Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar
WAKATI wanajamii wametakiwa kuwathamini wagonjwa maalum wa matatizo ya akili, imeelezwa kwamba hospitali ya Zanzibar Mental iko katika hali mbaya mno.
Taarifa zinaeleza kwamba, baadhi ya wagonjwa katika hospitali hiyo iliyopo Mnazi Mmoja kisiwani humo ambayo ni Hospitali Kuu na pekee ya wagonjwa wa akili iliyopo kitengo cha afya ya akili katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, wanakosa huduma muhimu za matibabu na inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa vitendea kazi na vyumba (wodi) za wagonjwa.
Uchakavu wa vifaa na majengo katika hospitali hiyo unatokana na umri mrefu wa majengo, kwani tangu hospitali hiyo ilipojengwa mwaka 1940, ukarabati wake umekuwa ni wa kusuasua.
Mkurungezi Mkuu wa hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk. Jamala Adam, amesema: “Kitengo hiki kinawahdumia wagojwa 70, kati yao 41 wako katika hali mbaya ya afya ya akili, wengine mahututi, na kuna wodi mbili tu kiasi ambacho hazitoshi kulingana na wingi wa wagonjwa hao.”
Akaongeza: “Wanapaswa kutengwa makundi makundi kwa kuchukuliwa hali zao za afya zinavyozidiana, maana walioathirika zaidi hawapaswi kuchanganywa na wengine kwani kuna wanaotaka hata kuwadhuru wenzao, lakini hapa hatuna jinsi, tumetenganisha tu wodi moja ya wanaume na nyingine ya wanawake, hii ni hatari.”
Mmoja wa watoa huduma hospitalini hapo, daktari na mwanasaikolojia Mariam Hamduni, amesema hospitali ina ukosefu wa dawa na wahudumu ambapo hali si ya kuridhisha ikiwemo majengo kuchakaa, kukosekana kwa ofisi za kufanyia kazi, hivyo kuiomba serikali iwasaidie ili kunusuru afya za waathirika na matatizo yao yatibike kabla hayajawa sugu.
Matatizo haya katika Hospitali ya Mental ya Zanzibar, si mara ya kwanza kutokea, mwezi Juni, 2014 iliripotiwa na vyombo vya habari kuhusu ulaji wa mlo mmoja kwa siku wa wagonjwa, kulala gizani hali ambayo ilielezwa kwamba inatokana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushindwa kulipa kipaumbele jambo hilo la afya za watu hao wenye mahitaji maalum.
Takwimu zinaonyesha kuwa, kiwango kikubwa cha wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo wengi wao na hasa wavulana matatizo yao yanatokana na utumiaji wa dawa za kulevya, pia ugonjwa wa malaria na matatizo ya kibinadamu ya kawaida vinatokea kwa uchache vikiwa chanzo cha matatizo hayo ya akili.
Vile vile, viongozi wa serikali wanatupiwa lawama, kwani inasemekana hawafiki hospitalini hapo ili kuweza kujionea hali ilivyo mbaya na matatizo waliyonayo, badala yake ni wasamaria wema tu ndio hufika mara moja moja na kutoa misaada midogo midogo.
Muuguzi mmojawapo wa wodi ya wanaume, Mohammed Suleiman, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema; “Kuna baadhi ya dawa hazipo kabisa, na ni muhimu sana kwa kwa dozi za wagonjwa hao, hii ni hatari kwani inarudisha maendeleo ya matibabu nyuma.”
Jambo lingine linalowakumba wagonjwa hao ni kukosa huduma za mlo kamili, kwani hutumia dawa kali sana zinazohitaji kula chakula cha kutosha.
Inaelezwa pia kwamba, ndugu na jamaa wa wagonjwa hao wanawatelekeza hospitalini hapo bila hata kuwajulia hali.
Dk. Jamala Adam amekiri kuwepo kwa hatua za kurekebisha udhaifu huo kutoka serikalini kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi ya Afrika (BADEA).
Uongozi wa hospitali tayari umeahidiwa kuwasomesha wauguzi na madaktari wengine, kukarabati miundo mbinu ya hospitali ikiwemo kujenga jengo jipya maalum la wagonjwa pamoja na kuweka mikakati ya upatikanaji wa dawa kwa wakati.
Aidha, Dk. Adam, anatoa wito kwa wanajamii kwa ujumla ambao wagonjwa wao wakiruhusiwa kwenda nyumbani hukosa huduma sahihi, kuacha tabia za kuwatelekeza.
“Kuna baadhi ya wagonjwa wanatakiwa kunywa dawa katika maisha yao yote, kinyume na hapo ugonjwa unarejea tena, sasa kama familia inashindwa kumsimamia mgonjwa ipasavyo matokeo yake ugonjwa unamrudia kwa kasi na kufanya arejeshwe hospitali tena, janga ambalo ndilo kuu hospitalini hapa,” anaeleza.