Utata wa vibali vya ARV wawafanya waathirika wa VVU kupoteza maisha KATIKA maeneo mengi ya Tanzania, kumezuka tatizo la waathirika wa Virusi Vya UKIMWI (VVU) kunyimwa madawa ya ARV kutokana na utata wa vibali uliomo katika sera ya afya ya taifa, na hivyo kupoteza maisha kwa sababu hiyo.
Watu wengi walioko vijijini wanaohama kutoka katika eneo kiliko kituo chao cha awali cha kuchukulia madawa hayo, wamekuwa wakipoteza maisha haraka baada yakunyimwa madawa hayo katika maeneo mapya wanakohamia. Waathirika hawa wamekuwa wananyimwa madawa hayo kwa sababu ya kutokuwa na vibali vinavyowaruhusu kupatiwa madawa hayo katika maeneo yao mapya walikohamia.
Tatizo hili pia linawakumba waathirika wanaosafiri kwa zaidi ya miezi mitatu kwenda nje ya maeneo ya makazi yao ya kawaida. Mtandao wa FikraPevu ulipata fursa ya kuongea na Waratibu wa Vituo vya Matunzo na Tiba kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya nchini, ambao wamethibitisha uwepo wa tatizo hili.
Waratibu hao wameieleza FikraPevu kuwa mwongozo wa Wizara ya Afya unawatakawatu wanaotumia ARVs kuomba kibali kipya cha kupewa dawa hizo pale wanapohamiaeneo tofauti, sharti ambalo wagonjwa wengi wanashindwa kulitimiza kwa sababu mbalimbali.
Kuhusiana na tatizo hili, Mratibu wa Kituo cha Matunzo na Tiba kwa watu wanaoishi navizuri vya UKIMWI, katika Hospitali ya Marangu ya Mjini Moshi, Dk. Joseph Msangi, ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kubadilisha utaratibu huo, kwa kuruhusu watu wanaotumia dawa hizo kupata dawa mahali popote kwa kutumia vibali vya awali.
Sambamba na tatizo la vibali, baadhi ya watumiaji wa dawa za kurefusha maisha wilayani Magu mkoani Mwanza (ambao hawakutaka majina yao yatajwe), wamelalamikia kutopatikana kwa dawa za ARV’s kwa muda muafaka, huku wakisisitiza kwamba uhaba wa dawa hizo hususani vijijini unachangia sana kukatisha mapema uhai wa baadhi yawaathirika.
Msangi aliifahamisha FikraPevu kwamba baadhi ya wagonjwa wenye vibali halali na wanaofika vituoni kupata dawa hizo wanazikosa. Hivyo, akaishauri serikali ianze kusambaza kwa kasi dawa za ARV kwenye Vituo, Zahanati na Hospitali ili kuwaondolea usumbufu waathirika wa VVU.
Naye mmoja wa waathirika aliyejitambulisha kwa jina moja la Saidi, mkazi wa Magu, amesema ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea, ni vyema serikali ikasogezahuduma ya utoaji wa dawa hizo katika zahanati zote za vijijini kuokoa maisha yawaathirika.
Kwa upande mwingine, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu, Athumani Pembe, akizungumzia hali ya ugonjwa wa UKIMWI ameifahamisha FikraPevu kwamba hakuna njia ya hakika ya kumtambua mtu aliyeambukizwa VVU zaidi ya vipimo vya maabara.
“Watu wanaoishi naVirusi Vya UKIMWI wanaweza kuonekana wazima na wasionyeshe dalili zozote za ugonjwa,” alisema Pembe. “Hata hivyo pamoja na kutokuonyesha dalili zozote, mtu huyu mwenye virusi anaweza akaambukiza watu wengine ikiwa atakuwa na mahusiano ya kimapenzi yasiyo salama,” aliongeza Pembe.
Hivyo, Pembe amewataka wagonjwa wa Ukimwi waepuke vitendo vya kujamiiana kwani hali hiyo inaweza kuwafanya washambuliwe na magonjwa mengine ukiwemo ugonjwa wa moyo. Kuhusu matumizi ya ARV’s, mmoja wa wataalam wa afya katika Halmashauri ya Wilayaya Kakonko mkoani Kigoma, aliwashauri waathirika wa VVU kutumia madawa hayo kwa kuzingatia vipimo sahihi.
“Matumizi madogo ya dawa hizo ni hatari kwani tabia hiyoinaondoa uwezekano wa mgonjwa kupata nafuu ya magonjwa nyemeleziyanayowasumbua, na hivyo kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi mapya yavirusi vya Ukimwi,” mtaalam huyo amesema.
“Wagonjwa wa UKIMWI wanaohitaji kuhudumiwa nyumbani kwao wakiwemo wale walio katika tiba ya kupunguza makali ya UKIMWI jamii isiwatenge bali iwasaidie huko huko ili waweze kuishi kwa matumaini bila shida ya kunyanyaswa kwa sababu ya hali yao,” aliongeza mtaalam huyo. Mtaalam huyu, aliyasema hayo baada ya kubainisha kwamba kuna wagonjwa ambao wamekuwa wakilalamikia kukosa huduma hiyo baada ya hali zao za kiafya kuwa mbaya na kutengwa na familia zao.
Virusi Vya UKIMWI vinapatikana katika damu na majimaji mbalimbali yanayotoka kwenye mwili na viungo vya uzazi vya wanawake na wanaume wenye uambukizo. Njia kuu ya kueneza virusi hivi, ni kujamiiana na mwathirika bila kutumia kinga.
Njia nyingine ya maambukizi ni kutoka kwa mama mjamzito aliye mwathirika kwenda kwa mtoto wake wakati akiwa tumboni, anapokuwa anazaliwa au wakati wa kumnyonyesha. Vimelea vya VVU pia huambukizwa kwa njia ya kuongezewa damu kutoka kwa mtu aliyeathirika.
Pia ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kwa kuchangia vifaa vyenye mabaki ya damu aliyoathirika. Vifaa hivyo ni kama sindano, mikasi, wembe, mipira ya kutolea mkojo au vifaa vya kutogea masikio.
The post Utata wa vibali vya ARV wawafanya waathirika wa VVU kupoteza maisha appeared first on Fikra Pevu.