IDADI ya wanaume wanaopima vinasaba (DNA) ili kubaini uhusiano wao wa kibaiolojia na watoto waliozaliwa na (wake au wapenzi wao), imezidi kuongezeka katika Mkoa wa Kilimanjaro, hali ambayo inaelezwa kuchangiwa na kukosekana kwa uaminifu baina ya wanandoa wengi FikraPevu imebaini.
Taarifa kutoka mkoani humo zinaeleza kuwa, mbali na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaohitaji huduma hiyo, imeelezwa kuwa kumeendelea kuwepo kwa ongezeko kubwa la wazazi wa kiume kubambikiziwa watoto ambao hawakuwazaa na wake zao wa ndoa au wapenzi wao, jambo ambalo limetajwa kuongeza mwamko wa wanaume kujitokeza na kuhitaji kupimwa DNA ili kujiridhisha na kuondoa mashaka baina ya familia nyingi mkoani humo.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Ustawi wa Jamii mkoani humo, zimebainisha kuwa mwamko wa watu wanaojitokeza kupima DNA, ili kuondoa malalamiko na kero ambazo zimekuwa zikisababisha watoto wengi kukosa haki zao za msingi (malezi ya wazazi wote wawili) imeongezeka mara dufu kuliko miaka iliyopita hadi kufikia leo.
Aidha, wakazi wa mkoa huo wameieleza FikraPevu kuwa kumekuwepo na tatizo kubwa la kukosekana kwa uaminifu baina ya wanandoa na wapenzi wao, kitendo ambacho kimekuwa likiibua kesi na migogoro mingi kwa watu hao kuhusiana na uhalali wa watoto waliozaliwa au wanaowalea na hivyo kupelekea wanaume wengi kuhitaji kupimo hicho ili kujiridhisha na watoto wao.
Katika kipindi cha mwaka 2013/2014, Ofisi hiyo ilipeleka maombi 18 ya DNA kwa Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kaskazini-mkoani Arusha, ambapo watoto 11 kati ya maombi hayo walionekana kuwa ni watoto halali huku watoto Saba wakionekana kuwa si watoto halali wa baba waliotajwa kuwa ni wao huku wakiendela kutoa matunzo kama familia na mara baada ya hali hiyo familia nyingi zimesambaratika.
Sampuli moja ya kipimo hicho inatajwa kuwa ni kati ya shilingi 100,000 na kwamba ili kupima sampuli tatu kwa maana ya Baba, Mama na mtoto zinahitajika shilingi 300,000 ambapo hali hiyo inasababisha mzozo mkali baada ya mmoja wao kudai hana uwezo wa kumudu gharama za vipimo.
Hata hivyo, moja ya changamoto zinazotajwa kukwamisha zoezi hilo ni pamoja na majibu yake kuchukua muda mrefu wa miezi mitatu hadi Sita au zaidi, jambo ambalo limetajwa kuwa linasababisha usumbufu mkubwa baina ya walengwa ambao wanakuwa na hamu ya kujua ukweli kuhusiana na matatizo ya kifamilia.
Ripoti ya Mkemia Mkuu
Ripoti hiyo Mkemia Mkuu wa Serikali Nchini, ya mwaka 2013 ilisema zaidi ya asilimia 48 ya wanaume waliojitokeza kupima vipimo vya vinasaba (DNA), waligundulika kubambikiziwa watoto ambapo takwimu za vipimo hivyo vilichukuliwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2010.
Tangu kuanza kwa utaalamu huo mwaka 2010 hadi kufikia mwaka 2012, mafanikio makubwa yalipatikana kwa kutatua mashauri na kuwatambulisha watu uhusiano wao pamoja na kubaini watoto hao, pia matukio mengine yaliyotumia teknolojia hiyo katika utatambuzi wa mauaji, majanga ya kimaumbile, ubakaji, wizi, utambuzi wa binadamu na jinsia tawala.