Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Fahamu ukubwa wa Tatizo la Ugonjwa wa Akili na aina ya Ugonjwa huo

$
0
0

WATAALAMU mbalimbali wa magonjwa ya akili, wanauelezea ugonjwa huo kama moja matatizo makubwa yanayoikumba jamii ya Watanzania na dunia kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Wataalamu hao, ugonjwa huo huathiri uwezo wa mtu wa kufikiri, kudhibiti hisia na tabia yake, ikilinganishwa na mtu ambaye hajaathirika kwa ugonjwa huo, hali inayomfanya ashindwe kufurahia uhusiano mzuri na binadamu wenzake, ikiwa ni pamoja na kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha.

Tafiti mbalimbali za magonjwa ya akili, zinabainisha kwamba ugonjwa huo hutofautiana kutegemeana na muda na kadiri ambavyo mtu ameathirika na aina ya ugonjwa wenyewe huo.

Kwa mujibu wa tafiti hizo, ugonjwa huo wa akili unaweza kuwapata watoto na watu wazima wa jinsia zote, matajiri na masikini, na bila kujali kiwango chochote cha elimu. Hata hivyo, mtu mwenye ugonjwa wa akili akipata tiba sahihi anaweza akapona kabisa na kuendelea na maisha yake ya kawaida.

Kwa kutambua umuhimu wa utafiti wa magonjwa mbalimbali nchini, Serikali iliamua kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kwa Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1979, kabla ya kufanyiwa marekebisho mwaka 2002 ili kushughulikia utafiti wa magonjwa mbalimbali ikiwemo yale yasiyo ya kuambukiza ukiwemo ugonjwa huu.

Takwimu kutokana na taarifa ya hivi karibuni kabisa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kwamba watu milioni 26 duniani wanaishi na ugonjwa wa akili, ambao kitaalamu hujulikana kama ’Skizofrenia,’ huku takwimu hizo zikibainisha kuwa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 60 kufikia mwaka 2050.

Hata hivyo, wakati takwimu za WHO zikionyesha ukubwa huo wa tatizo hilo duniani, kwa upande wa Tanzania tafiti zilizopo zinaonyesha kwamba takriban watu 450,000, kati ya idadi yote ya wananchi wa Taifa hili wanaofikia milioni 50, wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ya magonjwa ya akili.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar, tafiti hizo zinabainisha kwamba asilimia 6.8, sawa na takriban watu 70, ya wananchi wote Visiwani hivyo wapatao milioni 1.3 wanakabiliwa na tatizo hilo la magonjwa ya akili kwa mujibu wa utafiti wa wataalamu hao wa mwaka 2012.

Daktari Bingwa na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Frank Masawe, ameiambia FikraPevu kuwa mtu aliyeathiriwa na ugonjwa wa akili, hukosa uwezo wa kufanya kazi ya kumwingizia kipato, kutelekeza familia yake na wakati mwingine kujikuta akiwa mzururaji mitaani.

Shule ya Msingi Tandika, iliyoko katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, ni moja ya shule nchini zinazopokea na kuwafundisha masomo ya darasani watoto wenye matatizo ya magonjwa hayo ya akili.

Baadhi ya walimu wa shule hiyo, wanaohusika na Kitengo Maalumu cha Kuhudumia Watoto hao wenye matatizo ya akili, wameiambia FikraPevu kwamba mara kadhaa wamekuwa wapata shida sana kuwafundisha watoto hao, hasa katika suala zima la mawasiliano ya wanafunzi hao na walimu wao.

Ofisa Muuguzi wa Kituo cha Afya cha Chamazi katika Manispaa hiyo ya Temeke, ambacho ni Tawi la Afya la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Frednand Shangala, anasema ugonjwa huo huweza kutibiwa kwa muda usiotabirika kulingana na ukubwa wa tatizo.

Kwa mujibu wa Dk. Shangala mtu aliyekwishaathirika kwa ugonjwa wa akili, inaweza kumchukua kati ya mwaka mmoja hadi mitatu kuweza kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida ya ubinadamu, hasa kama mgonjwa mwenye na jamii inayomhudumia watazingatia masharti ya Daktari na tiba pia.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili, ambaye pia ni Mtaalamu wa Tiba ya Waathirika wa Dawa za Kulevya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, bila kutaka jina lake litajwe, ameiambia FikraPevu kuwa magonjwa ya akili kwa ujumla wake yameathiri vijana wengi nchini kutokana na kutohudhuria mapema katika Vituo vya Kliniki na Vituo vya Afya kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa mujibu wa Daktari huyo, tatizo hilo linaweza kumtokea mtu yeyote wakati wowote, hasa kwa wale wanaotumia dawa za kulevya, hususan vijana.

Takwimu zaidi zinaonyesha kwamba katika kila watu wazima 50, watu watatu hadi wanne, husumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya akili. Kwa mujibu wa taarifa za WHO, wengi wa watu hao wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali hayo ya akili, wanakuwa ni wale ambao hawapati matibabu mapema kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya mtazamo hasi wa jamii nyingi kuhusiana na magonjwa hayo.

Hata hivyo, ripoti ya hivi karibuni Shirika la Kitaifa la Magonjwa ya Akili la Marekani, inasema kwamba ingawa magonjwa ya akili yana tiba, takriban asilimia 60 ya watu wazima katika Taifa hilo kubwa duniani kiuchumi, pamoja na takriban asilimia 50 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka minane na 15 wameathirika kwa magonjwa hayo ya akili.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles