WAKATI serikali ikifanya mikakati mbalimbali ya kuthibiti dawa za kulevya na madhara yake kwa waathirika kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kupambana na athari za madawa hayo nchini, wapo wananchi wanaounga mkono mpango huo na wengine wanaona haufai bali ni kichocheo kikubwa cha kuendeleza matumizi ya dawa hizo.
Fikra Pevu katika mijadala yake mingi imebainisha kuwepo kwa matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini, licha ya serikali kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti suala hilo huku wengi wakiathiriwa na madawa na wengine wakikamatwa lakini inashindikana kuwa funzo kwa wengine.
Utegemezi wa dawa za kulevya ni ugonjwa sugu lakini unaotibika, matibabu yake hupatikana baada ya kuleta madhara au kabla ya madhara ambapo mhusika huwahi na kuacha mwenyewe au kulazimishwa na wengine kuacha.
Kwa watu wengi, matumizi ya dawa za kulevya hugeuka sugu, na kurejea matumizi huwezekana hata baada ya muda mrefu wa kuacha. Kama ugonjwa sugu unaorejea rejea, kulevya kunahitaji matibabu endelevu ili kuondoa kabisa athari za madhara.
Kuna Watanzania wengi ndani na nje ya nchi walioathirika kwa matumizi ya dawa za kulevya, huku mtandao wa uuzwaji wa dawa hizo pia ukishika kasi, cha kushangaza ni wahusika wa matukio hayo ni watu walioaminika na kuonekana kuwa kioo cha jamii.
Takwimu kutoka Umoja wa Mataifa zinabainisha kuwa, Afrika Mashariki imekuwa kinara wa kupokea na kusafirisha dawa kwenda nchi za nje, pengine na vigogo wakihusika.
Mwanadada aliyewahi kung’ara kwenye tasnia ya muziki wa bongo fleva nchini na Afrika Mashariki, Rehema Chalamila ‘Ray C’, ameathirika kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya na kumletea madhara makubwa ya kiafya na kiakili pia.
Pia msanii Rashidi Abdallah Makwiro maarufu kama Chid Benz, naye ameathirika sana na matumizi ya dawa za kulevya, japo naye ameingia katika kundi la watu wanaopatiwa matibabu ya kuondoa madhara ya sumu ya dawa hizo mwilini.
Taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii, inabainisha kuwepo kwa wasanii wengi zaidi ya hao wawili wanaojihusisha na matumizi ya dawa hizo.
Wanasemaje wanajamii kuhusu matibabu kwa waathirika?
Matibabu ya utegemeaji wa dawa za kulevya hutofautiana kulingana na aina ya dawa husika, kiasi cha dawa kilichotumika, muda wa utegemeaji wa dawa za kulevya, matatizo ya kiafya na mahitaji ya kijamii ya mtu binafsi.
Matumizi ya dawa ya kuondoa madhara ya dawa za kulevya aina ya Methadone kwa waathirika yanaonekana kama kuwatia kiburi cha wao kuendelea kutumia dawa za kulevya zaidi.
Hali halisi inaonyesha kuwa, mpango wa utoaji wa matibabu utaongeza maradufu utumiaji wa dawa za kulevya, kwani watu hutegemea kupona pindi wakiathirika, hivyo hutumia bila woga.
Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alimsaidia sana Ray C katika kufanikisha kupata matibabu, lakini jitihada zake hazikuleta mafanikio ya muda mrefu, kwani dada huyo amerudia hali yake ya kawaida na hali yake kuendelea kuathirika Zaidi.
Baadhi wengine wanaunga mkono suala la matibabu.
Hili ni janga kama majanga mengine ya kitaifa, hivyo watu wapewe matibabu ili warudie hali yao ya awali, na kuwaa hakuna haja ya kuwanyanyapaa.
Wanaona uwepo wa mahali pa kupatia matibabu ni lazima ili waathirika wapewe dawa.
Serikali na jamii kwa ujumla inapaswa kufanya yafuatayo kutokomeza suala hili.
Pengine wakashauri Kwamba, upunguzwe upatikanaji wa dawa za kulevya kwa kuimarisha operesheni za ukamataji wa dawa za kulevya mitaani.
Kuteketeza mashamba ya bangi, Kuongeza utoaji elimu juu ya athari za dawa za kulevya kupitia vyombo vya habari, mikutano, semina, matamasha, sanaa na michezo, kuwa na sera na sheria madhubuti za kupambana na tatizo la dawa za kulevya.
Aidha, mapendekezo ya Watanzania wengi yamebainisha kuwa, kuwepo kwa matibabu hakuna tija kwani huongeza kwa kasi watumiaji kuendelea kutumia dawa kwa kujipa moyo kuwa watatibiwa.
Serikali imejipangaje
Rais wa awamu ya tano, Mweshimiwa John Magufuli, ametoa tamko la kuvunja mtandao kuhusu wavurugaji wa amani katika utumiaji wa dawa za kulevya.
Rais Magufuli alitoa maelekezo mahsusi kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga akielekeza kuwa anataka kuiona Tanzania isiyokuwa na wauzaji wala watumiaji ‘unga’.
Rais Magufuli pia amewahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema, haiwezekani wauza unga wakawa na nguvu kuliko Serikali, na hivyo kuahidi kupambana nao.
Pengine juhudi za kukomesha janga la dawa za kulevya linakwama hapa nchini kwa sababu, ripoti mbalimbali kutoka katika baadhi ya vituo vya usalama nchini zinaonesha kuwa baadhi ya wahusika katika mtandao wa madawa, ni wale wenye dhamana ya kukataza matumizi ya madawa.
Serikali ya Awamu ya Nne, iliamua kupambana na dawa za kulevya kwa kubadili sheria na ikaelekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, lakini hadi sasa mpango huu unaonekana kusuasua na kuingiliwa upya na rais wa sasa mweshimiwa Magufuli.
Matumaini makubwa ya Watanzania sasa yapo mikononi mwa Rais Magufuli, kwani inaelezwa kuwa yeye hana ushirika, huruma wala hofu na wafanyabiashara ambao baadhi yao wanafanya biashara ya dawa za kulevya.
Ni wajibu wa kila mwanajamii kukataa janga hili la dawa za kulevya, kwani limekuwa tatizo linalowafanya wapendwa wetu kupata matatizo na madhara makubwa kiafya huku wahusika wakibaki kuwa tegemezi kwa kupoteza nguvu kazi.