Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Wauguzi Tanzania Waadhimisha Siku yao huku Wakiyaenzi Matatizo Lukuki

$
0
0

KESHO Mei 12, 2015 ni Siku ya Wauguzi Duniani. Wauguzi ni miongoni mwa kada muhimu kwa jamii yoyote duniani katika kada za utumishi wa umma, umuhimu unaotokana na taaluma yao hiyo kwa wagonjwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya nchini.

Katika kutathimini umuhimu wa Wauguzi kwa jamii yoyote duniani, FikraPevu imeangazia Siku ya Wauaguzi Duniani inayoadhimishwa kila tarehe 12 Mei ya kila mwaka, wauguzi kote duniani hujitathimini wao wenyewe pamoja na kazi yao hiyo, kama kweli wanaendelea kumuenzi muuguzi wa kwanza ulimwenguni, Florence Nightingale.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala haya katika kutathimini siku hiyo na kazi yao hiyo, Ofisa Muuguzi Mkuu wa Kituo cha Afya cha Palestina, Sinza, Dar es Salaam, Alphones Chiwambo, anasema pamoja na mambo mengine siku hiyo ina umuhimu kwao, kwani inawakumbusha kumuenzi muuguzi wa kwanza wa fani hiyo Florence Nightingale.

“Mbali na kumuenzi Florence, siku hii huitumia kujitathimini sisi wenyewe na kazi yetu hii, kuona ni wapi tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Tunatathimini mazingira ya kazi zetu kama yanafanana na jinsi yanavyopaswa kuwa kwa maana ya ubora wa mazingira na ubora wa huduma tunayoitoa kwa jamii,” anasema Chiwambo na kuongeza.

“Sekta hii ya uuguzi inazo changamoto nyingi sana, hasa kwa mataifa yetu haya masikini. Tunakabiliwa na upungufu wa wafanyakazi ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa ambao mMuuguzi mmoja anapaswa kuwahudumia siku.”

Kwa mujibu wa Chiwambo, kwa kawaida Muuguzi mmoja anatakiwa awahudumie wagonjwa wanne hadi watano kwa siku, lakini kutokana na upungufu wa Wauguzi katika hospitali na vituo vya afya nchini, Muuguzi mmoja anaweza kuhudumia wagonjwa kati ya 50 na 100, jambo analosema ni tatizo kwa Muuguzi na Mgonjwa mwenyewe pia.

Wauguzi kuhama fani

Imebainika kwamba lipo wimbi kubwa la watu walioamua kusomea fani ya uuguzi, lakini waliamua kuikimbia kutokana na ukweli kwamba kipato chao hakilingani na majukumu wanayokabiliana nayo wakati wa kuwahudumia wagonjwa. Mourine Ambwene ni mmoja wa Wauguzi katika moja ya vituo vya afya jijini Dar es Salaam anayekiri kwamba kipato cha muuguzi kinachotokana na mshahara wake kwa mwezi hakilingani na majukumu yake, hali inayowafanya baadhi ya wauguzi kuikimbia fani hiyo.

“Inafika mahali mtu anaamua kubadili fani hii badala ya kujiendeleza. Baadhi yetu wanaona ni afadhali wakauze mafuta kwenye vituo vya kuuzia mafuta ya magari, kuliko kuendelea na kazi hii,” anasema Mourine katika mazungumzo yake na FikraPevu katika tathimini yake juu ya Siku ya Wauguzi Duniani.

Kwa mujibu wa Mourine, kitu ambacho hadi sasa Serikali haijakipa kipaumbele ni uwiano unaopaswa kuwepo kati ya idadi ya wauguzi na idadi ya wagonjwa, sambamba na watoa hudumu nyingine za afya, wakiwemo madaktari.

Wahudumu kutoa lugha chafu kwa wagonjwa

Kuhusu malalamiko yanayoelekezwa kwa wahudumu wa afya kutumia lugha ya kuudhi kwa wagonjwa, kiasi cha baadhi ya wagonjwa hao kupoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya wauguzi, imeelezwa kwamba wakati mwingine lugha hizo za maudhi hutokana na sababu nyingi, ikiwemo kuelemewa na kazi.

“Wakati mwingine lugha chafu hutokana na kuelemewa na kazi. Kwa mfano unakuta muuguzi yuko mmoja tu au wako wawili, lakini mbele yao kuna wagonjwa 500 ambao kila mmoja wao anataka ahudumiwe yeye kwanza kutokana na kujiona yeye yuko katika hali mbaya zaidi kuliko wengine… katika mazingira haya mtu hujikuta akitokwa na kauli ambayo kwa kweli haistahili kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya kazi hii, lakini kutokana na kuzidiwa anajikuta ametoa tu kauli,” anasema mmoja wa wauguzi aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na FikraPevu wamewahimiza Wauguzi kote nchini, katika kuadhimisha siku yao hiyo kukumbushana umuhimu wa kutumia lugha za kiungwana kwa wagonjwa, wakitolea mfano wa matukio mbalimbali ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga, hasa kashfa ya hivi karibuni kabisa ya Muuguzi mmoja mkoani Dodoma kumchapa mama mjamzito kiboko wakati akiwa katika hali ya uchungu wa kujifungua na kusababisha mtoto kichanga kufariki kikiwa bado tumboni.

Baadhi ya wanawake wajawazito katika Kituo cha Afya cha Palestina, Sinza, wamekiri kwamba baadhi yao wamekuwa wakikosa huduma kutokana na kukosa fedha za kuwapatia wauguzi kama rushwa ili wawahudumie vizuri.

Kwa mujibu wa wanawake hao, pamoja na Serikali kusema mara kwa mara kwamba huduma ya mama na mtoto inatolewa bure, lakini ukweli ni kwamba hakuna huduma hiyo inayotolewa bure kwenye vituo vya afya.

Baadhi ya wauguzi jijini Tanga, wameelezea changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na hospitali na vituo vingi vya afya kukabiliwa na uhaba wa vifaa, kama vile glovu na maski kwa ajili ya kujikinga mikono na hewa puani wakati wa kumdumia mgonjwa, pamoja gharama kubwa wanayotumia kwenda na kurudi kwenye vituo vya kazi kutokana na uhaba wa nyumba za wauguzi kwenye hospitali na vituo hivyo afya.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mei 5, 2015 alikaririwa na FikraPevu akiwa mkoani Mara akisema Serikali imeanzisha Kurugenzi ya Wauguzi na Wakunga katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoa huduma hao kwenye utoaji wa huduma kwa umma.

Kwa mujibu wa Pinda, ili kukidhi mahitaji ya wauguzi na wakunga nchini, Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na fani hizo.

“Mwaka 2009 tulikuwa na wanafunzi wa Uuguzi na Ukunga 617 wa ngazi ya Cheti na 925 wa ngazi ya Diploma. Kufikia mwaka 2014 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia wanafunzi 2,566 wa Cheti, sawa na ongezeko la asilimia 31.5 na wanafunzi 2,294 wa Diploma, sawa na ongezeko la asilimia 14.1 katika kipindi cha miaka mitano,” anabainisha Waziri Mkuu Pinda.

The post Wauguzi Tanzania Waadhimisha Siku yao huku Wakiyaenzi Matatizo Lukuki appeared first on Fikra Pevu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>