MOYO ni ogani muhimu sana katika mwili. Inafanya kazi muda wote hata wakati ambapo umechoka sana au kulala.
Kazi kubwa ya ogani hii ni kusukuma damu sehemu mbalimbali za mwili kama kichwani hadi miguuni. Kuwa na moyo wenye afya njema kunachangia afya njema kwa ujumla na maisha yenye furaha.
Kutokula mlo bora, kutofanya mazoezi, kuvuta sigara na maradhi ya moyo huharibu afya ya moyo wako.
Nini sababu za Moyo kupanuka?
Moyo kupanuka au kuwa mkubwa (Cardiomegaly) siyo ugonjwa bali ni hali inayotokana na ugonjwa au tatizo katika mwili.
Kupanuka kwa moyo kunasababishwa na hali zote ambazo husababisha moyo kusukuma damu kwa nguvu ya ziada tofauti na kawaida kitu kinachosababisha misuli ya moyo kuharibika.
Wakati mwingine moyo hupanuka bila sababu zinazojulikana moja kwa moja. Na wakati mwingine moyo unaweza kupanuka kwa kipindi kifupi kutokana na mgandamizo kwenye mwili wako, mfano, ujauzito.
Tatizo la moyo ulilozaliwa nalo, kuharibika kwa moyo kutokana na mshtuko wa moyo, kudhoofu kwa misuli ya moyo au moyo kutodunda kwa mpangilio, vyote vinaweza sababisha moyo kupanuka.
Hali gani za kiafya zinazohusiana na Moyo kupanuka?
1. Kupanda kwa shinikizo la damu. Hali hii husababisha moyo kusukuma damu kwa nguvu zaidi ili kufikisha damu sehemu mbalimbali za mwili, hali inayosababisha misuli ya moyo kutanuka na kuwa minene hivyo kufanya moyo mkubwa.
Kupanda kwa shinikizo la damu kunaweza kusababisha ventrikali ya kushoto kupanuka na kufanya misuli ya moyo kudhoofika. Shinikizo la juu la damu, pia hufanya sehemu ya juu ya moyo (Atria) kutanuka.
2. Ugonjwa wa misuli ya moyo (Cardiomyopathy). Ugonjwa huu husababisha misuli ya moyo kukakamaa na kusababisha moyo kujaribu kusukuma damu kwa nguvu zaidi kitu kinachoweza kusababisha moyo kupanuka.
3. Kupanda kwa shinikizo la damu kwenye mshipa wa damu (Artery) unaounganisha moyo na mapafu. Hali hii hujulikana kitaalamu kama Pulmonary Hypertension. Hii husababisha moyo kusukuma damu kwa taabu kati ya mapafu na moyo, hali ambayo husababisha upande wa kulia wa moyo kutanuka au kuwa mkubwa.
4. Kuwepo maji kuzunguka moyo (Pericardial Effusion). Maji kukusanyika kwenye mfuko (Pericardium) unaobeba moyo huweza kusababisha moyo kuonekana mkubwa hasa baada ya kupiga picha ya x-ray ya kifua.
5. Upungufu wa damu mwilini. Kuwa na kiwango cha chini cha chembe hai nyekundu za damu hufanya ubebaji mdogo wa oksijeni kwenda sehemu mbalimbali za mwili, hivyo ili moyo kuweza kusambaza oksijeni kwa mwili wote husukuma kwa haraka zaidi na kusababisha moyo kupanuka au kuwa mkubwa.
6. Matatizo ya tezi (Thyroid Disorders). Ikiwa tezi zitatoa homoni kwa kiwango kikubwa au kidogo vyote vinaweza kusababisha matatizo ya moyo yanayojumuisha moyo kupanuka au kuwa mkubwa.
7. Kuwepo kwa wingi wa madini chuma mwilini (Hemochromatosis). Hali hutokea pale mwili unaposhindwa kutumia madini chuma vizuri na kusababisha madini haya kujijenga kwenye ogani mbalimbali za mwili ikiwa ni pamoja na ndani moyo. Kuwepo kwa madini chuma kwenye moyo husababisha kupanuka kwa ventrikali ya kushoto kutokana na kudhoofu kwa misuli ya moyo.
8. Magonjwa ya moyo kama Amyloidosis. Ugonjwa huu hutokana na protini isiyo ya kawaida inapozunguka kwenye damu, ambayo inaweza kufika kwenye moyo na kuziba baadhi ya mirija ya moyo hivyo kuingilia utendaji wa kawaida wa moyo na kufanya moyo kupanuka au kuwa mkubwa.
Nini Matibabu ya Moyo uliopanuka?
Moyo kupanuka huonekana kwa picha ya X-ray ya kifua ingawa vipimo vingine vinahitajika ili kubaini ni nini kinasababisha moyo kupanuka.
Baadhi ya watu wenye moyo mkubwa hawana dalili za moja kwa moja ingawa wengi hupata dalili kama kupumua kwa taabu, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, kujaa/kuvimba kwa mwili hasa miguu, kifua kuuma, kizunguzungu, kupoteza fahamu na kuzimia.
Moyo kupanuka ni hali ambayo inaweza kutibiwa kwa urahisi ikiwa itagundulika mapema, hivyo ni vyema kutafuta msaada wa kitabibu ikiwa unapata dalili yoyote kati ya hizo hapo juu. Matibabu ya moyo mkubwa yanaweza kuhusisha matumizi ya dawa, kubadili mfumo wa maisha na wakati mwingine upasuaji.