MAJI huunda zaidi ya 2/3 ya miili yetu, lakini wengi wetu huacha kunywa maji na kunywa vinywaji vingine tukisahau kunywa maji ya kutosha. Takwimu zinaonyesha kuwa mwili wa mwanadamu umejengwa kwa asilimia kati ya 55 na 75 za maji ambapo watu wembamba wana kiasi kikubwa cha maji mwilini kuliko wanene.
Asilimia 60 ya uzito wako ni maji na mifumo ya mwili wako hutegemea maji ili kufanya kazi zake kwa ufanisi, unapoanza kuhisi kiu mwili unakuwa umepungukiwa na maji. Hata katika upungufu mdogo wa maji mwilini, wakati ambapo asilimia 1 hadi 2 ya uzito wa mwili inapungua, suala hilo humfanya mtu akose nguvu na ajisikie amechoka.
Mwili unahitaji kwa kiasi kikubwa ili kufanya kazi zake vyema, mfano mapafu yako yanahitaji vikombe viwili vya maji hadi vinne kila siku ili kufanikisha kazi yake ya upumuaji kwa ufanisi. Na kiasi hicho huhitajika zaidi wakati wa baridi. Kunywa glasi 8 za maji zenye ujazo wa mililita 237 au robo lita kila siku ndio kiwango ambacho kipo akilini mwa wengi, wote wakiwa na imani kwamba ndicho kiwango kinachokubalika kiafya.
Ukweli ni kwamba : "Kiwango cha maji ambacho unachopaswa kunywa kinategemeana na mtu na mtu. Mahitaji ya maji yanatofautiana, mambo kama jinsia, hali ya hewa, kiwango cha joto la mwili, ushiriki wa mazoezi, aina ya kazi, umri na aina ya mlo unaokula ni mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa, " anasema Dk. Robert A. Huggins wa Chuo Kikuu cha Connecticut.
Msomaji wa FikraPevu faida za maji mwilini ni pamoja na kusaidia umeng'enyaji wa chakula, huboresha hali ya viungo na misuli, maji yanaweka ubongo katika hali nzuri zaidi ya ufanisi zaidi hivyo kunywa maji ya kutosha kunamuwezesha mtu kufikiria vyema zaidi, husaidia kupunguza uwezekano wa kupata baadhi ya magonjwa mfano mafua na kusaidia kupona haraka ugonjwa huo, mawe ya figo, matatizo ya ini, baadhi ya saratani n.k.
Tikiti maji ni chanzo kizuri cha vitamini. Katika tunda hilo kuna Vitamin A, inayosaidia kuboresha afya ya macho na pia kuondosha sumu mwilini, Vitamin C
Ikiwa unataka kupunguza unene na uzito, maji yanaweza kukusaidia kwa kuwa maji huongeza kasi ya shughuli za kimetaboliki na kufanya mwili kutumia nishati nyingi zaidi hivyo kupunguza kiasi cha nishati kitakachohifadhiwa mwilini katika hali ya mafuta hivyo kupunguza unene na uzito kiujumla.
Nini dalili za kupungukiwa maji mwilini?
Unapopungukiwa maji mwilini, mwili huwa katika kiwango cha chini kuliko kinachotakiwa kwa mwili kufanya kazi vizuri. Ishara/dalili kuu 4 zinazoonyesha mwili wako umepungukiwa maji ni :-
Uchovu
Kuna vitu vingi vinavyosababisha uchovu, lakini ukihisi uchovu wakati wa mchana inaweza kuwa kwasababu unakunywa vinywaji vyenye kafeini kama kahawa bila kunywa maji ya kutosha. Kitu cha kwanza unapo amka asubuhi kunywa maji ya uvuguvugu kwa kuwa husaidia kukuchangamsha vizuri kuliko kahawa, yatachangamsha ini na mfumo wa umeng'enyaji wa chakula.
Kuvimbiwa na kukosa choo au kupata choo kigumu
Maji husaidia kulainisha njia ya utumbo, husaidia kuweka unyevunyevu ndani ya utumbo. Usipotumia maji ya kutosha, unajiweka katika hatari ya utendaji mbaya wa mfumo wa umeng'enyaji wa chakula na kusababisha kuvimbiwa, kukosa choo au kupata choo kigumu.
Ngozi kavu
Ikiwa wewe ni mkavu kwa nje kuna uwezekano mkubwa wa kuwa mkavu ndani ya mwili pia. Usitumie losheni na krimu kufunika tatizo, badala yake jitahidi kunywa maji ya kutosha.
Kuumwa kichwa
Kichwa kuuma ni kiashilia kwamba unahitaji maji, hivyo unapoumwa kichwa jitahidi kunywa maji. Dalili zingine ni kuhisi kiu, mdomo kukauka, kukosa mkojo au kiasi cha mkojo kuwa kidogo na wakati mwingine kuwa na rangi iliyokolea na harufu kali, udhaifu wa misuli na kuhisi kizunguzungu.
Kwanini ni muhimu kunywa kiwango sahihi cha maji?
Njia bora ya kuupa mwili maji ya kutosha ni kutii kiu chako kila unaposikia kiu inabidi unywe maji ya kutosha. Njia nyingine ni kuchunguza mkojo wako kwa makini kuanzia rangi na harufu yake, ikiwa una rangi nzito na harufu kali hii ina maana mwili hauna maji ya kutosha.
Kwa wale wanaofanya mazoezi, Dk. Huggins anasema; "Watu wengi hupoteza kati ya lita moja na mbili za jasho kila saa moja la mazoezi ya kawaida. Hivyo mtu anapaswa kurudishia maji yaliyopotea kuputia jasho ingawa kuhisi kiu bado ndio muongozo wa kunywa maji.
Ripoti ya makubaliano iliyochapishwa na jarida British Journal of Sports Medicine ilidai wana michezo wengi wako katika hatari ya kupatwa na Hiponatremia (upungufu wa chumvi ya natri katika damu) inayotokana na michezo tatizo linaloweza sababisha mtu kunywa maji mengi hivyo kusababisha kichefuchefu, kutapika, kuumwa kichwa, uchovu na wakati mwingine huweza kusababisha matatizo makubwa kama kupoteza fahamu na hata kifo.
Ili kujilinda na kupungukiwa au kutozidisha kiwango cha maji, ni vyema kuusikiliza mwili wako unachotaka. Kunywa maji safi na salama kwa kiasi kinachostahili kiafya kunaweza kuboresha maisha na kumfanya mtu ajihisi mwenye afya na furaha zaidi.