Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Ukuaji na Maendeleo ya Mtoto Kiakili

$
0
0

Credit: Picha ya Mtandaoni

Kama mzazi au mlezi unayebeba majukumu yako kwa uzito, lazima ufuatilie ukuaji wa mtoto wako au unayemlea hasa ukuaji wa akili yake. Mtoto anapokua vizuri kiakili anaweza kuifadisha familia yake na jamii kwa ujumla katika kutatua changamoto zilizopo na kuleta maendeleo.

Kukua kiakili ni kuongezeka kwa ufahamu, uwezo wa kufikiri, kutafakari na kutatua matatizo kulingana na umri. Ukuaji na maendeleo ya mtoto kiakili unahusisha pia mabadiliko ya mtoto kitabia, usikivu, ubunifu, udadisi na jinsi mtoto anavyopokea na kutafsiri mambo mbalimbali katika mazingira yanayomzunguka.

Ukuaji wa ubongo wa mtoto unaanza tangu mimba inapotungwa. Imedhihirika kitaalamu kuwa ubongo wa mtoto hukua kwa kiwango cha asilimia 80 katika kipindi cha ujauzito hadi miaka 3 ya mwanzo ya maisha yake.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya mama mjamzito na ukuaji wa ubongo na akili ya mtoto. Hivyo ni muhimu mama mjamzito apewe mahitaji ya lazima, asifanye kazi nzito na ngumu, apewe upendo, apate muda wa kupumzika, mahala pazuri pa kulala, ahudhurie kliniki pamoja na kupata matibabu na ushauri wa kitaalam.

Hatua za Ukuaji na Uchangamshi wa Mtoto Kiakili

Mara mtoto anapozaliwa kuanza kujifunza juu ya mazingira anamoishi kwa kutumia milango ya fahamu (kwa kuona, kunusa, kusikia, kuonja na kugusa). Hivyo basi mtoto anapozaliwa wazazi na walezi wanatakiwa kuendelea na matendo ya uchangamshi yatakayochochea ukuaji kiakili hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka nane.

Miezi 0 – 6

Mtoto hufuata vitu vinavyopitishwa mbele yake, anavutwa na sauti, anaanza kutambua sauti za watu aliowazoea na anapenda kupeleka kila kitu mdomoni.

Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mpe vifaa safi na salama vya kuchezea, ongea naye kwa tabasamu na kumwonyesha upendo kwa kumpakata na kumkumbatia na kumwimbia nyimbo.

Miezi 7 – 12

Mtoto anaweza kuvumbua vitu kwa kujaribu kuvigonganisha, kuvirusha na kuchezea, anaiga na kutamka maneno mafupi. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake tumia mbinu zilizopo kwenye miezi 0-6 pamoja na kumsifu na kumpongeza.

Mwaka 1 – 2

Mtoto anavutiwa na vitabu vya picha, anaongea na kuuliza maswali mengi, anapenda kucheza muziki na kuimba, anaweza kuchagua kati ya vitu viwili anavyopenda na anaweza kutambua na kutofautisha vitu, watu, michoro na mazingira yanayomzunguka.

Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mpatie vitabu vya picha mbalimbali, kujibu maswali anayouliza, kumpatia vifaa vya muziki na kumpatia vifaa vya michezo.

Miaka 3 – 4

Mtoto anaweza kuonyesha na kutaja sehemu za mwili, anatambua matukio yoyote yanayotokea, anaweza kubadilisha maamuzi yake, anaweza kutofautisha vitu halisi na vya kuigwa, anapenda kuuliza maswali, anapenda kuwa na makundi rika.

Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake tumia mbinu zilizopo kwenye mwaka 1-2 pamoja na kusikiliza na kujibu maswali anayouliza kwa upole, upendo na usahihi, kumweleza na kufafanua vitu, mambo mbalimbali yanayojitokeza na kumpatia uangalizi wa kutosha.

Miaka 5 – 6

Mtoto anaweza kujieleza kwa ufasaha, anaweza kusoma, kuhesabu na kuandika, anaweza kusimulia hadithi na matukio mbalimbali. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake tumia mbinu zilizopo kwenye miaka 3-4 pamoja na kumhamasisha na kumhimiza kujifunza.

Miaka 7-8

Mtoto anaweza kufanya maamuzi ya busara, anaheshimu mawazo ya wengine, anao uwezo wa kutatua matatizo, stadi za mawasiliano zinaongezeka, anafikiri na kufanya vitu kwa makini, anatega na kutegua vitendawili.

Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mshirikishe katika maamuzi, kumpatia stadi zitakazomjengea uwezo wa kufanya maamuzi, kumjengea stadi ya mawasiliano, kumpa kazi zitakazomfanya afikiri, kumjengea uwezo wa kusaidia wengine, kumpongeza na kumsifia anapofanya vizuri.

Mambo yanayochochea Ukuaji na Maendeleo ya Mtoto Kiakili

Mahusiano na Wazazi, Walezi na Ndugu wa Karibu

Mahusiano mazuri yenye amani miongoni mwa wanafamilia na ndugu wa karibu ni muhimu katika kumkuza na kumwendeleza mtoto kiakili.

Hivyo wanandugu mmoja mmoja au kwa pamoja wanalo jukumu la kuhakikisha kuwa wanamfanyia mtoto vitendo changamshi vitakavyochochea ukuaji wa mtoto kiakili.

Kwa mfano, kitendo cha kumkumbatia na kumpakata mtoto kinamjengea hali ya kujiamini, ujasiri na kujitegemea na kuhisi yuko salama. Familia zenye mifarakano huathiri ukuaji wa mtoto kiakili.

Inashauriwa kwamba mzazi au mlezi apate muda wa kucheza na mtoto ili ajenge msingi imara wa mahusiano mazuri ambayo humfanya awe na furaha, kuwapenda na kuwajali watu wengine. Pia kuwahimiza kuthubutu kufanya mambo wanayoyaona ni magumu.

Vifaa na michezo kwa mtoto

Vifaa na michezo kwa mtoto ni muhimu katika kumkuza na kumwendeleza kiakili. Katika miezi ya mwanzo baada ya kuzaliwa, mtoto anasaidiwa kucheza kwa kusemeshwa, kurushwarushwa na kuimbiwa.

Katika ukuaji wake mtoto anapofikisha miezi mitatu ni vizuri aongezewe vifaa vya kuchezea vyenye rangi mbalimbali za kuvutia vinavyotoa milio kama kengele, manyanga au kayamba.

Kwa kadiri mtoto anavyoendelea kukua na kujimudu anahitaji vifaa vya kuchezea kama vile, mipira, kamba, vipande vya mbao, makopo, makasha ya karatasi, udongo wa mfinyanzi, vifuu, mchanga, kete ili aweze kukuza stadi za lugha, udadisi na ugunduzi.

Mazingira yanayomzunguka Mtoto

Mtoto anahitaji kuwekewa mazingira safi, salama na ya kusisimua. Mazingira hayo ni pamoja na mahali safi pa kulala, vifaa safi vya michezo ambavyo ni salama na vya kusisimua vinavyomwezesha kujifunza kama vile, vyenye rangi mbalimbali za kuvutia. Mazingira hayo hukuza na kujenga afya ya akili ya mtoto.

Wakati huo huo, serikali kupitia wizara zinazohusika na malezi ya awali kwa mtoto zina mchango mkubwa wa kuandaa mazingira yatakayowezesha familia, jamii na asasi mbalimbali kutoa malezi na uchangamshi wa awali kwa mtoto.

Mazingira hayo yanajumuisha sera, miongozo na uelimishaji jamii kuhusu malezi na uchangamshi wa awali.

Kwa kushirikiana na wadau, serikali pia inalo jukumu la kuhamasisha jamii na mashirika ili yaanzishe programu za malezi na uchangamshi wa awali kwa mtoto.

 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles