Babu wa Loliondo, Mchungaji Mwasapila, akitoa huduma ya 'kikombe' kwa 'wagonjwa' wake
SIYO jambo geni kila kukicha kusikia matangazo kwenye radio na runinga kuhusiana na kliniki ama zahanati zinazotoa tiba asilia na tiba mbadala zikitangaza dawa za magonjwa mbalimbali.
Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 kumezuka wataalamu wengi waliojiingiza kwenye ujasiriamali wa tiba asilia ambao wamekuwa wakijipambanua kuwa na uwezo wa kutibu watu kwa kutumia tiba asilia.
Ujasiriamali huu wa wataalamu wa tiba asilia umeshika kasi na wahusika wengi wamekuwa mamilionea kutokana na huduma wanazozitoa kugharimu fedha nyingi kwa wagonjwa, hivyo wenyewe kuzidi kujilimbikizia utajiri.
Lakini swali la kujiuliza ni je, afya za Watanzania sasa ziko mikononi mwa matabibu hawa wa tiba asilia?
Watu wengi waliopitia kwa matabibu hao wamesema wamewasaidia kwa kiwango kikubwa japokuwa wametumia gharama kubwa kupata matibabu hayo.
Ikiwa matabibu hao wanasifika hivi kwa watu je, hii inaleta maana gani kwa hospitali zetu zitoazo tiba za kisasa?
Tangu kufunguliwa milango kwa soko huria Tanzania, huduma za jamii zimegeuzwa kuwa bidhaa kwa mujibu wa sera za kibepari. Biashara hiyo ya kuuza huduma za jamii imeshamiri sana Tanzania ambapo inazidi kuwatajirisha mabepari uchwara hawa kila kukicha.
Hebu tazama wimbi la ongezeko la hospitali na shule binasfi Tanzania hivi leo ambapo wananchi wameendelea kutozwa gharama kubwa ili kupata huduma hizo.
Kutokana na ubovu wa huduma katika hospitali zetu za serikali, watu wamegeuzia fikra zao kwa zahanati za tiba asilia ambapo hupata tiba ya magonjwa sugu kama vidonda vya tumbo, uzazi, kisukari, uvimbe mbali mbali mwilini, saratani, shinikizo la damu na magonjwa mengineyo mengi yamekuwa sehemu kubwa ya matangazo yatolewayo na zahanati hizo.
Kubwa zaidi linalowapeleka huko watu wengi, ni matangazo ya kutibu matatizo ya nguvu za uzazi – kwa wanawake na wanaume – tatizo ambalo kwa sasa linawakabili watu wengi katika jamii, hususan wanandoa, ambapo wanaposikia mahali kuna tiba hukimbilia ili kuzinusuru ndoa zao.
Lakini kunamaswali muhimu ya kujiuliza. Kama zahanati hizo za tiba asilia zinaweza kutoa huduma kwa magonjwa yote hayo, je, hizi tafiti walizifanya wapi? Na kama wao wameweza, kwanini Wizara ya Afya kwa kupitia taasisi zake kama Hospitali ya Muhimbili na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR) zisiweze kufanya tafiti hizo na kutoa tiba kama hizi za asili? Au ndiyo tuseme uhuru wa soko huria umefanya mabepari uchwara kutumia fursa na kutumia afya za Watanzania kama mtaji wao?
Hivi ni nani mwenye dhamana ya afya kati ya serikali na mwananchi? Je, ni kwa kiwango gani zahanati hizi za tiba asilia hukaguliwa kuona ubora wa huduma watoazo? Au wahusika wenye dhamana na afya zetu hubaki kukagua vyeti walivyonavyo matabibu hawa?
Hii inanikumbusha wakati ule kilipokuja ‘kikombe cha babu’ ambapo Watanzania wengi pamoja na viongozi wetu wa serikali walikimbilia huko kupata ‘kikombe’ ili kunusuru afya zao. Sina uhakika ni kwa kiasi gani walipona magonjwa yao wakati ule, kwani sharti kubwa lilikuwa uwe na imani na bila ya imani huwezi kupona. Isitoshe, taasisi za afya za serikali zilichukua sehemu ya dawa ile ili kwenda kuifanyia uchunguzi kujua inatibu nini hasa. Je, majibu ya tafiti hizo yako wapi ili Watanzania tujue tulikuwa tunakunywa nini?
Wimbi la zahanati za tiba asilia linatia mashaka na kubaki kujiuliza ni kwa kiasi gani tunafaidika na huduma watoayo ama ni sehemu ya kuendeleza kutunyonya wavuja jasho maskini kwa jina la soko huria liliyobeba dhana ya matibabu.
Ni wapi ambako taaluma hiyo ya tiba asilia inapatikana, maana kila anayeanzisha kituo chake anasema ‘nimejifunza kutumia mimea na matunda’, amejifunza wapi na nani aliyemfundisha na ni kwa kiwango gani mafunzo hayo yanaweza kutathmini ubora wa huduma hiyo?
Nijuavyo mimi taaluma ya matibabu ya afya ni yakisayansi na inapaswa kufanyiwa tafiti nyingi ili kujua aina ya dawa zitakazoweza kutibu magonjwa kwa wanadamu n ahata wanyama pia. Ikiwa hawa wataalamu wa tiba asilia wanasomea – sijui ni wapi – kwa nini ishindikane kufanywa na wataalamu wetu wa afya?
Ukisikiliza vile ambavyo dawa za tiba asilia zinatangazwa huleta hamasa kubwa na kuonyesha matibabu hupatikana kirahisi. Sasa kama dawa hizo zimeruhusiwa kutumika na Watanzania ni vyema zikawekwa kwenye maduka ya dawa na hosipitali za serikali badala ya kuzikuta kwenye zahanati zao tu.
Wakati wa serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli tumeanza kuona tone la matumaini katika hili, japo sijui muendelezo wake ni wa kiasi gani. Wameanza kutembelea na kufanya ukaguzi katika baadhi ya zahanati za tiba asilia na kutambua wengine wamesajiliwa na wengine hawajasajiliwa.
Haijajulikana ni vigezo gani ambavyo serikali inatumia kuzihalalisha zahanati hizo na kama taasisi za serikali kama Shirika la Viwango vya Ubora (TBS) na Taasisi ya Chakula na Dawa (TFDA) zinahusika katika kupima dawa hizo na kuzithibitisha kwamba zinafaa kwa matumizi ya binadamu.
Ni kweli nchi inataka kupata kodi kutoka kwa mabepari uchwara hawa, lakini ni lazima kutambua huduma inayotolewa, kwa faida ya nani, kwa ubora gani na kadhalika badala ya kukazania kutoza kodi.
Kuwatoza kodi watalaamu hao kuna maana moja tu kwamba, tayari wamethibitishwa, hivyo ikiwa tiba zao zitaleta madhara watachukuliwa hatua kwa makossa ya uzembe wa utaalamu, siyo kwa kuwapatia wananchi tiba isiyostahili wala kuthibitishwa, ambayo inaweza kuwa sumu inayowaua pole pole.
Tumeshuhudia nchi yetu ikiendeshwa kwa matukio ambapo mpaka janga fulani litokee ndipo tuweke katazo ama kuzinduka.
Turejee wakati wa bendi ya Meridian Biao mwaka 1994 na hata wakati wa ‘DECI’, baada ya watu kurubuniwa pesa zao ndipo serikali ikaingilia kati. Ilipotokea milipuko ya mabomu Mbagala na Gongo la Mboto ndipo watu wakaambiwa wakae umbali gani na maeneo ya jeshi.
Kwanini isifike mahali sasa tujifunze kuchukua kinga kabla Watanzania wavuja jasho hawajaumia ndipo tuzinduke?
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kitabu chake cha ‘Reflection on Leadership in Africa’ ameeleza: “Ni ukweli usiopingika kuwa masuala ya maendeleo ni masuala halisi na hayawezi kuwa masuala ya ubabaishaji tu”.
Afya ni sehemu muhimu ya maendeleo nchini kwetu na inatupasa kuzingatia kwa dhati na hayahitaji ubabaishaji zaidi ya kutumia taaluma zetu kufanya tafiti zitakazoonyesha nini kinafaa na nini hakifai.
Kwa hali ilivyo sasa, itafika mahali hospitali zetu hazitaaminika tena na wengi wetu tutakimbilia katika zahanati hizi za tiba asilia, ambako ukitizama kwa undani utagundua gharama katika zahanati hizi hazina unafuu wowote zaidi ya kuendelea kutunyonya kama vile wafanyavyo mabebari uchwara wengine katika sekta ya elimu na viwanda.
Ifike mahali sasa, serikali na idara zake muhimu za afya kuliangalia jambo hili kwa kina ili kuwaondoa hofu Watanzania wajue wanapata tiba ya namna gani badala ya kuendelea kupata tiba ya ‘kunywa vikombe’ bila uhakika kama ni tiba sahihi huku wakizidi kuwatajirisha watoa huduma.