Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Upungufu wa madaktari nchini unachangia kuzorota kwa afya na uchumi

$
0
0

UCHUMI endelevu hauwezi kujengwa na taifa lenye watu wagonjwa kwa kuwa watu hao watatumia muda mwingi kujitibu badala ya kuzalisha mali, hali inayochangia kuzorota kwa uchumi na hivyo ongezeko la umaskini.

Watanzania walio wengi bado wanakabiliwa na adui maradhi. Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa madaktari nchini, ikilinganishwa na idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 45. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye madaktari wachache ikilinganishwa na idadi ya watu wake, ambapo kiuwiano, daktari mmoja huhudumia wagonjwa 30,000. Kwa mujibu wa WHO, daktari mmoja anapaswa kuhudumia wagonjwa 1,000 tu!

Takwimu zilizopo, zinaonyesha kuwa Tanzania inao madaktari wasiozidi 2,000, huku asilimia 32 kati ya hao, wakifanya kazi yao hiyo ktika jiji la Dar es Salaam, asilimia tisa wanafanya kazi katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Kilimanjaro na asilimia 19 wanafanyakazi katika mikoa mingine ya Tanzania.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 40 ya madaktari hao 2,000 hawafanyi kabisa kazi ya utabibu licha ya kuwa na taaluma ya utabibu, na badala yake wanajishughulisha na shughuli nyingine kabisa.

Kutokana na takwimu hizo, ni wazi kwamba asilimia 80 ya Watanzania wanaishi bila kuwa na daktari. Kwa maneno mengine, idadi kubwa ya Watanzania, hasa katika maeneo ya vijijini, wanaougua magonjwa mbalimbali, wanapoteza kwa sababu ya kukosa huduma ya utabibu.

Hali hiyo, kwa kiasi kikubwa imekuwa ikichangia kuzorota kwa hali ya uchumi wa nchi kwa kuwa nguvukazi nyingi, muda mwingi wanakuwa wagonjwa na hivyo kushindwa kufanya kazi na baadhi yao kupoteza maisha. Baadhi ya wadau wa maendeleo katika taifa hili, tayari wamebaini hatari inayolikabili taifa hili kutokana na upungufu huo wa madaktari, katika suala zima la afya na uchumi kwa nchi.

Miongoni mwa wadau hao wa maendeleo waliobaini hatari hiyo, ni Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), hali iliyowalazimu kuanzisha Shahada ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Archbishop James (AJUCO) kilichoko Peramiho, Jimbo Kuu Katoliki la Songea, ambacho ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostine (SAUT) cha Mwanza.

Akizungumza katika mahojiano maalum na FikraPevu, Mkuu wa Chuo Kikuu cha AJUCO), Padri Dk. Faustin Kamugisha, anasema kutokana na changamoto kubwa ya madaktari nchini, hasa katika maeneo ya vijijini, chuo chake hicho, kupitia kampasi yake ya Udaktari Peramiho, imeandaa mfumo maalum wa madaktari watakaohitimu kufanyakazi vijijini ambako kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaokosa huduma ya utabibu.

Kwa mujibu wa Dk. Kamugisha, mfumo huo wa kuwaandaa madaktari kupenda kufanyakazi vijijini, umefanikiwa katika nchi za Canada na Brazil, hali inayotoa matumaini kwamba hata watafanikisha mfumo huo. Anasema fani hiyo ya madaktari ilinzishwa rasmi mwaka 2013, ikiwa na idadi ya wanafunzi wapatao 257. Masomo hayo ya utaktari huchukua muda wa miaka mitano.

???????????????????????????????

Jengo la utawala chuo kikuu kishiriki cha SAUT kampasi ya udaktari Peramiho Songea

Hata hivyo, Dk. Kamugisha anazitaja baadhi ya changamoto kuu inayowakabili wanafunzi wa fani hiyo ya udaktari katika kampasi hiyo ya Peramiho, kwa ni ukosefu wa hosteli.

Hali hiyo, anasema inawalazimu wanafunzi hao kutembea kwa miguu umbali wa kilomita tatu kutoka chuoni hapo hadi katika Kijiji cha Morogoro yaliko makazi yao, kutokana na kutokuwepo kwa usafiri kati ya chuo na kijiji hicho, hali inayoifanya kampasi kampasi hiyo ionekane kama kisiwa.

“Kwa wanafunzi wanaosoma kozi ya udaktari hapa Peramiho, changamoto yao kubwa ni ukosefu wa hosteli kwa kuwa wananchi wanaotuzunguka katika kijiji cha Morogoro, hawana nyumba za kupangisha hali ambayo inawalazimisha wanafunzi kwenda kuishi umbali wa kilometa tatu, na hivyo kulazimika kulipia Sh 3,000 kila siku kwa ajili ya usafari,” anasema Dk. Kamugisha.

Anaitaja changamoto nyingine kwamba ni Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB), akisema mikopo inayotolewa haitoshelezi mahitaji ya wanafunzi hao, huku baadhi ya  wanafunzi wenye vigezo vya kupata mikopo wakiwa hawaipati kabisa licha ya kufuatilia kwa muda mrefu.

“Kwa kweli Bodi ya Mikopo inawakatisha tamaa madaktari wanafunzi katika kampasi yetu hii ya udaktari Peramiho, na hata katika vyuo vikuu vingine vya udaktari, pengine ndiyo maana baadhi yao wanapohitimu wanaamua kuacha taaluma hiyo na kuingia katika taaluma nyingine licha ya kusomeshwa kwa gharama kubwa na kadi ya umma,” anasema.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, Tanzania inatumia kati ya dola za Marekani 40,000 na 60,000 kusomesha daktari mmoja, ambapo inakadiriwa kwamba madaktari wanne kati ya kumi wanaomaliza elimu ya utabibu, wanaacha fani ya utabibu muda mfupi baada ya kuhitimu masomo yao.

Utafiti unaonyesha kuwa katika mikoa ya pembezoni kama vile Kigoma, daktari mmoja anahudumia watu 308,000. Mikoa mingine na idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa ikiwa kwenye mabano ni Mara (167,000), Tabora (132,000), Pwani (32,000), Arusha (22,000) na Dar es Salaam (24,000).

Inaelezwa kwamba upungufu huo wa madaktari nchini, ndio kwa kiasi kikubwa umesababisha nchi hii kushindwa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya Mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Ripoti ya WHO ya mwaka 2006, kuhusu Hali ya Afya Duniani, pamoja na Ripoti ya Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara, katika eneo hilo, kuna wakazi zaidi ya milioni 660, sawa na uwiano wa chini wa madaktari 13 kwa kila watu 100,000.
Ripoti zote mbili hizo, zinaeleza kwamba pamoja na eneo hilo la kusini mwa Jangwa la Sahara kubeba asilimia 24 ya mzigo wa magonjwa yote duniani, lakini kuna asilimia tatu tu ya nguvukazi katika sekta ya afya, huku rasilimali fedha duniani inayowekezwa katika sekta hiyo ikiwa ni asilimia moja tu. 

Inaelezwa na ripoti hizo kwamba idadi ya watu wanaoishi kusini mwa Jangwa la Sahara, ilipaswa kuwa na madaktari zaidi ya 700,000 ili kuziwezesha nchi za eneo hilo kuweza angalau kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) ya mwaka 2015, ambayo pamoja na mambo mengine, yanahimiza kupungua kwa vifo vya watoto wadogo, kuboresha afya ya uzazi, kupambana na VVU/Ukimwi, ugonjwa wa malaria na magonjwa mengineyo.

Kwa mfano, moja ya malengo ya MDGs, ni kupunguza vifo vya watoto wachanga kufikia 32 katika kila watoto 1,000 ifikapo mwaka huu wa 2015, ambapo katika hali halisi lengo hilo limeshindwa kufikiwa kwa kuwa tayari tumeuanza mwaka 2015, huku vifo vya watoto vikiwa ni zaidi ya 100 katika kila watoto 1,000.

Kwa upande wake, katika lengo la kuboresha afya ya uzazi, vifo vinavyotokana na uzazi vinaendelea kuongezeka badala ya kupungua kutokana na upungufu wa madaktari na wauguzi.
Hata hivyo, hatua hiyo ya Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT, Kampasi ya Udaktari Peramiho, kuanzisha mfumo maalum wa kuwaandaa madaktari kufanya kazi vijijini, huenda ikasaidia kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari nchini, hasa katika maeneo ya vijijini.

Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA, vimefanya utafiti ambao umeonyesha kwamba asilimia 39.6 ya madaktari wote nchini, hawafanyi kazi ya kutoa huduma za kitabibu wala za kiutawala katika Sekta ya Afya, bali wanafanya shughuli nyingine tofauti kabisa na fani ya utabibu.

Utafiti huo ulioshirikisha madaktari 2,246 waliohitimu shahada zao nchini, unabainisha kwamba madaktari 890 kati ya 2,246, sawa na asilimia 39.6, hawafanyi kazi ya kitabibu licha ya kusomea fani hiyo, hali inayochangia kuzorotesha zaidi sekta hiyo muhimu kwa uhai wa binadamu na maendeleo ya kiuchumi ya taifa hili.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, ni madaktari 964 tu kati ya 2,246, ndio wanaofanya kazi katika hospitali na vituo vya huduma za afya nchini, wengi wao wakifanya kazi katika majiji na miji mikubwa.

Aidha, kuna madaktari 184 wa kitanzania wanaofanyakazi nje ya nchi baada ya kuyakimbia mazingira ya ufanyaji kazi pamoja na hali ya kipato anachopata daktari nchini.

Hata hivyo, kuna sababu nyingi ambazo zinatajwa na madaktari hao zinazowasukuma wengi wao hao kuacha kufanyakazi walizosomea au wengine kukimbilia maeneo ya mijini au nje ya nchi.

Baadhi ya sababu hizo, ni uhaba wa vitendeakazi, nyumba bora za kuishi, mishahara ambayo hailingani na ugumu wa kazi zao, posho za kujikimu na ukosefu wa masilahi mengine anayostahili kupewa daktari.

Kwa hiyo, kutokana na tafiti na ripoti mbalimbali, afya bora imeelezwa kwamba ndiyo itakayomwezesha kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa lake hili.

Hii ni changamoto nyingine kwa Serikali, watunga sera na wadau wote wa afya katika kuhakikisha kwamba kunakuwepo na vivutio kwa madaktari na watoa huduma za afya kwa ujumla, ili pamoja na mambo mengine, waweze kufanyakazi yao hiyo vizuri na hivyo kupunguza magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Kwa kufanya hivyo, ni wazi taifa litaweza kuwa na nguvukazi yenye afya bora, yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa lao na hivyo kuinua uchumi wa jamii na nchi kwa ujumla.

The post Upungufu wa madaktari nchini unachangia kuzorota kwa afya na uchumi appeared first on Fikra Pevu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>