kudhibiti kiwango cha maji katika damu, ukunjikaji au kujivuta kwa misuli, udhibiti wa kiwango sahihi cha maji na uwiano sahihi wa chumvichumvi mwilini. 

Mwili unapata pia madini haya kutoka kwenye vyakula vingine kama maziwa na mayai, hivyo chumvi itumike kwa kiasi kidogo tu.

Chumvi yote inayotumika inapaswa kuwa na Lodone ambayo ni muhimu kwa ubongo wenye afya kwa mtoto aliye tumboni na anayekuwa pia huimarisha utendaji wa ubongo kiujumla. Matumizi makubwa ya chumvi ya zaidi ya gramu (2-5) kwa siku, huchangia kupanda kwa shinikizo la damu na kuongezeka hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na kiharusi. 

Watu wengi hutumia chumvi nyingi kwenye vyakula vyao, kwa wastani wengi hutumia gramu (9-12) kwa siku au mara mbili ya kiwango kinachopendekezwa.

Matumizi makubwa ya chumvi yana madhara gani?

Matumizi ya chumvi nyingi yanaongeza uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu, kwani chumvi husababisha maji kujikusanya mwilini. Maji yaliyojikusanya huongeza shinikizo kwenye moyo na mishipa ya damu na hivyo kusababisha moyo kufanya kazi kwa nguvu zaidi.

Shinikizo kubwa la damu huongeza uwezekano wa kupata magonjwa mengine sugu kama yale ya figo, moyo na pia mifupa kama "Osteoporosis". Hivi karibuni tafiti zimeonyesha uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya vyakula vilivyosindikwa au kuhifadhiwa kwa chumvi na saratani ya tumbo.

Mapendekezo ya kutumia chumvi kulingana na rika

Watu wazima, Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri watumie chumvi chini ya gramu 5 (Chumvi isiyozidi kijiko cha chai) kwa kila siku nzima.

Watoto (Miaka 2-15), Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri watumie chumvi chini ya kiwango cha juu cha matumizi ya chumvi kwa wakubwa kwa kuwa mahitaji ya nishati kwa mtoto na mkubwa hutofautiana.

Je, nini kifanyike ili kupunguza matumizi ya chumvi?

Nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zimekubali kupunguza matumizi ya chumvi kwa angalau asilimia 30 kufikia 2025.

Kupunguza matumizi ya chumvi hupunguza gharama kwa nchi kuboresha afya za wananchi wake. Inakadiriwa vifo milioni 2.5 vingeweza kuzuiwa kila mwaka endapo matumizi ya chumvi duniani yangepunguzwa kufikia kiwango kinachokubalika.

Jinsi ya Kupunguza Matumizi ya Chumvi, ngazi ya Taifa 

Kutokana na hali kuwa hatari zaidi naishauri Serikali iweze kuunda sera zitakazowabana wazalishaji na wauzaji wa vyakula, kutengeneza vyakula vyenye ubora kiafya na vya gharama nafuu. Aidha, iweze kudhibiti na kufuatilia matumizi ya chumvi kwenye jamii, kujua vyanzo vya chumvi na uelewa wa watu kuhusu matumizi ya chumvi.

Pia pamoja na hayo inatakiwa iweka mazingira mazuri ya kupunguza matumizi ya chumvi kwa kutekeleza sera na kuhamasisha vyakula vyenye afya sehemu kama shuleni, vyuoni n.k,Kufanya kazi na sekta binafsi kuboresha upatikanaji wa vyakula vyenye chumvi kidogo.

Kama mtaalam wa afya nawashauri wasomaji wa FikraPevu na Serikali kwa ujumla kupitia wizara zinazohusika waweze kuwapa elimu, utumiaji kwa vikundi juu ya umuhimu wa kupunguza matumizi ya chumvi.

Jinsi ya Kupunguza Matumizi ya Chumvi, ngazi ya mitaa 

Kujumlisha elimu ya kupunguza matumizi ya chumvi kwenye mafunzo ya waandaaji vyakula hasa mama lishe. Kuondoa mikebe ya chumvi kwenye meza za migahawa pamoja na kuweka lebo kwenye bidhaa zenye Sodium/chumvi nyingi.

Kutoa elimu ya lishe bora ukilenga matumizi ya chumvi kwa wateja/wagonjwa waliohudhulia vituo vya kutolea huduma za afya.
Kuelimisha watoto na kuwapa ushirikiano ili kuwazoeza kutumia kiwango kidogo cha chumvi kwenye vyakula vyao tangu wakiwa watoto.

Jinsi ya Kupunguza Matumizi ya Chumvi, ngazi ya familia 

(i) Punguza chumvi inayowekwa kwenye chakula wakati wa kuandaa au kupika chakula, kudhibiti matumizi ya vitafunwa vyenye chumvi mfano chips.

(ii) Usiweke chumvi mezani, kwa kuwa mara nyingi watu huongeza chumvi bila hata kuonja.

(ii) Epuka vyakula vilivyosindikwa kwa kutumia au kuongezwa chumvi, kama nguru aliyekaushwa kwa chumvi, baadhi ya vyakula vya makopo au paketi.

(iv) Ni vyema kusoma lebo kwa makini na chagua vyakula vilivyosindikwa bila ya chumvi iliyoongezwa (No salt added) au chagua bidhaa zenye sodium ndogo ndani yake.

(v) Tumia zaidi vyakula fresh unavyopika mwenyewe kwani unaweza kudhibiti kiasi cha chumvi unachotumia.

(vi) Tumia zaidi viungo kuongeza ladha kwenye chakula, mfano vitunguu saumu, tangawizi n.k

Maswali yaulizwayo mara kwa mara kuhusu chumvi

Swali: Je, unahitaji chumvi nyingi kwenye chakula ili kurudishia chumvi mwilini iliyopotea wakati unatokwa jasho jingi kipindi cha jua na joto kali?
Jibu: Hapana, hauhitaji kula chumvi nyingi kwa kuwa ni kiwango kidogo sana cha chumvi hupotea kwa njia ya jasho ingawa ni muhimu kunywa maji kwa wingi.

Swali: Je, chumvi ya baharini ni bora zaidi kuliko ya kiwandani kwa kuwa ni ya asili?

Jibu Hapana, bila kujali chanzo cha chumvi ni Sodium ile ile iliyomo kwenye chumvi ambayo husababisha matatizo ya kiafya.

Swali: Je, chumvi inayoongezwa wakati wa kupika sio chanzo kikuu cha chumvi inayotakiwa mwilini?

Jibu: Hapana, katika nchi nyingi asilimia 80 ya chumvi kwenye vyakula hupatikana kwenye vyakula vilivyosindikwa viwandani.
Swali: Je, chakula hakina ladha bila chumvi nyingi?

Jibu: Hapana, ingawa inaweza kuwa kweli mwanzoni ambapo vionja ladha vinakuwa havijazoea chumvi kidogo ila muda unavyozidi kwenda unazoea na kufurahia ladha ya chakula kama kawaida.

Swali: Je, ni kweli vyakula vyenye chumvi nyingi vinakuwa na ladha ya chumvichumvi?

Jibu: Hapana, kwa kuwa baadhi ya vyakula vyenye chumvi nyingi wakati mwingine huchanganywa na vitu vingine kama sukari na kufanya viwe na ladha isiyo na chumvi nyingi.

Swali: Je, ni watu wenye umri mkubwa tu ambao wanapaswa kuhofia juu ya matumizi makubwa ya chumvi?

Jibu: Hapana, ulaji wa chumvi nyingi unaweza kusababisha kupanda kwa shinikizo la damu katika umri wowote.

Swali: Je, kupunguza chumvi kunaweza kuwa ni hatari kwa afya yako?

Jibu: Hapana, kwa kuwa ni vigumu sana kula chumvi chini ya kiwango wakati kuna vyakula vingi vilivyo na chumvi tunavyokula kila siku mfano maziwa na mayai.

The post Jinsi ya Kupunguza Matumizi ya Chumvi katika Ulaji wa Vyakula na mengineyo appeared first on Fikra Pevu.


Baada ya Matibabu ya Moyo, Muhimbili yaanza Kutoa Huduma Mpya ya Kuzibua Mishipa ya Damu

$
0
0

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwa mara ya kwanza katika historia ya kuwepo kwa hospitali hiyo, imeanza kutoa huduma ya matibabu kwa njia ya kuzibua mishipa ya damu iliyoziba kutokana na sababu mbalimbali.

Habari za uhakika ziliziifikia  FikraPevu, zinasema huduma hizo za matibabu ya kuzibua mishipa ya damu iliyoziba, imeanza kutolewa wiki hii hosptalini hapo, ikiwa ni takriban miaka sita tangu hospitali hiyo ianze kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ya moyo.

Kabla ya huduma hiyo ya matibabu ya kuzibua mishipa ya damu pamoja na upasuaji wa moyo, huduma hizo zilikuwa zikitolewa nje ya nchi, hasa katika hospitali za India ambapo Serikali na watu wengine binafsi walikuwa wakiingia gharama kubwa kufuata matibabu hayo katika hospitali za nje.

Kuanza kutolewa kwa huduma hizo mbili za matibabu, kwa maana ya upasuaji wa moyo na uzibuaji wa mishipa ya damu, kumepokelewa kwa mikono miwili na wadau wengi wa sekta ya afya nchini, ambao wameweka wazi kwamba hiyo ni hatua kubwa mbele, katika jitihada za Serikali za kuboresha hospitali zote kubwa za rufaa nchini, ambazo pamoja na kusheheni madaktari bingwa wa tiba za aina hiyo, lakini hazikuwa zikitoa hutuma hizo kutokana na ukosefu wa vifaa tiba uliokuwa ukisababishwa na uchumi duni wa Serikali.

Daktari Mkuu katika Idara ya Magonjwa ya Moyo Muhimbili, Professa Mohamed Janabi, amethibitisha kuanza kutolewa kwa huduma hiyo ya upasuaji wa mishipa ya damu katika hospitali hiyo ya taifa, akisema huduma hiyo ya matibabu inatolewa na madaktari bingwa wa kigeni kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Kitanzania.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, ambaye kabla ya kuhamishiwa Muhimbili katika siku za karibuni na kuwa Mkuu wa Kitengo hicho cha Magonjwa ya Moyo alikuwa Daktari Mkuu wa Rais Jakaya Kikwete, huduma hiyo mpya ya matibabu itahusu uzibuaji wa mishipa inayosafirisha damu kwenda na kutoka kwenye moyo.

Uzibaji wa mishipa ya damu, unachangiwa na mambo mengi mbalimbali kutokana na mazingira na shughuli azifanyazo mwanadamu, lakini kubwa ikiwa ni ulaji wa aina ya vyakula vyema mafuta mengi.

DK. Joachim Mabula, ambaye ni mtumishi wa Serikali chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Tanga, anasema ulaji wa mafuta kuzidi kiasi kinachotakiwa mwilini, kwa kiasi kikubwa kunakaribisha hatari ya kuziba kwa mishipa ya damu kutokana na mafuta hayo kuganda katika kingo za mishipa hiyo.

Kwa mujibu wa Dk. Mabula watu wanene na wale wa magonjwa sugu kama vile kisukari wako katika hatari pia ya kuziba mishipa ya damu.

Aidha, baadhi ya wataalam wa afya wanabainisha kwamba mafuta pamoja na vitu vingine kama vile kemikali, vinavyoweza kusababisha matakaba kwenye mishipa ya damu, vinaweza kusababisha kuziba kwa mishipa inayosafirisha damu kwenda na kutoka kwenye moyo, hivyo kuhatarisha afya ya mwanadamu.

Wanasema kuziba huko kwa mishipa ya damu kusababishi njia ya damu katika mishipa hiyo kuwa nyembamba, hali inayochangia mgonjwa kupata na ugonjwa wa Mshtuko wa Moyo.

Kwa mujibu wa baadhi ya wataalam hao wa afya, kwa hapa nchini ugonjwa huo wa kuziba kwa mishapa ya damu, unapatikana kwa kiwango kikubwa katika jamii nyingi za wafugaji.

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu kwa siku kadhaa sasa umebaini kwamba tangu kuanza kutolewa kwa huduma ya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili miaka sita iliyopita, zaidi ya wagonjwa 400 wamekwishakupatiwa huduma hiyo, huku wagonjwa wawili kati yao wakipata huduma hiyo kwa kuwekewa mirija ya chuma kwenye mishipa ya moyo.

Kwa upande wa huduma ya matibabu ya uzibuaji wa mishipa ya damu, imebainika kwamba katika wiki moja tu ya kwanza ambapo huduma hiyo imeanza kutolewa hospitalini hapo, jumla ya wagonjwa 18 wako kwenye mandalizi ya kupata tiba hiyo, huku wagonjwa wawili kati ya hao wakihitaji matibabu ya ziada ya upasuaji mkubwa wa moyo pia.

Uchunguzi huo wa  FikraPevu, umebaini kwamba madaktari bingwa wa nje wanaoshirikiana na madaktari bingwa wa hapa katika kutoa huduma hiyo ya uzibuaji wa mishipa ya damu katika hospitali hiyo ya Muhimbili, wengi wao wanatoka katika nchi za Marekani na India.

Baadhi ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam waliozungumzia maboresho hayo makubwa ya huduma ya matibabu katika hospitali hiyo ya taifa, wameiomba Serikali kuongeza jitihada zaidi kwa kuhakikisha kwamba hospitali zote kubwa za rufaa nchini zinafanyiwa maboresho kwa kuongezewa wataalam bingwa wa magonjwa mbalimbali pamoja na kuzipatia vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya magonjwa ya moyo, saratani, uwekaji wa viungo bandia vya nyonga na goti, upasuaji wa ubongo, mishipa ya fahamu, figo na kadhalika.

Mkazi mmoja wa Dar es Salaam, aliyejitmbulisha kwa jina la Rebecca Kilakoy, amesema iwepo Serikali itachukua hatua za makusudi za kuboresha huduma hizo katika hospitali hizo, ni wazi kwamba si tu itakuwa imeokoa fedha nyingi zinazotuka kwa sasa kwa ajili ya kuwagharamia wagonjwa wanaosafirishwa kwenda nje kwa ajili ya kupatiwa huduma hizo za matibabu, bali itakuwa imeokoa pia vifo vya wananchi walio wengi, wanaofariki dunia kila siku kwa sababu ya matatizo hayo.

Huduma za matibabu kwa njia za upasuaji wa moyo, hadi sasa zinapaswa kuwa zinapatikana katika hospitali zote kuu za rufaa nchini, lakini kutokana na sababu ama zilizo nje ya Serikali au kutokana na vipaumbele vya watawala, huduma hizo hadi sasa hizipatikani kwa uhakika katika hospitali hizo, isipokuwa tu Muhimbili.

Kwa mfano, taarifa kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanajaro (KCMC) zinaeleza kuwa hadi sasa huduma ya upasuaji wa moyo katika hospitali hiyo si ya kuridhisha, kama ilivyo pia kwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, iliyoko jijini Mwanza.
“Hapa Bugando tunapokea wagonjwa wengi wa moyo. Kwa wastani tunapokea wagonjwa wawili au watatu kila wiki, na baadhi yao tumekuwa tukiwapa barua ya kwenda kupata matibabu Muhimbili,” anasema Daktari mmoja wa hospitali ya rufaa ya Bugando, Mwanza kwa sharti la kutotajwa jina lake.

The post Baada ya Matibabu ya Moyo, Muhimbili yaanza Kutoa Huduma Mpya ya Kuzibua Mishipa ya Damu appeared first on Fikra Pevu.

Utafiti: Ushuzi unaotokana na Kujamba, una Uwezo wa Kutibu Ugonjwa wa Saratani

$
0
0

UTOAJI wa ushuzi, katika mazingira yoyote yale, umekuwa na matokeo tofauti katika jamii yetu ya Kitanzania. Watu wanaotoa ushuzi au kujamba mbele za watu, huonekana mbele ya watu hao kama watu wasio kuwa na adabu, hivyo kudhalauliwa wakati mwingine.

Hata hivyo, taarifa za kitafiti za kisayansi, zinaweka wazi kwamba kutoa ushuzi au kujamba, ni afya. Kwa mujibu wa wataalam hao, kila mnyama kwa maana ya viumbe wote walio katika kundi la wanyama kisayansi, binadamu akiwemo, wakati fulani hujihisi tumbo kujaa gesi nyingi (kuvimbiwa), hivyo njia pekee ya ufumbuzi wake katika kuondokana na shida hiyo, ni kupunguza gesi hiyo kwa njia ya kujamba.

Kwa mujibu wa taarifa hizo za kitafiti, katika idadi yote ya viumbe hai vinavyojamba, mchwa anaongoza kuliko wanyama wengine wote. Aidha, mchwa huyo huyo anadaiwa kuchangia kupanda kwa joto la dunia (global warming) kwa kiwango kikubwa kwa kuwa huzalisha gesi ya methane kwa wingi kupitia njia hiyo ya kujamba. Kwa kawaida, gesi ya methane na hydrogen inaweza kusababisha moto.

Tafiti mbalimbali ambazo FikraPevu inazo, zimebainisha kwamba mwanadamu akijamba mfulululizo kwa kipindi cha miaka sita mfululizo akiwa ndani ya chumba kisichoruhusu hewa au gesi kutoka nje, anaweza kuzalisha nishati ya kutosha kutengeneza bomu mfano wa bomu la atomiki.

Kujamba ni tendo la kuachia hewa/gesi iliyobanwa ndani ya mwili (tumbo) kwa kutumia njia ya haja kubwa. Wakati binadamu anapokula au kunywa, hewa huingia tumboni kiasi kwamba hewa nyingine husababishwa na gesi kuingia kwenye utumbo ikitokea kwenye damu, huku baadhi ya gesi ikizalishwa na baadhi ya kemikali katika utumbo au bakteria.

Mtu anaweza kujamba akiwa katika fahamu zake zote au usingizini. Aidha, mtu anaweza kujamba pia hata baada ya kukata roho na kufariki dunia, ndani ya saa zake tatu za mwanzo. Hali hiyo ya maiti kutoa ushuzi au kujamba, husababishwa na hali ya kusinyaa kwa misuli baada ya kukata roho.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Exeter cha Uingereza, umebaini kuwa harufu ya ushuzi inaweza kutibu saratani/kansa na magonjwa mengine hatari. Kama ushuzi una nguvu za uponyaji huenda ukatumika kwa mambo mengine mengi, ingawa utafiti huu haukusema moja kwa moja.

Kwa zaidi ya wiki sasa, vyombo vingi vya habari vya Uingereza vimekuwa vikipambwa na vichwa vya habari vinavyohusiana na ushuzi kutibu hali zote za magonjwa hatari, ingawa si jambo lenye uhakika sana.

Kwa kawaida ushuzi unakuwa na asilimia 59 ya gesi ya nitrojeni, asilimia 21 ya gesi ya hydrogen, asilimia tisa ya gesi ya Carbon dioxide, asilimia saba ya methane na asilimia nne ni oksijeni.

Kwa hiyo, asilimia moja tu ya ushuzi inaweza kuwa Hydrogen Sulphide na Mercaptans, ambayo ndiyo ina Sulphur ndani yake. Kwa kawaida, Sulphur ndiyo inayofanya ushuzi utoe harufu mbaya. Ushuzi husafiri kwa mwendo wa futi 10 kwa sekunde na huchukua sekunde kati ya 10 na 15 hadi kuanza kusikika hatufu ya ushuzi baada ya mtu kujamba.

"Ingawa gesi ya Hydrogen sulphide inajulikana kuwa na harufu mbaya na hupatikana katika mayai yaliyooza pamoja na harufu ya mtu kujamba, hutengenezwa mwilini na inawezekana kuwa tiba kwa magonjwa fulani," anasema Dk. Mark Wood, Profesa wa Chuo Kikuu hicho cha Exeter.

Utafiti huo unadai kuwa kampaundi ziitwazo AP39, husababisha uzalishaji wa Hydrogen sulphide kwa wingi katika seli/chembe hai za mwili. Na kiwango kidogo tu cha Hydrogen sulphide, kimethibitika kulinda Mitochondria (Sehemu ya seli/chembehai inayotoa nguvu kwa seli yote na ambayo mara nyingi hushambuliwa na magonjwa).

Ndiyo kusema basi kwamba kama Hydrogen sulphide ina uwezo wa kulinda Mitochondria dhidi ya uharibifu wowote wa mwili wa binadamu, ni wazi kwamba Hydrogen sulphide hiyo inayokuwa kwenye ushuzi inaweza pia kuzuia kuendelea kwa magonjwa mengi yanayo shambulia mwili, mfano wa kansa.

Baadhi ya vipingamizi viliibuka na kuzuia furaha iliyoanza kusambaa. Kiukweli, utafiti ulikuwa na utata mkubwa na haukuhusisha moja kwa moja ushuzi, zaidi ya Hydrogen sulphide, gesi ambayo pia hutengenezwa na mwili ukiwa katika utendaji wake wa kawaida na kuupa ushuzi harufu mbaya.

Baadhi ya wanasayansi walidai sayansi inayohusu uvumbuzi huu ilibidi kuandikwa upya. Kwa kuwa inaaminika na wengi kwamba uvutaji wa mkusanyiko mkubwa wa Hydrogen sulphide ni hatari sana kwa afya.

Pia inaaminika kwamba kuvuta ndani ushuzi ina maana ya  sehemu ya gesi huingia kwenye mapafu na kutolewa nje tena bila kufyonzwa au kufikishwa kwenye seli/chembe hai iliyokumbwa na ugonjwa.

Wanasayansi wengi walishangazwa ni kwanini kitu hiki hakikuonekana kabla ya sasa, ikizingatiwa kwamba kwa kawaida, mtu anatoa ushuzi karibu mara 14 kwa siku, ingawa wengine huweza kutoa zaidi ya idadi hiyo, hasa wanapokuwa katika hali ya ugonjwa.

Kwa kuongezea, utafiti ulidhihirisha kwamba ni mara chache sana watu huzuiia upepo kwa watu walio wagonjwa mahututi kwa kuogopa kutokewa na kitu kibaya zaidi.

Wakati tamaduni nyingi za Kiafrika, ikiwemo Tanzania, zikichukulia tendo la kutoa ushuzi au  kujamba kuwa jambo lisilo la kistaarabu, kuna baadhi ya tamaduni hawaoni haya au aibu kujamba hadharani, huku wakifurahi tendo hilo. Kwa mfano watu wa kabila la Yanomami huko Amerika Kusini, kwao husalimiana kwa kujamba. Inasemekana hata nchini China mtu anaweza akapata ajira ya kudumu kwa kazi ya kunusa ushuzi.

Katika Roma ya zamani, Mfalme Claudius akihofia kwamba kujizuia kujamba kunaweza kuwa hatari kiafya, alipitisha sheria kwamba ni ruhusa kujamba kwenye ‘banquets’ zake, kwa maana ya hafla zinazofanyika kwenye makazi ya Mfalme au Ikulu.
Ndani ya jamii, baadhi ya watu huogopa kujamba hasa wakiwa na wenzi wao, wengine wakifikia hatua ya kushindwa kusinzia wakilala na wenzi wao wakiogopa kujamba kwa sauti wakiwa usingizini.Madaktari hawajakubaliana moja kwa moja kama kujizuia kujamba ni hatari kiafya au la.

Baadhi ya wataalamu wanafikiri kujamba ni sehemu muhimu katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula, hivyo kujizuia kujamba kunaweza kusababisha tumbo kujaa gesi na pia inaweza kusababisha kikundu.

Kikundu, ni ugonjwa wa kuvimba kwa mshipa wa damu ulio ndani ya njia ya haja kubwa na mara nyingi hutokeza nje na kumsababishia mtu maumivu makali. Hali hii, inadaiwa kusababishwa na mgandamizo mkubwa wa gesi, ambao kitaalamu hujulikana kama Hemorrhoids.

The post Utafiti: Ushuzi unaotokana na Kujamba, una Uwezo wa Kutibu Ugonjwa wa Saratani appeared first on Fikra Pevu.

Utafiti Mpya wabaini Ubora zaidi wa Maziwa kwa Afya ya Ubongo wa Binadamu

$
0
0

UTAFITI wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Kansas cha nchini Marekani, umebainisha kuwepo uwezezekano wa uhusiano wa karibu kati ya matumizi ya maziwa na afya ya ubongo.

Kwa mujibu wa utafiti huo mpya kabisa, matumizi ya maziwa mara kwa mara unaongeza kichocheo cha asili kinachopatikana kwenye ubongo wa mtu mzima mwenye afya njema, kichochea ambacho kitaalamu kinajulikana kama Glutathione.

Dk. In-Yung Choi ambaye ni Profesa Msaidizi wa Taasisi ya Tiba ya Chuo Kikuu hicho cha Kansas, ambaye pia hujishughulisha na mfumo wa fahamu, kwa ushirikiano na Dk Debra Sullivan, ambaye ni Profesa na Mwenyekiti wa Kitengo cha Lishe katika taasisi hiyo, ndio kwa pamoja wamebainisha hayo katika utafiti wao huo ambao FikraPevu imebahatika kuupata.

Matokeo ya utafiti wa madaktari wawili hao kuhusu maziwa, waliofanya kazi hiyo kwa kushirikiana, yamechapishwa na Jarida la The American Journal of Clinical Nutrition. Katika ushauri wao, wanasema kwamba unywaji wa maziwa, unaweza kuleta faida kwa mwili, hasa katika ubongo wa mwanadamu.

Kwa muda mrefu sasa imekuwa ikijulikana kwamba maziwa ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha afya ya mifupa pamoja na nyama za miili ya binadamu.

Hata hivyo, Dk. Sullivan, katika matokeo ya utafiti wao huo ameandika: "Utafiti huu unaonyesha kwamba maziwa yanaweza kuwa muhimu kwa ubongo wako pia."

Katika utafiti wao huo, madaktari hao waliwauliza maswali washiriki 60, kwa kuhusisha ulaji wao pamoja na kupiga picha za ubongo wao, ambazo zilitumika kupima viwango vya Glutathione ambacho ndicho kichocheo chenye nguvu katika ubongo. Wengi wa washiriki hao, ambao walikuwa wamekunywa maziwa muda si mrefu kabla ya kufanyiwa utafiti huo, walionyesha kuwa na viwango vikubwa vya Glutathione kwenye ubongo wao. 

Kwa mujibu wa madaktari hao, kichocheo cha Glutathione kinaweza kusaidia kuondoa mkazo (Oxidative Stress), pamoja na kuondoa uharibifu unaoweza kusababishwa na utendaji wa kawaida wa ubongo.

Mara nyingi, mkazo huo huambatana na magonjwa tofauti na hali mbalimbali, kama vile magonjwa ya Alzheimer (ugonjwa wenye dalili za upungufu wa akili), Parkinson (ugonjwa wenye kuharibu mfumo wa fahamu pamoja na kuharibu ujongeaji/kutembea) na magonjwa mengine mengi yanayomkumba mwanadamu.

Ni maziwa yapi bora zaidi kati ya maziwa freshi na mtindi?

Maziwa yote, freshi na mtindi yana virutubishi muhimu, hasa vya protini, madini na vitamini. Kutokana na hali hiyo, mtu anaweza kutumia maziwa aina yoyote kati ya aina hizo mbili kutegemeana naa matumizi yake.

Hata hivyo, maziwa ya mtindi yanaelezwa kuyeyushwa zaidi kwa urahisi tumboni, na pia husaidia uyeyushwaji wa vyakula vingine pamoja na ufyonzwaji wa baadhi ya virutubishi vilivyomo ndani ya vyakula alavyo mwanadamu.

Kwa hiyo, maziwa ya mtindi yanapendekezwa zaidi na wataalam, hasa kwa wagonjwa kwa kuwa yanamsaidia mgonjwa kupata virutubishi vingi zaidi kwa haraka. Aidha, maziwa ya mtindi yana aina ya bakteria wazuri na salama ambao huweza kuzuia au kutibu fangasi katika mfumo wa chakula.

The post Utafiti Mpya wabaini Ubora zaidi wa Maziwa kwa Afya ya Ubongo wa Binadamu appeared first on Fikra Pevu.

Zifahamu aina za Magonjwa ya Moyo, Dalili zake na Njia za Kujikinga

$
0
0

MAGONJWA ya Moyo (Cardiovascular Diseases), ni miongoni mwa magonjwa yaliyoko kwenye kundi la ugonjwa usioambukiza. Haya ni magonjwa yale yote yanayoathiri moyo na mishipa yake. Kwa hiyo, magonjwa ya moyo yanajumuisha ugonjwa wa Kupanda kwa Shinikizo la Damu (High Blood Pressure/Hypertension). Hili ni tatizo sugu la kiafya linalohusisha kuongezeka kwa mgandamizo wa msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu.

Magonjwa mengine ni Koronari za Moyo (Coronary Heart Diseases). Huu ni ugonjwa wa moyo ambapo mafuta yanaganda ndani ya ateri koronari na kuziba kwa kiasi fulani au kuziba kabisa kwa ateri ya koronari ya/za moyo, hivyo kusababisha upungufu wa damu katika sehemu ya moyo ambayo hupata damu kupitia mishipa hiyo.

Ugonjwa huu wa Koronari za Moyo hudhoofisha misuli ya moyo kiasi cha kusababisha moyo kushindwa kusukuma kiwango cha kutosha cha damu (Heart Failure). Aidha, ugonjwa huu  husababisha Arithmia (Arrhythmias), kwa maana ya ugonjwa unaosababisha mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio wa kawaida.

Kuna ugonjwa wa moyo unaoitwa Atherosklerosisi (Atherosclerosis). Hali hii ni kitendo cha mafutamafuta kuganda kwenye mishipa ya ateri. Kuganda kwa mafutamafuta huko, kunaweza kuchukua miaka mingi. Kadri miaka inavyosonga mbele, ndivyo mafutamafuta haya yanazidi kuwa magumu na kuzuia msukumo wa damu yenye oksijeni kwenye moyo.

Ikiwa mafutamafuta yataziba kabisa kwenye ateri koronari na kusababisha misuli ya moyo kukosa damu yenye oksijeni, huweza kumsababishia mtu maradhi mengine yanayoitwa Anjina (Angina), kwa maana ya maumivu makali ya kifua na Mshtuko wa Moyo (Myocardia Infarction/Heart Attack).

Anyurismu (Aneurysm) ni aina nyingine ya magonjwa ya moyo. Hiki ni kitendo cha mishipa ya ateri kuvimba kama puto kutokana na kuharibika kwa mishipa au kudhoofika kwa kuta za mishipa. Ikitokea mishipa hii ya ateri ikapasuka, husababisha damu kuvuja kwenye ubongo, hivyo kumsababishia mtu kukumbwa na Kiharusi (Stroke). Kiharusi ni ugonjwa wa kupooza unaotokana na kuingiliwa au kupungua kwa usambazaji wa damu kwenye ubongo hali inayosababisha seli za ubongo kukosa oksijeni na virutubishi.

Ugonjwa mwingine wa moyo hujulikana kwa jina la Rhumatiki ya Moyo (Rheumatic Heart Disease). Huu ni ugonjwa unasababisha kupungua utendaji kazi wa moyo kutokana na moyo kuwa na vivimbe tangu mtoto anapozaliwa (Congenital Heart Diseases), na mara nyingi huweza kusababisha vifo wakati wa utotoni.

Peripheral Vascular Disease ni ugonjwa mwingine wa moyo kwenye mishipa ya damu. Ugonjwa huu hutokea kwenye mfumo wa usambazaji wa damu nje ya ubongo na moyo. Mara nyingi, ugonjwa huu huwapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, hasa wavutaji wa sigara na wenye kisukari.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza kama yalivyo magonjwa ya moyo, kila mwaka huuwa watu milioni 38 duniani. Vifo vingi kati ya hivyo, hutokana na magonjwa ya moyo. Inakadiriwa kwamba watu takriban milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa hayo ya moyo, ikifuatiwa na magonjwa ya Saratani yanayouwa watu takriban milioni 8.2 kwa mwaka, wakati magonjwa ya njia ya hewa yanauwa watu milioni nne na Kisukari watu milioni 1.5 kila mwaka.

Kwa upande wa Tanzania, takwimu kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto nchini (PAT), zinaonyesha kwamba takriban watoto 13, 600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa aina mbalimbali ya moyo, huku watoto takriban 3, 400 kati yao, wakihitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.

Ni nini chanzo cha magonjwa ya moyo?

Kutozingatia kanuni za ulaji bora, ni moja ya mambo yanayoongeza uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya moyo. Kwa mfano, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi na lehemu nyingi, huku ulaji wa mbogamboga na matunda ukiwa ni wa kiwango cha chini, huongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo.

Aidha, hali ya kuwa na uzito uliozidi kiasi au kuwa na unene uliopitiliza pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili na viungo mara kwa mara, huchochea pia uwezekano wa magonjwa ya moyo.

Wakati mwingine magonjwa ya moyo huweza kutokana na historia ya ugonjwa huo katika familia. Umri unapozidi miaka 50 kuna uwezekano pia wa kupatwa na magonjwa haya ya moyo, huku wanaume wakiwa kwenye hatari zaidi ya kupatwa na tatizo hili mapema zaidi ikilinganishwa na wanawake.

Tafiti mbalimbali ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kuwa magonjwa ya moyo huanza kumwandama mtu pale mambo fulani yanaposababisha sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa. Mambo hayo fulani, ni pamoja na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha aina fulani za mafuta na lehemu katika damu. Hali hiyo inapompata mtu, mishipa ndani ya moyo huweza kufungamana kwa mafuta. hivyo kuleta Mshtuko wa Moyo (Heart Attack) au Kupooza, kwa maana ya Kiharusi (Stroke).

Aidha, ongezeko la lehemu huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Kiujumla, wingi wa lehemu unakadiriwa kusababisha vifo vya watu takriban milioni 2.6 duniani kila mwaka. Kuwepo kwa sukari nyingi katika damu, husababisha ugonjwa wa Kisukari, ambao unamweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa Moyo au Kupooza/Kiharusi mara mbili zaidi ya asiye na Kisukari.

Aidha, kuwa na sukari nyingi kwenye damu kwa muda mrefu, husababisha kuganda kwa mafutamafuta kwenye mirija ya damu. Kuganda huku kunaweza sababisha kupungua kwa mtiririko wa damu kwenye mishipa.

Shinikizo Kubwa la Damu, maana yake ni kwamba moyo unalazimika kusukuma damu kwa nguvu ili kutosheleza mahitaji ya mwili. Kuulazimisha moyo kufanya kazi kuliko kawaida yake, kunasababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure).

Uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku kwa kutafuna au kunusa (ugoro), husababisha pia sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo. Kemikali zinazopatikana kwenye tumbaku, huweza kuharibu seli za damu. Uharibifu huo wa seli, huingilia muundo na utendaji mzuri wa mishipa ya damu. Aidha, kuharibika kwa mishipa ya damu, kunachochea mafuta kuganda kwenye mishipa ya damu (Atheroskerosisi).

Unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji wa dawa za kulevya ni hatari tena kwa hili. Unywaji pombe mara kwa mara huongeza uzito wa mwili, hali inayoweza kusababisha Shinikizo la Damu kupanda. Aidha, pombe na dawa za kulevya hudhoofisha misuli ya moyo na mishipa ya damu. Misuli na mishipa ya damu ya moyo ikishadhoofika, huweza kusababisha moyo kutofanya kazi katika ubora wake (Heart Failure).

Lakini pia, ikitokea mishipa ya damu ikaharibiwa, mafuta mwilini hujikusanya katika sehemu ya mishipa iliyoharibiwa, hivyo kutengeneza utando wa mafuta (plaque). Kadri muda unavyoendelea ndivyo mafuta haya yanavyozidi kujijenga katika sehemu hiyo hadi kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba, hivyo kupunguza kiasi cha damu kinachobeba hewa ya oksijeni na virutubishi kwenda kwenye misuli ya moyo.

Kitendo hicho kitaalamu, huitwa Atherosklerosisi, ikimaanisha kukakamaa kwa mishipa ya ateri kutokana na mkusanyiko wa mafutamafuta ndani ya ateri. Hatimaye sehemu hiyo ikipasuka, sehemu ya seli za damu zinazoitwa pleteleti za damu (chembe ndogo mviringo ambazo zinahusika na kuganda kwa damu) ambazo husaidia mwili kuponya kidonda, hujigandisha kwenye mpasuko, hivyo kuanza kujikusanya.

Hali hii huongeza mkusanyiko, hivyo kuendelea kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba zaidi, hivyo kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure) na mtu kupata ugonjwa wa Mshtuko wa Moyo (Heart Attack).

Mkusanyiko wa mafuta na pleteleti za damu wakati mwingine, huweza kumeguka katika mfumo wa mabonge na kusafiri kwenda kuziba mishipa midogo ya damu kichwani. Hali hii ikitokea, mtu hupata Kiharusi (Stroke/Cerebrovascular Accident).

Dalili kuu za magonjwa ya moyo

Kinachosikitisha hadi sasa katika tasnia ya magonjwa ya moyo, ni kwamba mtu anaweza asione dalili zozote za moja kwa moja za magonjwa ya moyo, hadi wakati mishipa ya damu ya moyo inapokuwa imeziba kabisa au kushindwa kuruhusu damu kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.

Mara nyingi, hakuna dalili inayojitokeza moja kwa moya kwa wagonjwa wa aina hii, hadi pale moyo wenyewe unaposhindwa kufanya kazi ghafla (Heart Attack) au mtu anapopata Kiharusi (Stroke). Zaidi ya maelezo hayo ya wataalam wa magonjwa ya moyo, dalili zinapojitokeza mapema huweza kutofautiana kutegemea na aina ya ugonjwa wa moyo, ingawa dalili hizo nazo hazijitokezi mapema kama ilivyo kwa magonjwa mengine.

Hata hivyo, dalili kuu za magonjwa ya moyo ni pamoja na maumivu ya kifua (Hii ni dalili kuu ya ugonjwa wa moyo); moyo kwenda mbio na kumfanya mtu akose pumzi au kushindwa kupumua; kuvimba miguu, tumbo na mishipa ya shingoni kujitokeza nje; maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya; tumbo kujaa, kichefuchefu, na kutapika; kukosa usingizi; kupoteza fahamu na kikohozi kisichokwisha.

Kilicho muhimu kutambua hapa ni kwamba hadi dalili hizo zijitokeze wazi, ni kwamba mtu huyo amekuwa akiishi na ugonjwa huo kwa muda mrefu. Kwa hiyo, njia bora ya kugundua mapema dalili ya ugonjwa wa moyo ni kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Inashauriwa mtu kuwa na ratiba maalum ya kumuona daktari angalau mara moja kila mwaka ili kuweza kuchunguza afya ya moyo wako na mwili kiujumla. Endapo mtu atahisi maumivu ya aina yoyote kifuani, hasa baada ya kufanya mazoezi, ni muhimu kuonana na daktari haraka.

The post Zifahamu aina za Magonjwa ya Moyo, Dalili zake na Njia za Kujikinga appeared first on Fikra Pevu.

Wajawazito walazwa na Kujifungulia Nje ya Wodi za Wazazi

$
0
0

KINA mama wajawazito, wanaopata huduma za afya ya uzazi na kujifungua katika Kituo cha Afya cha Likombe, kilichopewa hadhi hivi karibuni kuwa Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Mtwara/Mikindani, baadhi yao wanalazimika kulazwa nje ya wodi ya kujifungulia kutokana na wodi za wazazi kujaa kupita kiasi.

Wakizungumza na FikraPevu kituoni hapo, baadhi ya kina mama wajawazito wamesema wamekuwa wakilala nje ya wodi ya wazazi tangu Aprili 9, mwaka huu, baada ya uongozi wa kituo hicho kuwataka wafanye hivyo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kukosekana kwa nafasi katika wodi ya wajawazito.

Mmoja kati ya kina mama waliofika kwa ajili ya kujifungua kituoni hapo akiwa na matatizo ya uzazi yanayohitaji kufanyiwa upasuaji, alisema baadhi yao walitandikiwa magodoro nje, hali iliyosababishwa na kujaa kwa wajawazito katika wodi yao.

Aidha, mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Fatma Khamisi, ambaye alikwenda kituoni hapo kwa lengo la kupata huduma, alisema hali hiyo ya kujaa kwa wodi ya wazazi, kumewalazimu baadhi yao kujifungulia nje.

Akizungumzia kadhia hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, Dk. Mohamed Gwao, anasema uongozi wa hospitali hiyo umekuwa ukitoa ushirikiano wa dhati katika hospitali za wilaya zote za mkoa huo pale wanapohitajika na kwamba hata siku moja hawajawahi kumkataa mgonjwa katika hospitali yake hiyo.

Kuhusu mlundikano wa wajawazito unaopelekea baadhi yao kulazwa na kujifungulia nje ya wodi za wazazi, Dk Gwao anasema uongozi wake haukuwa na taarifa hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Manispaa ya Mtwara, Jamadi Abdallah, amekiri kwa FikraPevu kuwepo kwa upungufu wa majengo ya wodi za wazazi katika kituo hicho cha Likombe. 

Alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa kituo hicho tayari umempata mkandarasi ambaye ameanza kufanya marekebisho kwa baadhi ya majengo ya wodi hizo ili kuongeza vyumba.

“Kuna mipango ya kuongeza wodi na tayari mkandarasi yupo. Tatizo linalokikabili kituo hiki cha afya ni kuwa na eneo dogo lisiloruhusu upanuzi zaidi wa majengo. Hili la wajawazito kulala nje ni la dharura tu kwa sababu mara nyingi inapotokea wajawazito wakawa wengi tunawapa rufaa ya kwenda hospitali ya Ligula,” anasema Abdallah.

Manispaa ya Mtwara/Mikindani iliamua kukipatia Kituo cha Afya Likombe hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya kutokana na mzigo mkubwa uliokuwa ukiielemea Hospitali ya Mkoa ya Ligula, ambayo kwa sasa imepewa hadhi ya kuwa hospitali ya rufaa.

The post Wajawazito walazwa na Kujifungulia Nje ya Wodi za Wazazi appeared first on Fikra Pevu.

Funguo Tano za Kumhakikishia Mtu kuwa na Afya Njema muda wote

$
0
0

Ili mtu aweze kufanikiwa malengo yake anapaswa kuwa na mahitaji fulani. Moja ya hitaji kubwa na la msingi ni kuwa na afya njema. Endapo mtu hatakuwa na afya njema atatumia gharama kubwa na muda mwingi ili kuboresha afya yake. Zifuatazo ni funguo tano za kudumisha afya njema.

Zingatia Usafi

Mtu kuwa na afya bora inabidi kuzingatia usafi wa mwili, mazingira anayoishi pamoja na vile anavyokula na kunywa. Kuna magonjwa mengi yanasababishwa na mazingira machafu, kwa mfano magonjwa ya kuhara na mchochota wa ini. Kudumisha usafi kunaweza pia kuepusha kuenea kwa magonjwa hatari kama vile nimonia (kichomi) na magonjwa ya kuhara.

Ikiwa ngozi ndio ogani kubwa kuliko zote katika mwili na inafanya kazi ya kulinda mwili dhidi ya vimelea/bakteria vya magonjwa. Hatuna budi kuitunza kwa makini. Inashauriwa kuoga maji safi ili kuondoa vimelea juu ya ngozi na sumu kutoka ndani ya mwili. Kuoga pia kunasaidia kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, kuboresha msukumo wa damu, kupunguza msongo wa mawazo na sukari mwilini.

Wengi husema uso ndio mapokezi au sehemu ya kwanza mtu kuingalia kabla ya sehemu nyingine ya mwili. Hivyo, unapaswa kutunza sura yako kwa umakini pia. Nawa uso kwa maji na sabuni kila siku ili kuzuia usiambukizwe magonjwa ya macho. Nyuso za watoto zinawishwe pia kila siku. Kwa maana nyuso chafu huvutia inzi walio na viini vinavyoweza kusababisha magonjwa ya macho na hata upofu.

Ni vyema kutunza meno yako kwa kupiga mswaki na kutumia uzi mwembamba kuondoa uchafu katikati ya meno kila baada ya kula, na hasa kabla ya kulala, kutazuia meno yasioze, magonjwa ya fizi na kung'olewa jino. Usipokuwa na meno huwezi kufurahia & kunufaika kabisa na vyakula unavyokula. Ni vyema kuwafundisha watoto kupiga mswaki & kuondoa uchafu katikati ya meno kwa kutumia uzi mwembamba baada ya kula ili wafurahie afya bora ujanani na maisha yao yote.

Magonjwa mengi yakuambukiza hasa ya kuhara yanayoua  watoto zaidi ya milioni mbili walio chini ya umri wa miaka mitano kila mwakayanasambaa haraka sana kupitia mikono. Hivyo usafi wa mikono yetu ni muhimu sana ili kulinda afya yetu na ya wengine. Unapaswa kunawa mikono baada ya kutoka chooni, baada ya kumbadilisha nepi mtoto au kumsaidia kutumia choo, kabla na baada ya kutembelea mgonjwa, kabla ya kutayarisha, kuhudumia au kula chakula, baada ya kupiga chafya, kukohoa, au kupenga kamasi, baada ya kumgusa mnyama au kinyesi cha mnyama na baada ya kutupa takataka.

Watoto wadogo hasa wanaotambaa, mara nyingi huweka mikono yao mdomoni. Hivyo, ni muhimu kuwanawisha mikono mara kwa mara, hasa baada ya wao kujisaidia au kabla ya kula. Wafundishe kunawa mikono yao na kutocheza karibu na vyoo au karibu na sehemu ambazo watu hujisaidia.

Aidha, ni jambo la busara kuhakikisha nyumba yako ni safi. Jitahidi sana kusafisha na kudumisha usafi na unadhifu wa nyumba yako, ndani na nje. Hakikisha kwamba maji hayajikusanyi mahali popote na hivyo kufanya mbu wazaane. Mahali ambapo vyoo havipo, kinyesi kinapaswa kufukiwa ardhini mara moja. Si vema kusahau kwamba vinyesi vyote vina viini vya magonjwa, hata vinyesi vya watoto wachanga. Hata vinyesi vya watoto vinapaswa kutupwa chooni au kufukiwa ardhini.

Ondoa takataka zote za nyumbani kwa kuwa inzi, mende na panya ambao hueneza viini vya magonjwa, huzaana sana na kufurahia maisha kwenye takataka. Ikiwa unapoishi hapana huduma ya kuondoa takataka, tupa takataka katika shimo ambamo zinaweza kufukiwa au kuteketezwa kila siku.

Usafi unakwenda sambamba na usafi wa maji ya kunywa. Maji yanaweza kusababisha magonjwa yanayotokana na vimelea kama vile kipindupindu, ugonjwa hatari wa kuhara, homa ya matumbo, mchochota wa ini na magonjwa mengine ikiwa chanzo cha maji si safi na salama au hakikutunzwa vizuri. Maji yasiyo safi na salama ni moja ya chanzo cha ugonjwa wa kuhara kwa visa vya watu bilioni 1.7 hivi kila mwaka.

Pata mlo kamili na unaofaa

Ili mtu awe na afya nzuri, anahitaji chakula chenye lishe bora. Mtu anahitaji kula vyakula vya kujenga mwili, kuupa mwili nguvu na kulinda mwili. Hivyo unapokula tumia pia matunda, mboga na uwe na kawaida ya kula vyakula vya aina mbalimbali. Vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa kama vile mkate, nafaka yenyewe mfano dona, tambi au mchele vina virutubisho na nyuzinyuzi kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka zilizokobolewa.

Mafuta yanayopaswa kutumika kupikia vyakula vyako yanafaa yawe ya asili ya mimea kama alizeti na sio ya yenye asili ya wanyama kwa maana yana kiwango kikubwa cha lehemu inayohatarisha afya ya mtumiaji. Pia, chumvi inabidi utumiwe kwa kiasi pamoja na kuendelea kuepuka kuongeza chumvi mezani wakati wa kula kwa maana ni hatari kwa moyo wa mtumiaji.

Ni muhimu nyama ya jamii za kuku na nyama nyingine zipikwe na kuiva barabara. Viini vya magonjwa huongezeka sana katika chakula chenye uvuguvugu. Kwa hiyo, chakula kiliwe mara moja baada ya kupikwa. Ikiwa itabidi kuhifadhi chakula zaidi ya masaa mawili, hakikisha kinahifadhiwa katika hali ya joto au kuwekwa mahali penye baridi kama jokofu.

Kutokana na kuongezeka kwa teknolojia na mapinduzi katika kilimo, mimea mingi ya chakula hukuzwa na kemikali ambazo zinaweza kuwa hatari kwa afya yako. Ni hatari kula vyakula visivyofaa maana vinaweza sababisha magonjwa au kifo. Pia, vyakula vyovyote visipotayarishwa na kutunzwa vizuri vinaweza kukuletea madhara.

Fanya mazoezi ya Viungo vya Mwili

Unahitaji kufanya mazoezi bila kujali umri wako ili kuwa na afya njema. Ni vizuri kuwasiliana na daktari au mtaalamu wa mazoezi kabla ya kuanza kufanya mazoezi yoyote mapya, kwa maana mazoezi yanayofaa yanategemeana na umri na afya ya mtu. Kufanya mazoezi kunaweza kukusaidia kulala vizuri, kuwa na furaha zaidi, kuwa na akili makini, kuweza kutembea kwa wepesi, kuwa na mifupa na misuli yenye nguvu, kudumisha au kuwa na uzito wa mwili unaofaa kiafya iwapo pia utakula chakula chenye lishe, kupunguza hatari ya kuwa na ugonjwa wa kushuka moyo, kupunguza hatari ya kufa mapema.

Ikiwa haufanyi mazoezi huenda ukapatwa na ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa kisukari, kupatwa na kupanda kwa shinikizo la damu, mwili kuwa na kiwango cha juu cha lehemu au kolesteroli pamoja na kupatwa na kiharusi (Stroke).

Wataalam wa mazoezi ya viongo wana mapendekezo yao ya mazoezi kulingana na umri wa mtu. Mtu anahitaji kufanya mazoezi rahisi na mazoezi magumu. Mazoezi rahisi hukufanya utoe jasho, lakini magumu ni yale ambayo unapoyafanya inakuwa vigumu kwako kuzungumza.

Kwa watoto wa chini ya miaka mitano, hawapaswi kuzubaa kwa muda mrefu labda wawe wamesinzia. Kutazama luninga na kusafiri mara kwa mara na kwa muda mrefu kwa kutumia basi au garimoshi/treni kunadhoofisha afya ya mtoto na ukuuaji wake. Mazoezi mepesi kwa watoto ni pamoja na kusimama na kutembea polepole, wakati mazoezi magumu kwa watoto ni kama kutembea haraka, kuogelea, kuruka kamba na kuendesha baiskeli.

Kwa upande wa watoto wa miaka mitano hadi 18 (5-18), wanapaswa kutumia angalau dakika 60 (saa moja) za mazoezi kila siku, ikijumuisha mazoezi rahisi kama ya kuendesha baiskeli taratibu, wakati mazoezi magumu ni kukimbia haraka na kucheza tenisi. Siku tatu za wiki, mazoezi yanapaswa kushirikisha, mazoezi ya kunyoosha misuli kama pushapu pamoja na mazoezi ya kunyoosha mifupa kama kukimbia.

Watu wazima wa miaka 19-64, wanahitaji angalau dakika 150 (saa 2.5) za mazoezi rahisi kama kuendesha baiskeli taratibu na kutembea haraka kwa kila wiki na siku mbili au zaidi kwa wiki fanya mazoezi ya misuli kama kubeba uzito mkubwa na pushapu. Njia nyepesi ya kufaulu kutimiza muda uliopendekezwa wa mazoezi ni kufanya mazoezi kwa dakika 30 kila siku kwa siku tano za wiki.

Pumzika au pata muda wa kutosha kulala usingizi

Mabadiliko ya maisha yameongeza vikengeushafikira na hekaheka za maisha ya sasa na kufanya watu wasiwe na wakati wa kutosha kulala. Kulala na kusinzia vya kutosha muhimu kwa ajili ya ukuzi na maendeleo ya watoto na vijana, kujifunza na kukumbuka habari mpya, kudumisha usawaziko unaofaa wa homoni zinazosaidia kumeng'enya chakula na uzito wa mwili, kudumisha moyo wenye afya nzuri na kuzuia magonjwa.

Usingizi huimarisha mfumo wa kinga na kupunguza hatari ya kupatwa na maambukizo, kisukari, ugonjwa wa moyo, kansa, kunenepa kushuka moyo na pengine hata ugonjwa wa Alzheimer. Usingizi ni muhimu tunapokuwa wagonjwa. Miili yetu inaweza kushinda magonjwa fulani kama vile mafua tukilala kwa muda mrefu zaidi na kunywa vinywaji vingi.

Kutolala vya kutosha kumetajwa kuwa chanzo cha kunenepa kupita kiasi, kushuka moyo, ugonjwa wa moyo, kisukari na chanzo cha aksidenti mbaya.

Kiasi kinachohitajika cha usingizi kinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Watoto wengi wachanga hulala saa 16 hadi 18 kwa siku, watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi mitatu hulala saa 14 na wale wenye umri wa miaka mitatu hadi minne hulala saa 11 au 12 hivi. Watoto walio na umri wa kutosha kwenda shule kwa ujumla wanahitaji kulala kwa saa 10, vijana kwa saa 9 au 10 na watu wazima kwa saa 7 hadi 8.

Pima na Linda Afya yako

Baadhi ya magonjwa huhitaji uchunguzi wa daktari. Kwa kawaida, ugonjwa ukigunduliwa mapema, unaweza kutibiwa kwa urahisi na mtu atatumia pesa kidogo. Kwa hiyo, usipojihisi vizuri, badala ya kujaribu kutibu dalili tu, muone daktari ili achunguze kisababishi ni nini.

Epuka kujijeruhi wakati unafanya shughuli. Unashauriwa kufuata sheria za usalama unapofanya kazi, unapoendesha baiskeli, pikipiki au gari. Hakikisha chombo chako cha usafiri ni salama. Vaa nguo za kujikinga na vifaa vinavyofaa vya kujikinga kama vile miwani, kofia, viatu na pia mikanda ya usalama na vifaa vya kulinda masikio.

Epuka kukaa kwenye jua kwa muda mrefu kwa kuwa hilo husababisha kansa na pia kufanya ngozi ipate makunyazi mapema. Acha kuvuta sigara na kutumia bidhaa za tumbaku kama ugolo ikiwa wewe hutumia. Kuacha sasa kutapunguza sana hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo, kansa na mapafu na kiharusi.

Katika dunia hii, haiwezekani kuwa na afya kamilifu kwa maana wanadamu  hatujakamilika. Hivyo, tunapokuwa wagonjwa huenda ikawa si kwa sababu ya uzembe wetu, bali kwa sababu ya udhaifu wa kibinadamu tuliorithi kwa Adamu na Hawa.

The post Funguo Tano za Kumhakikishia Mtu kuwa na Afya Njema muda wote appeared first on Fikra Pevu.

Wauguzi Tanzania Waadhimisha Siku yao huku Wakiyaenzi Matatizo Lukuki

$
0
0

KESHO Mei 12, 2015 ni Siku ya Wauguzi Duniani. Wauguzi ni miongoni mwa kada muhimu kwa jamii yoyote duniani katika kada za utumishi wa umma, umuhimu unaotokana na taaluma yao hiyo kwa wagonjwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya nchini.

Katika kutathimini umuhimu wa Wauguzi kwa jamii yoyote duniani, FikraPevu imeangazia Siku ya Wauaguzi Duniani inayoadhimishwa kila tarehe 12 Mei ya kila mwaka, wauguzi kote duniani hujitathimini wao wenyewe pamoja na kazi yao hiyo, kama kweli wanaendelea kumuenzi muuguzi wa kwanza ulimwenguni, Florence Nightingale.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala haya katika kutathimini siku hiyo na kazi yao hiyo, Ofisa Muuguzi Mkuu wa Kituo cha Afya cha Palestina, Sinza, Dar es Salaam, Alphones Chiwambo, anasema pamoja na mambo mengine siku hiyo ina umuhimu kwao, kwani inawakumbusha kumuenzi muuguzi wa kwanza wa fani hiyo Florence Nightingale.

“Mbali na kumuenzi Florence, siku hii huitumia kujitathimini sisi wenyewe na kazi yetu hii, kuona ni wapi tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Tunatathimini mazingira ya kazi zetu kama yanafanana na jinsi yanavyopaswa kuwa kwa maana ya ubora wa mazingira na ubora wa huduma tunayoitoa kwa jamii,” anasema Chiwambo na kuongeza.

“Sekta hii ya uuguzi inazo changamoto nyingi sana, hasa kwa mataifa yetu haya masikini. Tunakabiliwa na upungufu wa wafanyakazi ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa ambao mMuuguzi mmoja anapaswa kuwahudumia siku.”

Kwa mujibu wa Chiwambo, kwa kawaida Muuguzi mmoja anatakiwa awahudumie wagonjwa wanne hadi watano kwa siku, lakini kutokana na upungufu wa Wauguzi katika hospitali na vituo vya afya nchini, Muuguzi mmoja anaweza kuhudumia wagonjwa kati ya 50 na 100, jambo analosema ni tatizo kwa Muuguzi na Mgonjwa mwenyewe pia.

Wauguzi kuhama fani

Imebainika kwamba lipo wimbi kubwa la watu walioamua kusomea fani ya uuguzi, lakini waliamua kuikimbia kutokana na ukweli kwamba kipato chao hakilingani na majukumu wanayokabiliana nayo wakati wa kuwahudumia wagonjwa. Mourine Ambwene ni mmoja wa Wauguzi katika moja ya vituo vya afya jijini Dar es Salaam anayekiri kwamba kipato cha muuguzi kinachotokana na mshahara wake kwa mwezi hakilingani na majukumu yake, hali inayowafanya baadhi ya wauguzi kuikimbia fani hiyo.

“Inafika mahali mtu anaamua kubadili fani hii badala ya kujiendeleza. Baadhi yetu wanaona ni afadhali wakauze mafuta kwenye vituo vya kuuzia mafuta ya magari, kuliko kuendelea na kazi hii,” anasema Mourine katika mazungumzo yake na FikraPevu katika tathimini yake juu ya Siku ya Wauguzi Duniani.

Kwa mujibu wa Mourine, kitu ambacho hadi sasa Serikali haijakipa kipaumbele ni uwiano unaopaswa kuwepo kati ya idadi ya wauguzi na idadi ya wagonjwa, sambamba na watoa hudumu nyingine za afya, wakiwemo madaktari.

Wahudumu kutoa lugha chafu kwa wagonjwa

Kuhusu malalamiko yanayoelekezwa kwa wahudumu wa afya kutumia lugha ya kuudhi kwa wagonjwa, kiasi cha baadhi ya wagonjwa hao kupoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya wauguzi, imeelezwa kwamba wakati mwingine lugha hizo za maudhi hutokana na sababu nyingi, ikiwemo kuelemewa na kazi.

“Wakati mwingine lugha chafu hutokana na kuelemewa na kazi. Kwa mfano unakuta muuguzi yuko mmoja tu au wako wawili, lakini mbele yao kuna wagonjwa 500 ambao kila mmoja wao anataka ahudumiwe yeye kwanza kutokana na kujiona yeye yuko katika hali mbaya zaidi kuliko wengine… katika mazingira haya mtu hujikuta akitokwa na kauli ambayo kwa kweli haistahili kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya kazi hii, lakini kutokana na kuzidiwa anajikuta ametoa tu kauli,” anasema mmoja wa wauguzi aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na FikraPevu wamewahimiza Wauguzi kote nchini, katika kuadhimisha siku yao hiyo kukumbushana umuhimu wa kutumia lugha za kiungwana kwa wagonjwa, wakitolea mfano wa matukio mbalimbali ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga, hasa kashfa ya hivi karibuni kabisa ya Muuguzi mmoja mkoani Dodoma kumchapa mama mjamzito kiboko wakati akiwa katika hali ya uchungu wa kujifungua na kusababisha mtoto kichanga kufariki kikiwa bado tumboni.

Baadhi ya wanawake wajawazito katika Kituo cha Afya cha Palestina, Sinza, wamekiri kwamba baadhi yao wamekuwa wakikosa huduma kutokana na kukosa fedha za kuwapatia wauguzi kama rushwa ili wawahudumie vizuri.

Kwa mujibu wa wanawake hao, pamoja na Serikali kusema mara kwa mara kwamba huduma ya mama na mtoto inatolewa bure, lakini ukweli ni kwamba hakuna huduma hiyo inayotolewa bure kwenye vituo vya afya.

Baadhi ya wauguzi jijini Tanga, wameelezea changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na hospitali na vituo vingi vya afya kukabiliwa na uhaba wa vifaa, kama vile glovu na maski kwa ajili ya kujikinga mikono na hewa puani wakati wa kumdumia mgonjwa, pamoja gharama kubwa wanayotumia kwenda na kurudi kwenye vituo vya kazi kutokana na uhaba wa nyumba za wauguzi kwenye hospitali na vituo hivyo afya.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mei 5, 2015 alikaririwa na FikraPevu akiwa mkoani Mara akisema Serikali imeanzisha Kurugenzi ya Wauguzi na Wakunga katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoa huduma hao kwenye utoaji wa huduma kwa umma.

Kwa mujibu wa Pinda, ili kukidhi mahitaji ya wauguzi na wakunga nchini, Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na fani hizo.

“Mwaka 2009 tulikuwa na wanafunzi wa Uuguzi na Ukunga 617 wa ngazi ya Cheti na 925 wa ngazi ya Diploma. Kufikia mwaka 2014 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia wanafunzi 2,566 wa Cheti, sawa na ongezeko la asilimia 31.5 na wanafunzi 2,294 wa Diploma, sawa na ongezeko la asilimia 14.1 katika kipindi cha miaka mitano,” anabainisha Waziri Mkuu Pinda.

The post Wauguzi Tanzania Waadhimisha Siku yao huku Wakiyaenzi Matatizo Lukuki appeared first on Fikra Pevu.


Watoto Njiti 40 Wazaliwa Biharamulo ndani ya Miezi Sita

$
0
0

Wakati Tanzania ikitajwa kuwa nchi ya 12 duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya kufikisha majuma 37 (Njiti), sawa na miezi tisa ya mtoto kukaa tumboni, takriban watoto zaidi 40 wa aina hiyo wamezaliwa katika Wilaya ya Biharamulo, Kagera, katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Akizungumza na FikraPevu hivi karibuni, Mganga Mkuu wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo (DDH), Dk. Grasmus Sebuyoya, anasema watoto hao njiti wamezaliwa katika kipindi cha kati ya Juni  na Desemba mwaka jana 2014.

Alizitaja baadhi ya sababu zinazochangia kuongezeka kwa watoto njiti katika wilaya hiyo, ni wajawazito kutohudhuria kikamilifu kliniki, unywaji wa baadhi ya dawa za kuongeza uchungu, kufanya kazi nyingi na nzito hasa kina mama wa vijijini, ugonjwa wa malaria pamoja na magonjwa ya ngono.

Kwa upande wake, Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali hiyo, Lena Nchonchona, alisema elimu kwa wajawazito na jamii kwa ujumla kwa wananchi wa Wilaya ya Biharamulo, bado inahitajika kwa kuwa baadhi ya wajawazito huanzia kwa waganga wa jadi na inaposhindikana huko ndiyo wanakwenda hospitali, huku wakiwa tayari wameathiri mfumo wa uzazi na kiumbe kilichomo tumboni.

Kwa mujibu wa Nchonchona, licha ya wataalam wa afya kuwahamasisha wananchi wa wilaya hiyo kwa kutumia njia ya Kangaroo (ngozi kwa ngozi) kuokoa maisha ya watoto njiti, hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa maalum vya kuwatunzia watoto hao pindi wanapozaliwa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Dk. Tumpale Akimu, ameiambia FikraPevu kwamba ili kunusuru vifo vya watoto njiti, hospitali yake imetenga chumba maalum ambacho kimeongezwa taa maalum zenye joto kwa ajili ya kulelea watoto hao.

"Hatua hiyo imetusaidia sana kunusuru maisha ya watoto njiti kwa maana chumba hiki kina joto la kutosha. Hata hivyo, changamoto kubwa ni jinsi ya kuishi hapa wazazi wa watoto hao kwa kuwa baadhi yao hawana ndugu wanaoishi karibu kwa ajili ya kuwahudumia chakula na mahitaji mengine muhimu," anasema Dk. Akimu.

Takwimu rasmi zilizopo, zinaonyesha kwamba takriban watoto njiti 213,500, huzaliwa kila mwaka nchini, kati yao watoto 9,400 wakielezwa kufariki dunia mara tu baada ya kuzaliwa.

The post Watoto Njiti 40 Wazaliwa Biharamulo ndani ya Miezi Sita appeared first on Fikra Pevu.

Fahamu Chanzo na Dalili za Uvimbe wa Tezi za Uzazi kwa Wanawake na Tiba yake

$
0
0

Wanawake wengi wamekuwa na tatizo la kutoshika ujauzito, lakini bila ya kujua sababu yake pia ni nini. Moja ya sababu ya kutoshika ujauzito, ni ugonjwa wa Sisti au Nziba unaopatikana kwenye Ovari za uzazi (Ovarian Cyst).

Ili kuweza kuuelewa vyema ugonjwa huu, inatubidi kwanza kuelewa maana ya Ovari. Ovari ni moja ya pea za tezi za uzazi kwa mwanamke zilizo katika pango la nyonga, kila tezi ikiwa imejishikiza upande mmoja wa uterasi (Uterus). Uterasi ni nini? Hii ni ogani ambayo utungo wa mimba hupokelewa na kustawishwa.

Kwa hiyo, kazi kubwa ya Ovari ni kutengeneza mayai ya mwanamke (Ova) na homoni za kike ziitwazo Istrojeni (Estrogen) na projesteroni (Progesterone). Kwa kawaida, Ovari ndicho chanzo kikubwa cha homoni za kike zinazoongoza ukuaji wa sifa za msichana kama matiti, umbo la mwili na nywele za mwilini. Aidha, homoni hufanya kazi ya kurekebisha mzunguko wa hedhi na mimba. Sasa basi, uvimbe kwenye tezi za uzazi za mwanamke (Ovari), hutokana na mkusanyiko wa majimaji au ute mzito unaozungukwa na kuta nyembamba ndani ya tezi za uzazi za mwanamke (Ovari).

Uvimbe huu ambao hupatikana ndani ya tezi za uzazi za mwanamke, ndio unaojulikana kitaalam kama Sisti kwenye Ovari hiyo. Uvimbe huu hutokea kwa wanawake wa umri wowote ule, na mara nyingi huonekana kwa wanawake waliofikia kikomo cha umri wa kupata ujauzito.

Tezi za uzazi za mwanamke, ni nini? Kwa kawaida, mwanamke anakuwa na tezi mbili katika mwili wake. Tezi moja upande wa kulia na tezi nyingine upande wa kushoto. Tezi hizi, hupatikana pembezoni mwa mfuko wa uzazi (Uterasi).

Watafiti wa mambo ya uzazi, wanasema tezi za uzazi za mwanamke huanza kuzalisha mayai ya uzazi yanayojulikana kitaalamu kama Ova, na mayai hayo ya uzazi hukua ndani ya tezi za uzazi ya mwanamke (Ovari) kwa kuchochewa na baadhi ya homoni, katikati ya mwezi, kwa maana ya siku ya 14, na huweza kudumu kwa muda wa kati ya saa 24-36.

Baada ya kiwango cha kichocheo/homoni ya ulutenishaji (Luteinizing Hormone) kuwa juu, mayai ya uzazi hutolewa katika kila Ovari. Kitendohiki hujulikana kama Uovuleshaji (Ovulation) au kufikia kilele cha upevukaji wa mayai. Mayai haya ya uzazi huishi kwa saa chache mno, wa hadi saa 24, ikiwa hayatorutubishwa na mbegu (Sperms) kutoka kwa mwanamme.

Shirika la Habari la Tehran, limesema kwamba: "Mabaki ya mfuko wa mayai ya uzazi yanayojulikana kama Foliko ya Graaf (Graafian Follicle) ndani ya Ovari, hugeuka na kuwa Kopasi Luteamu (Corpus Luteum) ambao huhusika na utoaji wa kichocheo au homoni aina ya Projesteroni (Progesterone) kwa wingi. Homoni hii ya Projesteroni (Progesterone), ndiyo inayosababisha mfuko wa uzazi kujiandaa kwa kujikita yai (Implantation) lililorutubishwa kwa mbegu ya kiume ndani ya mfuko wa uzazi kwa kuongeza unene kwenye kuta zake."

Yai hili husafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi ambako hukua na kuwa mtoto. Kama upachikwaji wa yai liliorutubishwa hautafanyika, basi ndani ya wiki mbili, Kopasi Luteamu (Corpus Luteum) huanza kusinyaa na kupotea na kusababisha kushuka kwa kiwango cha homoni aina ya Projesteroni (Progesterone) na Istrojeni (Estrogen).

Kushuka kwa viwango vya vichocheo hivi ndio husababisha mfuko wa uzazi kuanza kutoa mabaki ya kuta zake pamoja na yai la uzazi na hii ndiyo pale mwanamke anapotoka damu ukeni inayojulikana kama Hedhi (Menstrual Cycle). Unaweza ukajiuliza, ni kwa nini nimeanza na maelezo haya, lakini jibu ni kutaka kuonyesha umuhimu wa mayai ya uzazi kwa mwanamke pamoja na kazi yake.
Aina za Sisti/Nziba kwenye Ovari Kwa mujibu wa watafiti wa masuala ya kiafya na kisayansi, kuna aina nyingi za uvimbe kwenye tezi za uzazi za mwanamke. Hata hivyo, aina saba hizi ndizo huonekana sana kwa wanawake wengi.

Kwanza, ni Sisti/Nziba inayopatikana kwenye Foliko (Follicular Cyst). Huu ni uvimbe ambao hutokea wakati Uovuleshaji (Ovulation) usipotokea au baada ya Kopasi Leteamu (Corpus Luteum) kuanza kusinyaa na kupotea yenyewe baada ya kutopachikwa kwa yai kwenye kuta za mfuko wa kizazi.

Uvimbe huu unakuwa na wastani wa inchi 2.3 kwa upana. Upasukaji wa uvimbe huu husababisha maumivu makali katikati ya mzunguko wa hedhi, kwa maana ya siku ya Uovuleshaji (Ovulation). Maumivu haya huonekana kwa robo ya wanawake wenye aina hii ya uvimbe. Kwa kawaida, uvimbe huu hauna dalili zozote za wazi, na hupotea wenyewe baada ya miezi kadhaa.

Pili ni Sisti/Nziba inayokuwa kwenye Kopasi Luteamu (Corpus Luteum Cyst). Huu ni uvimbe unaotokana na kutopachikwa kwa yai la uzazi lililorutubishwa na mbegu ya kiume kwenye mfuko wa kizazi.

Kwa kawaida Kopasi Luteamu (Corpus Luteum) husinyaa na kupoteay enyewe, au wakati mwingine inaweza ikajaa maji, hivyo kusababisha uvimbe wa aina hii. Uvimbe huu huonekana kwenye upande mmoja (kushoto au kulia) wa mwanamke na hauna dalili zozote zile.

Tatu, ni Sisti/Nziba yenye kutoa damu (Hemorrhagic Cyst). Huu ni uvimbe unaotokea wakati kukiwa na uvujaji wa damu ndani ya uvimbe wa aina yoyote ule, ambao umeshajitengeneza tayari. Huambatana na maumivu makali kwenye upande mmoja wa ubavu wa mwanamke (kushoto au kulia).

Nne, ni Sisti/Nziba ya Demoidi (Dermoid Cyst). Hii ni tyuma ya kiteratoma yenye kujumuisha viundwa vitokanavyo na ektodemu. Uvimbe huu ambao si saratani, hujulikana pia kama Teratoma kubwa yenye Sisti/Nziba (Mature Cystic Teratoma).

Aina hii huathiri wanawake wadogo walio katika umri wa kushika mimba, na huweza kukua na kufikia inchi sita (6) kwa upana na ndani yake huweza kuwa na mchanganyiko wa nywele, mfupa, mafuta na gegedu (Cartilage).

Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa zaidi au kujizungusha, hivyo kuathiri usambazaji wa damu kwenda kwenye uvimbe huu na kwa hiyo kusababisha maumivu makali maeneo ya tumboni. Tano, ni Sisti nyingi (Polycysitic appearing Cyst). Uvimbe wa aina hii unakuwa ni mkubwa sana, na huwa umezungukwa na vijivimbe vyengine vidogo vidogo na huonekana hata kwa wanawake wenye afya njema au wale wenye matatizo ya homoni.

Sita, ni Adenoma yenye Sisti (Cystadenoma). Hii ni aina ya uvimbe unaotoka kwenye tishu za Ovari, na hujazwa na majimaji yenye kuvutika. Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa sana hata kufikia inchi 12 auz aidi kwa upana. Saba, ni Sisti kwenye Endometria (Endometriomas/Endometrial Cyst).

Uvimbe huu husababishwa na uwepo wa aina mojawapo ya kuta za mfuko wa kizazi unaojulikana kama Endometria (Endometrium) kwenye mayai ya mwanamke. Aina hii huathiri wanawake waliofikia kikomo cha umri wa kupata ujauzito, na huambatana na maumivu sugu ya nyonga wakati wa hedhi. Uvimbe huu unakuwa na damu ya rangi nyekundu inayoelekea kuwa kahawia
na ukubwa wake ni kuanzia inchi 0.75 hadi 0.8. 

Ni nini chanzo cha uvimbe kwenye tezi za uzazi za mwanamke? Vihatarishi vikuu vya tatizo la uvimbe kwenye tezi za uzazi za mwanamke, kwanza ni historia ya awali ya Sisti/Nziba kwenye Ovari (Ovarian Cyst). Kwa kawaida, wanawake ambao wazazi wao au watu wao wa karibu wamekuwa wakisumbuliwa na ugonjwa huo, wanakuwa kwenye
uwezekano mkubwa wa kupatwa na tatizo hilo.

Sababu nyingine inayoweza kusababisha uvimbe katika Ovari za mwanamke ni kuwa na mzunguko wa hedhi usiokuwa na mpangilio maalum au kama tunavyouita kwa kimombo, Irregular Menstruation Cycle. Kihatarishi kingine ni kuwa na mafuta mengi kwenye sehemu ya juu ya mwili. Tatizo hili mara nyingi linawapata wanawake wanene.

Ugumba na kuvunja ungo au kubaleghe mapema, ni sababu nyingine. Mtoto wa kike anapobaleghe akiwa na umri wa miaka kwa mfano 11 au chini ya hapo, huweza kupatwa na uvimbe katika Ovari zake. Aidha, kukosekana uwiano sawa wa vichocheo au homoni mwilini au ugonjwa wa hypothyroidism na pia dawa ya kutibu saratani ya matiti ya Tamoxifen, husababisha tatizo hilo.

Itaendelea katika makala za FikraPevu zijazo.

 

The post Fahamu Chanzo na Dalili za Uvimbe wa Tezi za Uzazi kwa Wanawake na Tiba yake appeared first on Fikra Pevu.

Dalili za Ugonjwa wa Uvimbe wa Tezi za Uzazi kwa Wanawake na Tiba yake (2)

$
0
0

Katika makala iliyopita ambayo ni (sehemu ya kwanza) tulijadili namna wanawake wengi wanavyoteseka na tatizo la kutoshika ujauzito bila ya kujua sababu yake pia ni nini. Moja ya sababu ya kutoshika ujauzito, ni ugonjwa wa Sisti au Nziba unaopatikana kwenye Ovari za uzazi (Ovarian Cyst). Katika makala haya ya sehemu ya pili tutaangazia tena dalili na viashiria vya kwanza kabisa vya ugonjwa huu wa Sisti/Nziba.

Dalili na viashiria vya kwanza kabisa vya ugonjwa wa Sisti/Nziba kwenye Tezi za Uzazi za Mwanamke ni maumivu makali ambayo hayana mwanzo maalum na yanayochoma, ambapo maumivu hayo yanaweza yakawa yanakuja na kupotea au yakawepo moja kwa moja.

Lakini pia, mwanamke anaweza kupata usumbufu na kutojisikia vizuri kwenye maeneo ya chini ya kitovu, kwenye nyonga, uke, kwenye mapaja na mgongoni upande wa chini kiunoni.

Dalili nyingine ni maumivu ya muda mrefu kwenye nyonga wakati mwanamke anapokuwa kwenye siku zake, maumivu ambayo huweza kuhisiwa sehemu ya kiunoni. Kwa kawaida mumivu haya yanaweza kuanza muda mfupi tu baada ya kuanza hedhi, wakati wa hedhi au mwisho wa hedhi.

Maumivu ya nyonga baada ya kufanya kazi ngumu, mazoezi au baada ya kujamiiana. Kuhisi kichefuchefu, kutapika na kutokwa na matone ya damu ukeni.

Ugumba na kuhisi uchovu, mabadiliko ya haja ndogo, yaani kukojoa mara kwa mara, kujikojolea au kushindwa kutoa mkojo wote kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kupata haja ndogo.

Mabadiliko ya haja kubwa, kwa maana ya kupata haja kubwa kwa shida sana kutokana na presha kwenye maeneo ya nyonga; nywele kukua kwa kasi na kuongezeka kuota kwa nywele kwenye uso au sehemu nyingine za mwili.

kuumwa kichwa, kuongezeka uzito, maumivu ya kwenye mbavu, kutokewa na uvimbe chini ya ngozi na kuvimba mara kwa mara; maumivu kwenye matiti na kuapata hedhi isiyokuwa na mpangilio maalumu na kuhisi tumbo kuwa zito, kujaa au kuvimba.

Mwanamke mwenye dalili na viashiria hivi afanye nini?

Kwanza kabisa ni kufanyiwa kipimo cha mawimbi ya sauti ndani ya uke (Endovaginal Ultrasound). ambacho hufanywa kwa kuingiza mpira maalum kupitia ukeni na kuangalia mfuko wa uzazi na mayai ya mwanamke.

Kwa kutumia kipimo hiki, ni rahisi kwa daktari kugundua kama kuna uvimbe wowote kwenye Ovari na uvimbe huo ni wa aina gani au atajua kama ni maji tu (Fluid filled sac), au ni maji pamoja na mchanganyiko wa ute mzito, au ni ute mzito pekee.

Kipimo kingine kinachoweza kuchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi ni kipimo cha mawimbi ya sauti kutoka kwenye nyonga hadi kwenye fumbatio (Pelvic Abdominal Ultrasound) ambayo ni Ultrasound ya kawaida. Hii husaidia kujua aina ya uvimbe uliopo kwenye tezi za uzazi (Ovari) za mwanamke.

Vipimo vingine vinavyoweza kuonyesha uvimbe kwenye Ovari ni pamoja na Computerized Tomography (CT) Scan na Magnetic Resonance Imaging (MRI) Scan.

Matibabu ya Ugonjwa wa Tezi za Uzazi za Mwanamke Matibabu ya Sisti/Nziba kwenye Ovari yanategemea sana umri, aina na
ukubwa wa uvimbe pamoja na dalili anazohisi mgonjwa. Mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia vidonge vya uzazi wa mpango ili kupunguza hatari ya kupata Sisti/Nziba kwenye Ovari.

Ni muhimu kufahamu kwamba vidonge vya uzazi wa mpango, mbali na kuzuia upatikanaji wa mimba zisizokuwa na mpango, hupunguza pia hatari ya kupata Kansa au Saratani kwenye Ovari za Uzazi wa Mwanamke.

Kwa hiyo, matiba ya magonjwa haya yanaweza kuhusisha vipimo vya damu kama CA-125 ili kuangalia uvimbe huo kama ni Saratani au ni uvimbe wa kawaida tu. Uvimbe kama haupungui na unasababisha maumivu makali sana, mgonjwa anaweza kushauriwa kufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo.

Kama mgonjwa atalazimika kufanyiwa upasuaji, uvimbe uliotolewa unaweza kupelekwa kwa mtaalam wa Patholojia kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kupata bainisho la mwisho la ugonjwa (Final Diagnosis).

Endapo uchunguzi utaonyesha kwamba uvimbe huo ni wa Saratani, basi Daktari atamshauri mgonjwa kutolewa kwa viungo vyote vya uzazi (Total Hysterectomy) ili kuzuia Saratani kutosambaa kwenye viungo vingine.

The post Dalili za Ugonjwa wa Uvimbe wa Tezi za Uzazi kwa Wanawake na Tiba yake (2) appeared first on Fikra Pevu.

Yafahamu Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, Chanzo chake na jinsi Kuishi nayo

$
0
0

Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa ni magonjwa yanayoathiri njia za hewa pamoja na sehemu nyingine zinazohusiana na mapafu, kama vile magonjwa ya Pumu, Kufungana kwa njia za pumzi (Chronic Obstructive Pulmonary Disease-COPD), ugonjwa wa mapafu unaotokana na kazi (Occupational Lung Disease), kupanda kwa shinikizo la damu kwenye Mapafu (Pulmonary Hypertension) na kadhalika.

Magonjwa haya, mara nyingi huathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa hewa na kuzuia kiasi cha hewa inayotoka na kuingia kwenye mapafu, kwa mfano ugonjwa wa Pumu. Hali hii humfanya mgonjwa apumue au kuvuta hewa kwa shida, hasa pale anapokuwa mgonjwa. Magonjwa haya huweza kusababisha kuwepo kwa makohozi katika njia ya hewa, hivyo kusababisha maambukizi mengine.

Kulingana na takwimu ambazo FikraPevu imezipata kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni 235 duniani kote wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa Pumu, huku watu milioni 64 wakitajwa kusumbuliwa na magonjwa sugu ya kufungamana kwa njia ya Pumzi (COPD). Kwa mujibu wa WHO, takriban asilimia 90 ya vifo vinavyotoakana na magonjwa hayo, hutokea katika nchi zilizo na uchumi duni na wa kati, Tanzania ikiwa mojawapo.

Watu wengi hudhani kwamba mtu anapokuwa mwembamba kupita kiasi na akawa na uzito kidogo, basi mtu huyo atakuwa na ugonjwa wa Ukimwi. Wanaodhani hivyo, hawajui kwamba magonjwa sugu ya njia ya hewa, nayo yanaweza kumsababishia mtu akakonda na kupungua uzito pia.

Hali hiyo hutokea kutokana na ukweli kuwa magonjwa hayo ya njia ya hewa, humfanya mgonjwa atumie nguvu nyingi wakati wa kupumua kuliko mtu asiyekuwa na magonjwa hayo.

Matumizi makubwa ya nguvu wakati wa kupumua, humfanya mgonjwa asiwe na nishati ya akiba ambayo huhifadhiwa mwilini, hivyo kufanya mtu kuwa mnene. Lakini pia unene uliokithiri, unaweza kusababisha magonjwa mugu ya njia ya hewa.

Ni nini chanzo cha magonjwa sugu ya njia ya hewa?

Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, mara nyingi husababishwa na kuharibika kwa njia ya hewa katika mapafu. Uharibifu huo wa njia ya hewa huweza kutokana na uvutaji wa sigara na matumizi ya ugolo; kuvuta hewa yenye sumu au vumbi kutoka viwandani, uchafuzi wa hewa ya ndani mfano kwa kutumia jiko la utambi na mafuta ya taa; uchafuzi wa hewa ya nje kutokana na vumbi au poleni ya maua na unene uliokithiri kiwango.

Anayesumbuliwa na ugonjwa sugu wa njia ya hewa azingatie nini ili aweze kuishi?

Mgonjwa wa ugonjwa sugu wa njia ya hewa anashauriwa kuzingatia ushauri wa daktari na matibabu yake, kufuata kanuni za mtindo bora wa maisha, kuepuka visababishi kama vile vumbi, barafu na harufu, kuhakikisha mazingira na nyumba anaoishi ni safi muda wote, na zaidi pia iwe na madirisha yanayoruhusu mzunguko wa hewa.

Aidha, wagonjwa wa magonjwa hayo wanashauriwa kula mlo kamili na vyakula vya aina mbalimbali ili wapate virutubishi vyote vinavyohitajika kwa afya zao. Inashauriwa kula zaidi matunda freshi, mbogamboga zenye rangi ya kijani, matunda yenye rangi ya njano kama vile ndizi, papai, embe, mapera na kadhalika.

Lakini pia, wanashauriwa kula vyakula vyenye makapi mlo kwa wingi ili kusaidia mfumo wa kusaga chakula kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa uchafu tumboni kwa urahisi. Hali hii huwasaidia kuweza kupumua kwa urahisi.

Ikumbukwe kuwa mgonjwa wa aina hiyo anatumia nguvu nyingi wakati wa kupumua, hivyo basi anahitaji kula chakula cha kutosha ili kumpatia nguvu za kutosha. Ni vizuri kula milo midogo midogo mara kwa mara, ikiwa ni pamoja nakupunguza matumizi ya chumvi ili kuepuka maji kujikusanya mwilini na kusababisha kupumua kwa shida. Ni muhimu pia kuepuka uzito uliozidi kwa sababu unene huongeza tatizo la kupumua.

Je, mgonjwa wa mugonjwa sugu wa njia ya hewa anaruhusiwa kufanya mazoezi?

Mazoezi ya mwili yana faida nyingi kiafya. Baadhi ya faida hizo ni kuimarisha mapafu na moyo. Ili kuviwezesha viungo hivyo muhimu katika mwili wa mwanadamu vifanye kazi kwa ufanisi, mazoezi ni muhimu sana. Aidha, mazoezi husaidia kuimarisha misuli ambayo hutumika wakati wa kupumua.

Kwa hiyo, mgonjwa wa magonjwa sugu ya hewa anaruhusiwa kufanya mazoezi kwa sababu mazoezi ni sehemu ya matibabu yake. Mgonjwa anapaswa kujitahidi mara kwa mara kufanya mazoezi, kwa kuanza mazoezi ya taratibu kwa kadri mwili wake unavyoweza kustahimili, na kisha kuongeza hatua kwa hatua.

Hata hivyo, inashauriwa mgonjwa anayefanya mazoezi, pindi asikiapo maumivu kifuani au kushindwa kuhimili mazoezi hayo, punguza kasi ya mazoezi hayo na fanya kwa taratibu kadri iwezekanavyo.

The post Yafahamu Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, Chanzo chake na jinsi Kuishi nayo appeared first on Fikra Pevu.

HATARI: Vimelea vipya vya Kisonono Visivyotibika kama Virusi vya Ukimwi vyagundulika

$
0
0

WAKATI dunia ikipalangana kutafuta dawa ya kutibu ugonjwa wa Ukimwi, imeripotiwa kubainika kwa vimelea vipya vya ugonjwa wa Kisonono, ambavyo havisikii dawa za ugonjwa huo zilizokuwa zimezoeleka ulimwenguni kama tiba sahihi ya maradhi hayo, hivyo ugonjwa huo sasa sasa kutajwa kuwa hatari sawa na Ukimwi.

Taarifa mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inaeleza kwamba kuna aina mpya vimelea vya ugonjwa wa kisonono vinavyoendelea kusambaa kwa kasi duniani, ambavyo vinahimili dawa zilizokuwa zinatumika kutibu ugonjwa bila kudhulika.

Kwa mujibu wa WHO, vimelea hivyo vipya havisikii dawa, hivyo baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika huko nyuma, zimekuwa hazina tena athari kwa vijidudu vipya hivyo.

Tayari nchi nyingi duniani zimeripotiwa kukumbwa na usungu wa kisonono hata pale mgonjwa anapopatiwa tiba sahihi ya Antibiotiki (Viuasumu) za jamii ya Sefalosporini na kadhalika, zikiwemo Hongkong, Australia, Ufaransa, Japan, Norway, Sweden na Uingereza.

Aina hii mpya ya vimelea vya kisonono vinadaiwa kuonyesha usugu dhidi ya dawa zote za Antibiotiki zinazotumiwa kuviangamiza, zikiwemo dawa hizo za jamii ya Sefalosporini, ambazo WHO inazitaja kama dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono.

Dk. Manjula Lusti-Narasimhan, kutoka Kitengo cha Afya ya Uzazi na Utafiti cha WHO, amekaririwa na FikraPevu akisema: “Kwa mara ya kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidi ya Antibiotiki (Viuavijasumu) jamii ya Sefalosporini viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na Uingereza, Hongkong na Norway."

Daktari huyo hakukomea hapo, bali anasema katika miaka michache ijayo, aina hii mpya ya vimelea vya ugonjwa wa kisonono, huenda ikawa sugu kwa dawa zote ambazo zinapatikana kwa sasa ulimwenguni. Dk. Manjula anasema: “Ugonjwa sugu wa kisonono si tatizo la Bara la Ulaya au Afrika pekee, bali ni tatizo la dunia nzima. Lazima tahadhari zichukuliwe mapema. Upo uwezekano wa vimelea hivi sugu vya kisonono kusambaa kwa haraka duniani kote bila kugundulika. Hii inatokana na nchi nyingi kutokuwa na ufuatiliaji na utunzaji kumbukumbu mzuri wa wagonjwa wake.”

Baadhi ya Wanasayansi wa magonjwa hayo ya zinaaa wanaamini kwamba matumizi holela ya dawa aina ya Antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya ugonjwa huo kubadilika na kuzoea mazingira mapya, ndicho chanzo kikuu cha ugonjwa huo kwa sasa kuwa sugu.

Kwa mujibu wa wanasansi hao, ugonjwa wa kisonono ambacho si sugu kilicho kwenye shingo ya kizazi (Cervix), Urethra na Puru, hutibiwa kwa Antibiotiki (Kiuavijasumu) jamii ya Sefalosporini, ambapo mgonjwa hupewa dozi moja ya dawa hizo pamoja na dawa aina ya Macrolide kama vile Azithromycin, na za jamii ya Penicillin kama vile Doxycyclin kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Chlamydia.

Mara nyingi kwa wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa sindano. Mgonjwa lazima afuate masharti na ushauri wa daktari kabla hajatumia dawa hizo, kwa kuwa dawa nyingi huwa na madhara kwa wajawazito kwa mfano Doxycyclin.

“Kawaida ushauri nasaha hutolewa kwa washirika wote wawili wa ngono. Na ni vizuri wote wawili watibiwe hata kama mmoja wao hatakuwa na dalili za ugonjwa huu wa kisonono,” wanasema Watafiti na Wanasayansi kuhusu tiba sahihi ya ugonjwa huo.

Namna ya kujikinga na ugonjwa huo mpya wa kisonono

Utafiti wa wanasayansi waliobobea katika magonjwa ya binadamu, wanasema kwamba mtu anaweza kujikinga na ugonjwa wa kisonono kwa kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha vitendo vya zinaa na uasherati. Aidha, mtu anaweza kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuchukua tahadhari na kuzungumzia juu ya ugonjwa huo kwa mshirika wake wa ngono pindi mmoja wapo anapojibaini kuwa na hali yenye dalili zote za ugonjwa ili wote kwa pamoja waweze kutibiwa na kupata ushauri wa daktari mapema.

Njia nyingine ya kujikinga ni kuepuka kufanya ngono na mtu aliyeambukizwa gono au kujenga tabia ya kutumia mipira ya kiume (Kondomu) wakati wa kujamiiana. Kwa upande wa wanawake wajawazito ni muhimu kuhudhuria kliniki mapema ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa tiba muafaka iwapo watagundulika kuwa na ugonjwa huo wa zinaa au ugonjwa mwingine wowote.

Kwa mujibu wa WHO, wanawake wajawazito wanatakiwa wajifungulie katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ili kama watoto wanaozaliwa watabainika kuathirika kwa ugonjwa huo wa kisonono waweze kupata matibabu ya mapema mara tu baada ya kuzaliwa hivyo kuwaepusha na uwezekano wa kupata upofu.

Kutokana na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo mpya wa kisonono, kila nchi duniani, kupitia Serikali zao na madaktari wao, zinapaswa kuongeza umakini katika ufuatiliaji wa aina hii mpya ya ugonjwa wa kisonono kwa sababu ugonjwa huo una madhara makubwa kwa afya ya binadamu kama vile kusababisha ugumba kwa wanawake, utasa kwa wanaume, upofu, moyo, uvimbe, ubongo na homa ya mapafu.

Takwimu zilizopo kutoka WHO, zinaonyesha kwamba kisonono ni ugonjwa hatari kwa usalama wa binadamu, hivyo muda si mrefu ugonjwa huo unaweza kutangazwa kama moja ya majanga makubwa ya dunia, kama hatua madhubuti na haraka hazitachukuliwa kwa kila nchi. Kutokana na hali hiyo, WHO imezitaka nchi zote duniani kuongeza ufuatiliaji wa wagonjwa wake, pamoja na kudhibiti matumizi holela ya dawa za Antibiotiki hadi pale taarifa kamili za ugonjwa huo zitakapojulikana.

The post HATARI: Vimelea vipya vya Kisonono Visivyotibika kama Virusi vya Ukimwi vyagundulika appeared first on Fikra Pevu.

Yafahamu mambo muhimu ambayo Mwanamke anatakiwa Kufanyia Uchunguzi wa Kiafya

$
0
0

KWA jinsi maisha ya sasa yalivyo na pilikapilika nyingi za kujitafutia riziki, wakati mwingine hata mtu kupata muda wa kumuona daktari akiwa haumwi sana, mara nyingi inakuwa ni vigumu.

Hata hivyo mwili wa binadamu ni sawa na mashine inayofanya kazi nyingi, hivyo ili mwili huo uweze kufanya kazi vizuri, unahitaji matunzo, ikiwemo uchunguzi wa mara kwa mara wa kiafya ili kuhakikisha ubora na uimara wa mwili wenyewe.

Uchunguzi wa afya kwa ukawaida ni muhimu kwa wanawake wote bila kuzingatia umri hata kama huna dalili za ugonjwa wowote.
Makala haya ya FikraPevu, kama mada inavyojieleza, yanahusu Mambo Muhimu ya Kufanyia Uchunguzi wa Kiafya kwa Mwanamke, pindi kina mama wanapotaka kufanyia uchunguzi wa afya ya mwili kiujumla.

Hayo ni pamoja na magonjwa ya klamidia, maambukizi ya VVU, moyo, kiwango cha kolesteroli, kisukari, utendaji wa viungo vikubwa vya mwili, osteoporosisi (aina ya kusinyaa kwa mifupa ya sehemu moja au mifupa yote miwili ambapo tishu ya mfupa hupotea lakini bila ya kuathiri muundo wa mfupa mzima) pamoja na saratani za aina mbalimbali, hasa zilizozoeleka kama vile saratani ya Ini, utumbo mpana na ya shingo ya kizazi.

Katika kufanyia uchunguzi maeneo hayo, Daktari huoanisha maelezo yanayotolewa na mtu anayefanyiwa uchunguzi kuhusu dalili zilizomsukuma kuhitaji kufanyiwa uchunguzi; historia yake ya nyuma kiafya; staili ya maisha, hasa ulaji wa vyakula; umri wa mhusika, historia ya familia yake kiafya; shughuli anazofanya na kama anatumia bidhaa za tumbaku kama vile sigara pamoja na unywaji wa pombe.

Wakati wa kuchunguza afya ya mwanamke daktari anaweza kumwomba mteja wake afunue baadhi ya maungo yake ya mwili au kuvua nguo kabisa ili kufanya uchunguzi vizuri. Vitu vinavyoweza kufanyika ni pamoja na kuchukua sampuli kwa pamba kutoka kwenye via vya uzazi au seviksi pamoja na kuchunguza sehemu za nje za via hiyo, sampuli ya mkojo na sampuli ya damu.

Aina ya vyakula vinavyotumiwa mara nyingi katika maisha ya siku hizi pamoja na aina ya mafuta yanayotumika kupikia vyakula, vinamuweka binadamu katika hatari ya ongezeko la kiwango cha kolesteroli kwenye damu, kinachoweza kusababisha magonjwa ya Moyo, hivyo ni muhimu kupima kiwango cha kolesteroli kama kiko katika hali ya kawaida au kimezidi. Klamidia ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria waitwao kitalamu kwa jina la Klamidia, hivyo magonjwa haya yanapaswa kupimwa kwa kutumia kipimo cha Klamidia, ambacho wanawake wanaojali afya zao hufanyiwa uchunguzi walau mara moja kila mwaka kuanzia kipindi cha kuanza balehe.

Ni muhimu pia mwanamke anapofanyiwa uchunguzi wa afya ya mwili wake, akapima pia kama anaambukizi ya VVU pamoja na magonjwa mengine ya zinaa, kama vile kisonono, kaswende pamoja na virusi vya Human Papilloma Virusi (HPV). HPV ni ugonjwa wa zinaa ambao huwapata wanawake wengi zaidi ulimwenguni. Hasa nchi za ulimwengu wa tatu, Tanzania kiwemo. Chanzo kikuu cha ugonjwa huu ni saratani ya mlango wa tumbo la uzazi.

Kwa hiyo, inashauriwa mwanamke yeyote mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kufanyiwa kipimo cha Pap (Pap Smear) kila baada ya miaka mitatu, ili kubaini mapema kama ana tatizo lolote katika mlango wa tumbo la uzazi. Hata hivyo, inashauriwa kwa wanawake wenye umri wa miaka 30 na kuendelea, kufanya kipimo hicho cha Pap pamoja na cha HPV kila baada ya miaka mitano. Mara nyingi, kipimo hicho cha Pap huhusisha uchunguzi wa chembe za seviksi (mlango wa tumbo la uzazi), ambazo huchukuliwa na madaktari kwa kutumia kijiko kidogo au brashi maalumu.

Ili kuchunguza sehemu za ndani za uzazi, Daktari anaingiza vidole vya mkono kwenye njia ya uzazi, huku mkono mkono mwingine akiwa ameshika tumbo ili kuhisi ovari au glandi za uzazi za mwanamke vinavyotoa yai pamoja na uterazi/kizazi (ogani ambamo utungo wa mimba hupokelewa na kustawishwa).

Endapo Daktari atahisi kitu kisicho cha kawaida kama vile uvimbe wa aina yoyote, atatoa ushauri wa vipimo gani vifanywe, kama vile Ultrasound, kwa ajili ya kubaini tatizo ili kuchukua hatua za matibabu mapema. Mwanamke anatakiwa pia kufanyiwa uchunguzi wa Matiti kwa kutumia Mamografi. Uchunguzi wa matiti kwa mamografi unahusisha X-ray ya tishu laini za matiti ili kuchunguza matiti kama yana uvimbe au saratani baada ya Daktari kuchunguza kwa njia ya kupapasa kwa mkono ili kuhisi uvimbe wowote.
Ikiwa kuna saratani yoyote iliyobinika, mgonjwa anaweza kushauriwa kukata titi/matiti ili kuzuia saratani kusambaa mwili mzima, la kama utakuwa ni uvimbe wa jipu tu, mgonjwa hukamliwa usaha na kupewa antibiotiki (kiuavijasumu).

Osteoporosisi ni ugonjwa wa kusinyaa kwa mifupa ya sehemu moja au mifupa yote ya miwili bila ya kuathiri muundo wa mfupa mzima. Mwanamke anapawa kufanya kipimo cha osteoporosisi walau mara moja kwa mwaka, hasa anapofikia umri wa kuanzia miaka 65. Huu ni ugonjwa ambao mtu anaweza kuupata kwa njia ya kurithi kutoka kwenye familia au akaupata kutokana na mwenendo wake wa maisha kama vile uvutaji wa sigara, kukoma kwa hedhi na kadhalika.

Aidha, mwanamke anashauriwa kufanyiwa uchunguzi wa Shinikizo la Damu kila mara anapotembelea kituo cha kutolea huduma za afya, hasa kwa kina mama wajawazito au kwa kina mama wenye umri wa zaidi ya miaka 35.

Viwango vya shinikizo la damu vinatofautiana kulingana na umri wa mwanamke pamoja na hali ya ujauzito. Kupima mara kwa mara kipimo cha shinikizo la damu, kunasaidia kufahamu kiwango cha kawaida na kisicho cha kawaida.

The post Yafahamu mambo muhimu ambayo Mwanamke anatakiwa Kufanyia Uchunguzi wa Kiafya appeared first on Fikra Pevu.

Mamlaka zinazosimamia Sheria ya Kudhibiti Uvutaji Sigara hadharani, zimekwenda Likizo?

$
0
0

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Sheria ya Kudhibiti Uvutaji wa Sigara kwenye ofisi za umma pamoja na kwenye mikusanyiko wa watu. Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge mwaka 2003 ili pamoja na mambo mengine, ikilenga kuhakikisha kwamba watu hawapati madhara yatokanayo na moshi wa sigara au matumizi ya tumbaku kutokana.

Jina la sheria hiyo ya afya, inaitwa Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL, ya mwaka 2003. Kipengele cha 12(1) cha sheria hiyo, kinapiga marufuku matumizi ya bidhaa yoyote ya tumbakuh katika maeneo ya umma.

Kutokana na kuwepo kwa sheria hiyo, wananchi wote wanaotumia bidhaa za tumbaku, wanatakiwa kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya bidhaa hiyo, ikiwa ni pamoja na kuhimiza umuhimu wa kutolewa elimu kwa jamii nzima ili kujua madhara ya matumizi ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia uvutaji katika maeneo ya umma. Uvutaji sigara ulianza kupigwa marufuku kwa mara ya kwanza na Kanisa Katoliki mwaka 1,575, lakini katika karne ya 20 harakati dhidi ya uvutaji wa sigara zilipamba moto kwa sababu za kiafya.

Licha ya kuwepo kwa sheria hiyo nchini, utekelezaji wake kwa vitendo umeshindikana kwa kuwa ni jambo la kawaida katika mikusanyiko ya watu kukuta mvutaji wa sigara au mtumiaji wa tumbaku aina ya ugolo akifanya hivyo hadharani bila kuhojiwa na yeyote. Hata hivyo, wakati sheria hiyo ikishindikina kusimamiwa katika Tanzania, nchini China sheria hiyo imesimama kama ilivyo.

FikraPevu inaweza kuthibitisha kwamba China inaongoza ulimwenguni kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaovuta sigara. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, idadi ya wavuta sigara katika nchi hiyo inafikia milioni 300. Kwa hiyo, kutokana na madhara makubwa ya sigara yanayotokana na idadi hiyo ya wavutaji, Serikali ya nchi hiyo imeamua kutekeleza kwa vitendo sheria ya kuzuia uvutaji wa sigara kuanzia Juni Mosi, mwaka huu wa 2015.

Katika sheria hiyo mpya ya China, mtu yeyote atakayekamatwa akivuta sigara katika mikusanyiko ya watu atalazimika kulipa faini ya dola za Marekani 30, sawa na karibu Sh 60,000. Nionavyo mimi, kama Serikali ya nchi ya China imeweza kuamua kusimamia sheria hiyo kwa vitendo pamoja na kuwa na idadi kubwa hiyo ya wavutaji na watumiaji wa tumbaku, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara ya kiafya yanayotokana na bidhaa hiyo kwa wananchi wake, Tanzania tumeshindwa nini kusimamia sheria hiyo?

Takwimu kutoka nchini China zinaonyesha kwamba kila mwaka, watu zaidi ya milioni moja wanafariki dunia kutokana na magonjwa yanayotokana na uvutaji wa sigara na matumizi mengine ya tumbaku.

Aidha, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2003, zinaonyesha kuwa kila baada ya sekunde 10, mtu mmoja hufariki dunia kutokana na maradhi yatokanayo na matumizi ya tumbaku.

Kwa mujibu wa takwimu hizo za WHO, inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2025, vifo vitakavyotokana na matumizi ya tumbaku vitaongezeka kwa kiwango cha asilimia 70 kuliko ilivyokuwa mwaka 2003. Lakini pia, takwimu hizo zinaonyesha kuwa kufikia mwaka 2030, idadi ya watu milioni 10 watakuwa wakifariki dunia kila mwaka kutokana na uvutaji wa sigara ulimwenguni, huku ikitajwa kuwa asilimia 70 ya vifo hivyo vikitokwa katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwemo.

Inaonyesha pia kwamba asilimia 36 ya wavuta sigara barani Afrika ni wanaume, huku asilimia tisa tu wakiwa ni wanawake, wakati kwa upande wa Tanzania asilimia ya wanaume wanaovuta sigara ni asilimia 46, wakati wanawake inatajwa kuwa ni asilimia nne tu.

Kuna aina mbalimbali za matumizi ya tumbaku, kama vile kubwia, kunusa, kuvuta na kutafuna, ambapo wananchi wengi katika maeneo ya mijini na vijijini, wamekuwa wakitumia tumbaku kwa wingi bila kujua madhara ya kiafya ambayo yanaweza kuwapata.

Kwa mujibu wa tafiti zilizopo, matumizi makubwa ya tumbaku yamekithiri zaidi katika nchi zinazoendelea kuliko nchi zilizoendelea kutokana na juhudi za kampuni kubwa zinazozalisha bidhaa hizo kupanua wigo wao wa kibiashara kwa kuweka matangazo mbalimbali yanayotoa tahadhari juu ya madhara yasababishwayo na tumbaku. Wataalamu wa afya wanayataja magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababishwa na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kuwa ni pamoja na saratani ya ngozi, saratani ya mapafu, saratani ya kizazi, saratani ya koo, saratani ya kinywa na saratani ya kibofu.

Magonjwa na madhara meninge ni magonjwa ya moyo, kuathirika kwa mimba, mtoto anayezaliwa kuwa mlemavu wa akiri, watoto kuzaliwa na afya hafifu hivyo kuathiri ukuaji wao, kupungua kwa nguvu za kiume, vidonda vya tumbo, mtoto wa jicho, kunyonyoka nywele na kuziba kwa mishipa ya damu.

Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa za kuelimisha jamii madhara ya tumbaku ili wananchi wasihamasike kutumia bidhaa za tumbaku. Hata hivyo, pamoja na kutengwa siku maalum ya kutotumia tumbaku duniani ambayo huadhimishwa kila Mei 31 kila mwaka, bado inaonekana tatizo la matumizi ya tumbaku linaongezeka kwa kasi kubwa katika jamii.

Ni muhimu basi wakati jamii ikiishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa busara wa kutunga sheria hiyo ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya, kikiwemo Chama cha Afya ya Jamii Tanzania(TPHA), wahusika wakuu wa usimamizi wa sheria hiyo wakatimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wote wanaovuta sigara kwenye mikusanyiko ya watu na maeneo ya umma, wanachukuliwa hatua za kisheria.

Wakati China ikitajwa kuwa nchi ya mfano katika kusimamia sheria hiyo, Juni 22, 2009, Rais Barack Obama wa Marekani alisaini muswada wa sheria ya usimamizi wa tumbaku, ambao uliipatia Idara ya Usimamizi wa Chakula na Dawa katika nchi hiyo, mamlaka makubwa ya kusimamia matumizi ya tumbaku.

Kwa mujibu wa muswada huo, unaujulikana kama Sheria ya Kuzuia Uvutaji wa Sigara Majumbani na Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku, Idara ina mamlaka ya kupunguza kiwango cha nikotini kwenye bidhaa za tumbaku, kupiga marufuku uuzwaji wa sigara zenye ladha ya pipi kwa vijana, pamoja na kupiga marufuku alama za kibabaishaji kama vile kiwango cha chini cha kemikali na kuchapisha onyo la madhara ya uvutaji kwa afya.

Aidha, Oktoba 28, 2009, Serikali ya Uswisi pia iliidhinisha ratiba ya kuanza utekelezaji wa sheria ya kuzuia uvutaji sigara hadharani, ambapo ilipangwa kuanza kutumika Mei Mosi, 2010. Sheria hiyo ya Uswisi inapiga marufuku uvutaji sigara hadharani au kwenye sehemu yoyote ya kazi yenye watu zaidi ya wawili.

Desemba 8, 2009, Serikali ya Korea Kusini, kupitia Wizara ya Afya na Huduma za Jamii, ilitangaza mpango wa kupiga marufuku uvutaji sigara kwenye maeneo ya wazi, sharia iliyotakiwa kuanza kutumika mwaka 2011.

Novemba 15, Serikali ya Poland nayo ilisaini sheria hiyo. Kwa mujibu wa sheria hiyo ya nchi hiyo, watu wanaovunja sheria hiyo watalipa faini ya dola 175 za Marekani, sawa na karibu Sh 350,000. Aidha, sheria hiyo inawataka wamiliki wa maeneo ya wazi, kuweka alama zinazopiga marufuku uvutaji sigara katika maeneo yao hayo, vinginevyo wakibainika kutofanya hivyo, wanalipa faini ya hadi dola 700 za Marekani, sawa na karibu Sh milioni 1.4.

Nchi nyingine ulimwenguni ambayo imesaini sharia hiyo na kuisimamia ni Sweden. Sheria hiyo ya tangu mwaka 1993, inapiga marufuku uvutaji sigara katika sehemu zenye shughuli za watoto, huduma za matibabu na sehemu za mawasiliano ya umma.

Aidha, sheria hiyo inawataka waajiri wote nchini humo kuhakikisha wanaweka mazingira yasiyo ruhusu uvutaji sigara katika maeneo yote ya kazi, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku wauzaji wa sigara kuuza bidhaa hiyo kwa vijana wenye umri chini ya miaka 18.

Je, kama nchi zote hizo zimeweza kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa sheria za matumizi ya bidhaa za tumbaku kutokana na madhara yake kiafya, Serikali ya Tanzania na Watanzania, tumeshindwa kwanini wakati sheria tunayo?


HADHARI: Maziwa Bora ya Kopo ya Watoto yaadimika, Maziwa Feki yauzwa Madukani

$
0
0

KUADIMIKA kwa maziwa bora ya kunyonyeshea watoto wadogo, kumewafanya baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu na wenye tamaa ya kipato kuingiza sokoni maziwa feki yaliyokwishapigwa marufu nchini na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), FikraPevu imebaini.

Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wetu katika jiji la Dar es Salaam, umebaini kwamba maziwa bora kwa watoto yaliyopendekezwa na TFDA kuingizwa sokoni, yamekuwa adimu kwa siku kadhaa sasa, hali iliyotoa mwanya kwa wafanyabiashara hao kuanza kuuza maziwa hayo feki kwa baadhi ya familia zinazohitaji ambazo hazina uelewa wa kutofautisha aina ya maziwa bora na feki.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, FikraPevu imebaini kwamba maziwa feki yaliyopigwa marufuku na TFDA kutokana na kukosa ubora hali inayoweza kuhatarisha afya za watoto wadogo, ndiyo kwa sasa yamefurika katika maduka mengi ya jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuziba pengo la soko la maziwa baada ya bidhaa bora hiyo kuadimika.

Maziwa hayo feki ambayo kwa sasa yameingizwa sokoni ingawa yamepigwa marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, sura ya 219, ni pamoja na S-26, SMA, Isomil, Cow & Gate Infant Formula, Infantcare, Nutrient optium na Ifasoy. Katika baadhi ya maduka, maziwa hayo yamekuwa yakiuzwa kwa bei mbaya ya hadi Sh 20,000 kutokana na kuadimika kwa maziwa bora.

Maziwa bora na yaliyoidhinishwa na TFDA kuingizwa sokoni, ambayo baadhi ya wafanyabiashara wamekiri kuadimika, lakini bila kuelewa chanzo hasa cha kuandimika kwa maziwa hayo, nchi zinazotengeneza bidhaa hiyo zikiwa kwenye mabano, ni pamoja na Lactogen 2 Follow-up formula (Ufaransa), NAN-2 Infant Formula (Ufaransa), Cow Bell Infant Formula (Ufaransa) na NAN-1 Infant Formula (Uholanzi).

Mengine ni Lactogen-1 Infant Formula (Afrika Kusini), Lactogen-2 Follow up Formula (Afrika Kuzini), NAN-1 Infant Formula (Afrika Kusini), NAN-2 Infant Formula (Afrika Kusini) na Lactogen-1 Infant Formula (Ufaransa).

Kwa mujibu wa TFDA, maziwa yote ya watoto yanayouzwa nchini yanapaswa kuwa na maelezo juu ya ubora wake, mchanganyiko wa viini lishe na njia sahihi ya matumizi kwa lugha zote mbili za Kiswahili na Kiingereza, lakini maziwa mengi feki yanayounzwa kwa sasa katika maduka mengi, yakiwemo baadhi ya maduka makubwa, maarufu kwa jina la Super Market, yana maelezo ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine ambazo wananchi wengi hawana uelewa nazo.

Baadhi ya wananchi wakazi wa Dar es Salaam, wameanza kulalamikia hali hiyo ya kuzagaa kwa maziwa hayo feki madukani, hali iliyozua hofu kubwa kwenye familia nyingi zenye watoto wadogo wanaohitaji kunyonyeshwa kwa maziwa ya kopo kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kiafya kwa mama zao.

Kutokana na hali ya dunia ya sasa iliyokumbwa na ugonjwa wa Ukimwi, kina mama wengi wanaojifungua watoto wao wakiwa tayari wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo, hushauriwa kutowanyonyesha watoto wao kwa maziwa ya mama, badala yake hushauriwa kutumia maziwa hayo ya kopo pamoja na maziwa ya ng’ombe.

Imeelezwa na baadhi ya wafanyabiashara wanaojishughulisha uuzaji wa bidhaa hizo za maziwa ya watoto ya kopo kuadimika sokoni kwa maziwa bora hayo yaliyoidhinishwa TFDA, kunaweza kuchukua hata zaidi ya miezi minne kuanzia sasa.


Baadhi ya wafanyabiashara hao wamewatahadhirisha kina mama wanyonyeshao watoto wao kwa maziwa hayo ya kopo, kuepuka kununua maziwa ya kwenye kopo yenye rangi ya njano, maziwa hayo yakidaiwa kuwa na mchanganyiko wa maziwa bora na feki, hivyo kuwashauri kununua maziwa yanayohifadhiwa kwenye makopo yenye rangi ya blue, ambayo yanaelezwa kutokuwa na shaka yoyote ya ubora.

Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina la Patrick Aron, ameiambia FikraPevu kuwa maduka yote yaliyokuwa yakiuza maziwa bora kwa bei ya jumla, hasa yaliyoko katika maeneo ya Kitumbini, katikati ya jiji la Dar es Salaam, kwa sasa hayauzi maziwa hayo kutokana na kuadimika huko, huku akisema maduka machache ambayo yana akiba ya maziwa bora hayo, huyauza kwa bei mbaya ya mwendo wa kuruka. 

Patrick amezishauri familia zenye kuhitaji maziwa ya kopo kwa sasa kuwa makini na maziwa yanayouzwa madukani, ikiwa ni pamoja na kuyachunguza vyema kwa manufaa ya watoto wao, kabla ya kununua.

Kwa upande wake, mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Ndosi, ameomba TFDA kufanya ukaguzi juu taarifa hizo za kuzagaa madukani kwa maziwa feki hayo ya kopo ili kuwaondolea hofu wananchi.

FikraPevu imetembelea maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam na kubaini kuwepo kwa maziwa hayo feki madukani. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na Mwenge, Kinondoni, Kurasini, Manzese, Ubungo na Sinza.

Kampuni ya Nestle Equatorial African Region Tanzania, imetajwa kuwa moja ya kampuni nchini yenye kibali cha kuingiza na kusambaza maziwa ya watoto wachanga aina ya NAN-1 na NAN-2, Lactogene (Nestle), S-26, Promil Gold (Wyeth), Infacare (Aspen) na kadhalika.

Wataalamu afya na lishe nchini wanayataja maziwa ya kopo ya watoto kama kundi la vyakula vyenye hatari (risk food), hali inayowalazimu maofisa wa TFDA kufanya operesheni za mara kwa mara kuhusu bidhaa hiyo kwa lengo la kukabiliana na hatari hiyo.

Ofisa Habari wa TFDA, Gaudencia Simwanza, amekiri taasisi yake hiyo kuwa na taarifa za kuadimika kwa maziwa ya watoto pamoja na kusambazwa sokoni kwa maziwa hayo feki kinyume cha sheria.

“Tunazo taarifa za kuzagaa kwa maziwa feki madukani kwa kisingizio cha kuadimika kwa maziwa halisi, ndiyo maana wauzaji wanauza kwa uficho. Tunaendelea na operesheni ya kushitukiza katika maeneo mbalimbali na wote watakaobainika watachukuliwa sheria stahiki.

Utafiti: Kuanza Mapema Matibabu ya Virusi vya UKIMWI hata kama Hujaathirika kunaboresha Afya kwa muathirika

$
0
0

TAKWIMU za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa nchi zilizopo Kusini Mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo, zinaongoza kuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa kiwango kikubwa, ambapo watu milioni 24.7 walikuwa wanaishi na VVU hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2013.

Kwa mujibu wa takwimu hizo za WHO, ukanda huo unabeba asilimia 70 ya maambukizi mapya ya VVU duniani na kwamba duniani kote kumekuwa na tafiti nyingi kuhusu janga hilo ili kupata suluhisho la moja kwa moja kupitia tiba mbalimbali.

Jaribio kubwa la kitafiti la kimataifa lililopewa jina la Strategic Timing of AntiRetroviral Treatment (START) limegundua kuwa watu walioambukizwa VVU wana hatari ndogo ya kupata UKIMWI au maradhi sugu nyemelezi kama Kifua Kikuu ikiwa wataanza kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU mapema wakati idadi ya CD4 ikiwa bado kubwa badala ya kusubiri idadi ya CD4 kushuka chini.

Tafiti za WHO zinaonyesha kuwa watu wanaoanza matibabu ya kupunguza makali ya VVU mapema, kunapunguza hatari ya kuambukiza VVU kwa mke, mume, au mpenzi asiye na maambukizi ambapo matokeo ya tafiti hizo yanaunga mkono kutoa matibabu kwa kila mtu aliyegundulika kuwa na VVU.

Aidha, matokeo haya mapya yametokana na utafiti mkubwa uitwao START ambao ulidai kuwa watu wote walio na maambukizi ya VVU wakianza matibabu ya kupunguza makali ya VVU watanufaika.

Taasisi ya Taifa ya Mzio na Magonjwa ya Kuambukiza inayojulikana kama The National Institute of Allergy and Infectious Diseases (NIAID) ya nchini Marekani kama moja ya taasisi za afya nchini humo ilifadhili utafiti huo, ingawa utafiti huo ulitarajiwa kukamilika 2016, bodi inayohusika na takwimu nchini humo ijulikanayo kama Data and Safety Monitoring Board (DSMB) ilipendekeza matokeo kutolewa mapema zaidi.

Mkurugenzi wa NIAID, Daktari. Anthony S. Fanci, amesema wanao uthibitisho kwamba utafiti huo ni kitu chenye manufaa makubwa kwa mtu yeyote aliyeambukizwa VVU kuanza matibabu ya kupunguza makali ya VVU mapema kuliko kuanza baadae.

"Kuanza matibabu mapema hutoa faida mara mbili zaidi, sio tu kuboresha afya za walioambukizwa lakini pia kupunguza wingi wa virusi (viral load) kitu kitakachosaidia kupunguza hatari ya kuambukizwa VVU kwa wengine. Matokeo haya ya utafiti yanaweza kubadili miongozo ya matibabu ya VVU dunia nzima", aliongezea Dk.Fanci.

Kwa upande wake Daktari, Jens Lundgren, kutoka Chuo Kikuu cha Copenhagen,mmoja wa wenyeviti wa utafiti huo alisema hatua hiyo ni muhimu katika utafiti wa VVU, “Sasa tunao ushahidi mkubwa kwamba kuanza matibabu mapema ni faida kwa mtu mwenye VVU. Matokeo haya ya utafiti yanahamasisha kutibu mtu yeyote mwenye VVU bila kujali idadi ya CD4 zake na kuanza matibabu mapema kunaleta faida kwa watu wote bila kujali unatoka katika nchi yenye kipato cha chini, cha kati au cha juu”.

Utafiti wa START uliozinduliwa rasmi Machi, 2011 na kuendeshwa na taasisi ya The International Network for Strategic Initiatives in Global HIV Trials (INSIGHT) katika vituo 215 kwenye nchi 35. Ulibaini kwamba jumla ya watu wenye VVU 4, 685, wanaume kwa wanawake kuanzia miaka 18 na zaidi, wengi wao wakiwa na miaka 36 walitumika katika jaribio. Washiriki hawakuwa kwenye matibabu ya kupunguza makali ya VVU na walikuwa na CD4 zaidi ya 500.

Kwa mujibu wa utafiti huo, walikadiria nusu ya washiriki na kuwaanzishia matibabu ya kupunguza makali ya VVU mapema na nusu waliobaki waliachwa hadi idadi ya CD4 zao zilipoteremka hadi 350 ambapo kwa wastani washiriki wa utafiti walifuatiliwa kwa miaka mitatu. Utafiti ulipima jumla ya matokeo yaliyohusisha hali mbaya zinazotokana na UKIMWI kama Kifua Kikuu na Saratani zinazohusiana na UKIMWI kama Saratani ya Seviksi (Shingo ya Kizazi) pamoja na hali mbaya zisizohusiana na UKIMWI ikiwemo magonjwa ya moyo, Ini, figo na kifo.

Kulingana na takwimu za Machi, 2015; DSMB walipata sampuli 41 zisizo na hali mbaya, zisizohusiana na UKIMWI kwa wale walioanza matibabu mapema na hali mbaya 86 kwa wale ambao hawakuanza matibabu mapema. Uchambuzi uliofanywa na DSMB wamegundua hatari ya kupata maradhi nyemelezi mabaya au kifo ambayo ilipunguzwa kwa asilimia 53 kwa wale walioanza matibabu mapema ikilinganishwa na wale waliochelewa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa utafiti wa START ni utafiti mkubwa na wa kwanza kutoa ushahidi wa kisayansi wa kuunga mkono muongozo wa matibabu ya VVU nchini Marekani unaopendekeza watu wote wenye VVU hata wasio na dalili za VVU kuanza matibabu mapema bila kujali idadi ya CD4 zao. Muongozo wa sasa wa matibabu ya VVU wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unapendekeza kuwa watu wenye VVU waanze matibabu ya kupunguza makali ya VVU ikiwa CD4 zao zitashuka hadi 500 au chini ya hapo.

Nchini Tanzania, utafiti wa kiashirio cha VVU/UKIMWI na Malaria 2011-2012 uliojumuisha kwa kupima zaidi ya wanawake na wanaume 20,811 kwa mujibu wa utafiti huo asilimia 5.1 ya watanzania wenye umri wa miaka (15-49) wana maambukizi ya VVU/UKIMWI. Maambukizi ya VVU/UKIMWI ni ya kiwango cha juu miongoni mwa wanawake kuliko wanaume katika maeneo ya mjini na vijijin na wakazi wa mijini ni mara mbili zaidi ya wakazi wa vijijini.

Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa mkoa wa Njombe unaongoza kwa maambukizi ya VVU kwa asilimia 14.8 ambapo Iringa ina asilimia 9.1 ya watu walioathirika na VVU na Mbeya ikiwa na asilimia 9.0, kwa upande wa mikoa yenye kiwango cha chini cha maambukizi ya VVU ni Manyara na Kilimanjaro ambazo zina asilimia 2 ya maambukizi ya VVU na Pemba ikiwa ni chini ya asilimia 1 ya maambukizi ya VVU.

Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2013 zinasema tayari watu milioni 1.4 wanaishi na VVU nchini Tanzania. Wakati takwimu za Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) zikiripoti kuwa kuwapatia watu waishio na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) 70, 000 tiba ya kuongeza kinga ya mwili hadi kufikia 2006. Baadhi ya vitu vinavyosababisha kuenea kwa VVU nchini ni pamoja na kufanya mapenzi bila ikiwa ni pamoja na kutotumia kondomu, matumizi ya pombe, dawa za kulevya na kuwepo kwa maradhi ya ngono ikiwemo Kisonono na Kaswende.

Wanaotoa Mimba chini ya Miaka 18, hatarini kupata Ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi

$
0
0

WASICHANA wanaopata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18 pamoja na wenye tabia ya kutoa mimba mara kwa mara, wametajwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi, FikraPevu imefahamishwa.

Mbali na kundi hilo, pia watumiaji wa dawa za kulevya, watu wenye magonjwa ya zinaa, wanawake wanaozaa mara kwa mara na wanaume wasio tahiriwa nao wapo katika hatari ya kupata aina hiyo ya saratani.

Mshauri wa masuala ya Afya ya Uzazi, Leojin Mnzava, ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibaha, amebainisha hayo katika mafunzo ya kuwapatia elimu hiyo ya Afya ya Uzazi wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari wilayani humo na kuwa tayari wameanza kutoa elimu ya ugonjwa wa Saratani ya shingo ya kizazi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanafunzi walio na tabia ya kufanya mapenzi kabla ya wakati.

Amesema kwamba saratani ya shingo ya kizazi, ni hatari kuliko magonjwa mengine kama vile Ukimwi na Malaria, hivyo wanawake wanapaswa kuwa makini na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha au kuchochea magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa huo.

Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Asasi ya Maendeleo ya Wanawake ya INUKA, Gaudience Msuya, yenye makao yake makuu Jijini Dar es Salaam, amesema wametoa mafunzo kwa walimu 40 waliopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, ambayo yamelenga kuwakumbusha walimu visababishi vya saratani ya shingo ya kizazi ili waielimishe jamii wakiwemo wanafunzi.

Lindi yatajwa kuongoza Saratani za Matiti na Shingo ya kizazi

Wakati huo huo, Mkoa wa Lindi umetajwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake waliogundulika kuwa na saratani ya matiti na shingo ya kizazi kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutambua dalili za ugonjwa huo, ambao kama ukitambuliwa mapema unatibika.

Daktari Faridi Ally kutoka Hospitali ya Sokoine iliyoko Mkoani Lindi, amebainisha hayo wakati wa mahojiano na FikraPevu na kwamba wataalamu kutoka katika hospitali hiyo wamekwishaanza kutoa elimu kwa wanawake zaidi ya 300, juu ya kutambua dalili za ugonjwa wa saratani na kusisitiza umuhimu wa kuwa na kitengo maalumu cha kutibu maradhi hayo.

Mkuu wa mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza, amesema mipango ya Serikali ya mkoa ni pamoja na kuwa na kitengo maalumu cha kutibu maradhi hayo na kwamba kwa kuanza wameanza kutoa elimu ili kupunguza tatizo kabla ya mipango hiyo haijakamilika.

Saratani ya kizazi ni nini?

Ni aina ya saratani inayoshambulia seli/chembechembe zilizoko kwenye ngozi laini inayozunguka shingo ya kizazi. Chanzo cha ugonjwa huo ni kirusi kiitwacho 'Human Pailloma Virus' na huambukizwa kwa njia ya kujamiana na mtu mwenye maambukizi hayo.

Aidha, dalili za ugonjwa ugonjwa huo ni pamoja na kutokwa na majimaji au uchafu usio wa kawaida ukeni, kutokwa na damu ukeni wakati ambao mwanamke hayuko kwenye hedhi pamoja na maumivu makali wakati wa kujamiana.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa na taasisi za Afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) zimebainisha kwamba tabia hatarishi inayopelekea kupata magonjwa haya ni pamoja na kuanza ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 18), uvutaji wa sigara, kuzaa mara kwa mara, matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula, kuwa na wapenzi wengi au kujamiana na mtu mwenye wapenzi wengi.

Ajali ikiua 20 Serikali inaguswa, Wanawake 720 Wanaofariki Dunia kwa Uzazi wala haiguswi

$
0
0

Jumla ya wanawake 720 wanakufa kila mwezi nchini Tanzania kutokana na matatizo ya uzazi, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa kuwa na vifo vingi vitokanavyo na matatizo ya uzazi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa kila siku wanawake 24 wanafariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi ambapo kwa mwaka mmoja zaidi ya wanawake 8,600 wanakufa jambo ambalo linakwamisha malengo ya millennia.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika wizara hiyo, Dk Georgina Msemo, amezitaja sababu zinazochangia vifo hivyo kuwa ni pamoja na kina mama wajawazito kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, kuchelewa kuanza kliniki pamoja na kujifungilia katika vituo vya afya ambavyo havina huduma za kutosha za uzazi.

Kwa mujibu wa Dk Msemo, nchi ya Sirilanka ni miongoni mwa nchi duniani ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi. Inaelezwa kwamba nchi hiyo imefanikiwa kutokana na Rais wa nchi hiyo kuhusika kwa asilimia 100 katika kampeni ya kutokomeza vifo hivyo.

Takwimu za vifo vya wajawazito na watoto nchini Tanzania vinatishia ustawi wa Taifa kutokana na  kuwepo takwimu za kutisha zinazoonyesha kuwa kwa mwaka mmoja pekee, wanawake zaidi ya 8,600 wanafariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi, huku takriban watoto 50,000 wakifariki dunia kila mwaka.

Mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 ujulikanao kama ‘One Plan’ ulipanga kuweka vifaa vya kufanyia upasuaji wa dharura kwenye vituo vingi vya afya nchini, jambo ambalo limeshindikana hadi sasa.

Hata hivyo, taarifa ya hivi karibuni ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekuja na habari njema inayoelezea kushuka kwa idadi ya vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi (MMR), kutoka 578 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2005 hadi vifo 454 mwaka 2010, hivyo kufikia lengo la nne la millennia.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi kama hicho, vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 68 katika kila vizazi 1,000 hadi kufikia 54. Mwaka 2010, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 260 duniani zilizotoa ahadi kadhaa mbele ya jumuiya ya Umoja wa Mataifa (UN), za kuboresha huduma ya afya kupitia mpango wa kuboresha afya ya mama na mtoto ujulikanao kama “Kila mwanamke, kila motto.”

Katika ahadi yake hiyo, Tanzania ilipanga kuongeza bajeti ya sekta ya afya kutoka asilimia 12 hadi 15, kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya afya kutoka 5,000 hadi 10,000 na kuongeza idadi ya wahitimu kwenye vyuo hivyo kutoka 3,000 mwaka huo hadi 7,000 ifikapo 2015. Lakini pia Tanzania iliahidi kuboresha upatikanaji bure wa huduma za uzazi, kuongeza huduma ya uzazi wa mpango kutoka asilimia 28 mwaka huo hadi 60 mwaka 2015, kuboresha mifumo ya mawasiliano ya simu kwenye hospitali pamoja na kuanzisha matumizi ya magari ya wagonjwa yenye gharama nafuu.

Tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 2010, nchi nyingi duniani, hasa za Kiafrika zilijitokeza na kuahidi kufanya mambo kadhaayatakayosaidia kuboresha afya ya jamii katika nchi zao. Hata hivyo, kutokana na kuendelea kuwepo kwa idadi kubwa ya vifo
vinavyotokana na uzazi nchini Tanzania, ni wazi kwamba hadi sasa Serikali imeshindwa kutimiza ahadi zake hizo za tangu mwaka 2008, za kwamba kufikia mwaka huu wa 2015, vituo vya afya vitakuwa vinatoa huduma za afya za dharura kwa asilimia 50.

Utafiti uliofanywa na FikraPevu unaonyesha kuwa ni asilimia tisa tu ya vituo vya afya  nchini vinavyotoa huduma za afya za dharura, ikiwemo upasuaji. Aidha, utafiti huo umebaini kutokuwepo kwa mipango thabiti ya pamoja ya utekelezaji wa Sera ya Afya miongoni mwa wadau wakuu wa sekta hiyo kwa kuzingatia takwimu zilizopo ndani ya Serikali yenyewe.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya uzazi, ikielezwa kwamba hadi sasa bado tatizo la vifo vya uzazi halijapewa kipaumbele kama ambavyo mambo mengine yanapewa uzito na Serikali.

Ukubwa wa tatizo la uzazi unatazamwa kama tukio la kawaida wakati ni janga la kitaifa kwa sababu linamaliza maisha ya wanawake ambao ndiyo kiwanda cha uzalishaji wa kizazi cha Taifa la kesho. Kwa mfano, inapotokea ajali tu ya basi na kuuwa watu tuseme 20, Serikali inashituka na kuchukua hatua, lakini inapotokea wanawake 20 wakapoteza maisha kila siku kutokana na matatizo ya uzazi, Serikali hiyo hiyo inaonekana kutoshituka na kuchukua hatua madhubuti. Hapo ndipo tatizo kuu lilipo katika janga hili la Taifa.

Fahamu ukubwa wa Tatizo la Ugonjwa wa Akili na aina ya Ugonjwa huo

$
0
0

WATAALAMU mbalimbali wa magonjwa ya akili, wanauelezea ugonjwa huo kama moja matatizo makubwa yanayoikumba jamii ya Watanzania na dunia kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Wataalamu hao, ugonjwa huo huathiri uwezo wa mtu wa kufikiri, kudhibiti hisia na tabia yake, ikilinganishwa na mtu ambaye hajaathirika kwa ugonjwa huo, hali inayomfanya ashindwe kufurahia uhusiano mzuri na binadamu wenzake, ikiwa ni pamoja na kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha.

Tafiti mbalimbali za magonjwa ya akili, zinabainisha kwamba ugonjwa huo hutofautiana kutegemeana na muda na kadiri ambavyo mtu ameathirika na aina ya ugonjwa wenyewe huo.

Kwa mujibu wa tafiti hizo, ugonjwa huo wa akili unaweza kuwapata watoto na watu wazima wa jinsia zote, matajiri na masikini, na bila kujali kiwango chochote cha elimu. Hata hivyo, mtu mwenye ugonjwa wa akili akipata tiba sahihi anaweza akapona kabisa na kuendelea na maisha yake ya kawaida.

Kwa kutambua umuhimu wa utafiti wa magonjwa mbalimbali nchini, Serikali iliamua kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kwa Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1979, kabla ya kufanyiwa marekebisho mwaka 2002 ili kushughulikia utafiti wa magonjwa mbalimbali ikiwemo yale yasiyo ya kuambukiza ukiwemo ugonjwa huu.

Takwimu kutokana na taarifa ya hivi karibuni kabisa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kwamba watu milioni 26 duniani wanaishi na ugonjwa wa akili, ambao kitaalamu hujulikana kama ’Skizofrenia,’ huku takwimu hizo zikibainisha kuwa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 60 kufikia mwaka 2050.

Hata hivyo, wakati takwimu za WHO zikionyesha ukubwa huo wa tatizo hilo duniani, kwa upande wa Tanzania tafiti zilizopo zinaonyesha kwamba takriban watu 450,000, kati ya idadi yote ya wananchi wa Taifa hili wanaofikia milioni 50, wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ya magonjwa ya akili.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar, tafiti hizo zinabainisha kwamba asilimia 6.8, sawa na takriban watu 70, ya wananchi wote Visiwani hivyo wapatao milioni 1.3 wanakabiliwa na tatizo hilo la magonjwa ya akili kwa mujibu wa utafiti wa wataalamu hao wa mwaka 2012.

Daktari Bingwa na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Frank Masawe, ameiambia FikraPevu kuwa mtu aliyeathiriwa na ugonjwa wa akili, hukosa uwezo wa kufanya kazi ya kumwingizia kipato, kutelekeza familia yake na wakati mwingine kujikuta akiwa mzururaji mitaani.

Shule ya Msingi Tandika, iliyoko katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, ni moja ya shule nchini zinazopokea na kuwafundisha masomo ya darasani watoto wenye matatizo ya magonjwa hayo ya akili.

Baadhi ya walimu wa shule hiyo, wanaohusika na Kitengo Maalumu cha Kuhudumia Watoto hao wenye matatizo ya akili, wameiambia FikraPevu kwamba mara kadhaa wamekuwa wapata shida sana kuwafundisha watoto hao, hasa katika suala zima la mawasiliano ya wanafunzi hao na walimu wao.

Ofisa Muuguzi wa Kituo cha Afya cha Chamazi katika Manispaa hiyo ya Temeke, ambacho ni Tawi la Afya la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Frednand Shangala, anasema ugonjwa huo huweza kutibiwa kwa muda usiotabirika kulingana na ukubwa wa tatizo.

Kwa mujibu wa Dk. Shangala mtu aliyekwishaathirika kwa ugonjwa wa akili, inaweza kumchukua kati ya mwaka mmoja hadi mitatu kuweza kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida ya ubinadamu, hasa kama mgonjwa mwenye na jamii inayomhudumia watazingatia masharti ya Daktari na tiba pia.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili, ambaye pia ni Mtaalamu wa Tiba ya Waathirika wa Dawa za Kulevya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, bila kutaka jina lake litajwe, ameiambia FikraPevu kuwa magonjwa ya akili kwa ujumla wake yameathiri vijana wengi nchini kutokana na kutohudhuria mapema katika Vituo vya Kliniki na Vituo vya Afya kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa mujibu wa Daktari huyo, tatizo hilo linaweza kumtokea mtu yeyote wakati wowote, hasa kwa wale wanaotumia dawa za kulevya, hususan vijana.

Takwimu zaidi zinaonyesha kwamba katika kila watu wazima 50, watu watatu hadi wanne, husumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya akili. Kwa mujibu wa taarifa za WHO, wengi wa watu hao wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali hayo ya akili, wanakuwa ni wale ambao hawapati matibabu mapema kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya mtazamo hasi wa jamii nyingi kuhusiana na magonjwa hayo.

Hata hivyo, ripoti ya hivi karibuni Shirika la Kitaifa la Magonjwa ya Akili la Marekani, inasema kwamba ingawa magonjwa ya akili yana tiba, takriban asilimia 60 ya watu wazima katika Taifa hilo kubwa duniani kiuchumi, pamoja na takriban asilimia 50 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka minane na 15 wameathirika kwa magonjwa hayo ya akili.

Viewing all 296 articles
Browse latest View live


<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>