Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Ununuaji holela wa Dawa wa Wananchi unadidimiza Afya zao

$
0
0

Mara nyingi matumizi ya dawa muhimu zijulikanazo kama vijiuasumu au ‘antibayotiki’ zinazopatikana kwenye maduka ya dawa muhimu zisipotumiwa ipasavyo, vinadhuru afya ya mgonjwa kutokana na mazoea ya kutumia dawa pasipokuwa na cheti cha mtibabu kutoka kwa daktari. Uuzaji wa dawa za binadamu kwa njia hiyo unatajwa kama njia moja wapo ya wafamasia kujipatia kipato.  

Sifa kubwa ya famasia hizo zilizo nyingi katika kila mahali nchini, hua na wauzaji wasiokuwa na sifa sahihi wala uzoefu wa kitabibu unaomwezesha kutoa huduma sahihi kwa wateja. Hilo linafanya watumiaji kuweza kununua dawa zozote zilizopo katika famasia hiyo kuuziwa hata wasipokuwa na cheti toka kwa daktari kwa ajili ya kupatiwa dawa za ugonjwa husika.

Wananchi wamekua na tabia ya kununua dawa tokana na uzoefu tegemeana na ugonjwa wanaoumwa, hadi pale wanapozidiwa ndiyo hulazimika kwenda hospitalini kwa ushauri zaidi wa daktari. Hata hivyo, hali hii imeelezwa na wananchi kuwa inatokana na usumbufu uliopo hospitalini lakini pia na gharama za matibabu pamoja na umbali wa vituo vya afya na hospitali hivyo kuwalazimu wananchi kununua dawa pasipo kuwa na cheti hicho.

Uchunguzi wa FikraPevu katika maduka hayo unaonyesha kuwa unawapa wahusika utajiri mwingi licha ya kwamba inaweza kuwa chanzo kikubwa cha maangamizi na mauaji duniani.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, dawa hununuliwa baada ya mgonjwa kuthibitishwa na daktari kuwa anaugua ugonjwa flani na kuhitaji dawa kwa haraka lakini wananchi wengi inadaiwa hawana fedha za kutosha zinazowawezesha kuanza kwenda hospitali au zahanati binafsi, kwa ajili ya kuchukua vipimo ndipo anunue dawa. Katika mazingira ya kawaida zoezi hili linaweza kugharimu shilingi 3, 000 hadi 5,000 kabla ya kununuliwa dawa (ili kufikia huduma).

Mara nyingi ndivyo inavyokuwa katika masuala ya kununua dawa na kutafuta vipimo kama katika usemi wa matangazo ya ‘dawa baridi’ unaoelekeza kuwa ‘maumivu yakizidi mwone daktari,’ ila pale unapohitaji tu dawa baridi hakuna haja ya kumwona daktari na tafsiri hiyo hueleweka vibaya.

Ni wazi kuwa mtu akiwa na ugonjwa unaohitaji dawa isiyo ‘baridi’ na hana fedha za kutosha atakachofanya si kupima na kurudi nyumbani kukaa, ila kununua dawa na wala wakati mwingine hamalizi dozi.

Baada ya kupata ‘dozi’ moja, inayotazamiwa kuondoa ugonjwa, akiwa bado hajisikii vizuri au hana hakika ya kupona, hapo kwa jumla atahitaji kupata ushauri wa daktari kwani kwa vyovyote hataendelea kubahatisha na kuendelea kuweka sumu ya dawa mwilini.

Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanasema “Pale mtu anapoona hajapona vizuri ni tofauti na pale ugonjwa unapolipuka akashindwa hata kuketi, kulala au kufanya kazi za kawaida, katika hali hiyo ni lazima apate dawa kwa haraka kutoka katika maduka ya dawa muhimu”.

Maslahi na ugonjwa

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa muuza dawa hawezi kukataa kata kata kuuza chochote bila cheti cha daktari kama wakazi wa Mbezi Mwisho, kwa ujumla wanasema kutokana na umaskini unaowakabili, mfanyabiashara anaweza kugombana na wateja wake na akakosa uhusiano unaohitajiwa katika kuendesha biashara, hivyo atatoa ushauri anaoweza au unaopasa kuhusu matumizi ya dawa na mtumiaji kuendelea na matumizi ya dawa atakazonunua.
 
Licha ya sheria kuhitaji muuza dawa awe pia na utaalamu wa kazi hiyo, kwa vile siyo kila kitu kitategemea cheti cha daktari, katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo ikiwemo katika eneo la Bomba mbli na Kivule mwisho CCM, Makabe Kwa Paulo, Kigogo na Magomeni, yapo maduka hayo na wanaouza maduka hayo wanatuhumiwa kuwa hawajui matumizi wanayouzia wananchi na hivyo kuhatarisha usalama wa watumiaji.

Ukosefu wa kipato/umaskini

Baadhi ya wauza maduka ya dawa wanasema watu wenye kipato cha chini wanashindwa kwenda hospitalini kutokana na kukosa fedha za nauli, vipimo na dawa hivyo kuchagua kutumia pesa kidogo waliyo nayo kununua dawa kwenye duka la dawa na wakati mwingine wakinunua nusu dozi.

Mmoja wa wauza maduka ya dawa anayefanyakazi kwenye duka la Nakiete lililopo Shekilango, anasema wagonjwa wanalalamikia foleni zilizopo hospitalini hasa zile za serikali, mlolongo unakuwa mrefu hadi wagonjwa wanaona ni bora kununua dawa wakameze kuliko kufuata taratibu zinazohitajika.

Kwa ujumla wahudumu wa afya wanasema kumpa mgonjwa dawa bila cheti cha daktari ni kosa lakini inawalazimu kufanya hivyo kutokana na hali ngumu ya maisha.

Mazoea ya maradhi

Wateja wanaoenda kununua dawa hizo akiwemo, Ruth Philipo (27) anasema kutokana na kuumwa mara kwa mara watu wanakuwa wazoefu wa dalili za magonjwa hivyo wanapojisikia hali fulani hufahamu kinachowasumbua na kununua dawa badala ya kwenda hospitali kwa vipimo zaidi.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), inasema dawa muhimu za vijiuasumu au ‘antibayotiki’ zisipotumiwa ipasavyo vinadhuru afya ya mgonjwa kwani ni mahususi kutibu magonjwa mbalimbali hasa yatokanayo na vimelea.

Mara kwa mara Mamlaka hiyo imekuwa ikikemea tabia ya wananchi kukimbilia kununua dawa dukani badala ya kwenda hospitali kwanza, japo watu wanadai hufanya hivyo kwa kisingizio cha kukwepa gharama lakini ni tabia hatarishi.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Celestine Onditi, wanajizatiti kutoa karipio kwa Wafamasia watakaobainika kutoa dawa kwa mgonjwa anapokwenda katika maduka yao kwa lengo la kupatiwa huduma bila ya kuwa na cheti cha daktari kinachoonyesha dawa gani anatakiwa kuzinunua, kwani ni kosa na kwamba anakiuka utaratibu uliowekwa kisheria.

Anawashauri wagonjwa wasinunue vijiuasumu kiholela au hata kutumia cheti cha mtu mwingine kununulia dawa na kuwakanya wagonjwa kugawana dawa na watu wengine.

The post Ununuaji holela wa Dawa wa Wananchi unadidimiza Afya zao appeared first on Fikra Pevu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>