Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Tanga: Wajawazito wazalishwa kwa mwanga wa vibatari

$
0
0

WAJAWAZITO wanaokwenda kujifungua nyakati za usiku katika Zahanati za Kiberashi na Negero katika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, wameililia Serikali kutaka msaada kufuatia zahanati hizo kukosa vitanda vya kujifungulia na kulazimika kujifungua watoto kwa kutumia mwanga wa vibatari/koroboi.

Wahudumu wa afya katika vituo hivyo, wameidokeza FikraPevu kuwa wanalazimika kutumia taa aina ya vibatari kumhudumia akina mama wajawazito wakati wa kujifungua, kutokana na ukosefu wa huduma za nishati ya umeme katika hospitali hizo na kukosekana kwa vitanda kwa ajili ya kundi hilo.

Wakizungumza na FikraPevu kwa nyakati tofauti, baadhi ya wagonjwa katika zahanati hizo wameitaka Serikali kuharakisha zoezi la uwekaji umeme kutokana na kuhofia afya za akina mama wajawazito wanaopelekwa kupatiwa msaada wa huduma ya kujifungulia katika kituo wananchoamini kina wataalamu watakaosaidia kutatua matatizo yanayoweza kujitokeza tofauti na kujifungulia majumbani.

Imeelezwa kuwa wakati mwingine wajawazito wanapopelekwa katika moja ya Zahanati hizo kwa ajili ya kujifungua, wanaagizwa kwenda kununua mafuta ya taa kwa ajili ya kuweka katika vibatari na kuwa wakati mwingine wajawazito wanalazimika kutandikiwa magunia chini kwa ajili ya kujifungulia kutokana na ukosefu wa vitanda.

Akielezea hali hiyo Mganga Mkuu wa Zahanati ya Kibirashi, Agustino Semizigi, amekiri kuwepo na tatizo la ukosefu wa umeme katika zahanati hiyo na kuwa wahudumu wanalazimika kutumia mbinu mbadala kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na kuokoa maisha ya wajawazito.

Amebainisha kuwa zoezi la usambazaji wa nyaya za umeme katika jengo la Zahanati hiyo umeshafanyika, lakini hadi sasa umeme haujaunganishwa kwa zaidi ya miaka mitatu ambapo ameitaka serikali kuharakisha zoezi hilo ili kunusuru maisha ya Mama na mtoto.

Juhudi za kumtafuta Mkuu wa wilaya, Selemani Liwowa, hiyo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, maisha ya wajawazito katika maeneo mbalimbali nchini hususani vijijini yako hatarini endapo jitahada za kuzipatia umeme zahanati zilizoko katika mazingira hayo hazitafanyiwa kazi.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>