TABIA ya baadhi ya watu kuwatelekeza wagonjwa Hospitalini mkoani Arusha bado inaendelea kuota mbawa, baada ya mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Robson Nkusa (38), kutekelezwa na ndugu zake kwa zaidi ya miezi nane katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu.
Taarifa za awali zilizoifikia FikraPevu zinasema kuwa mgonjwa huyo alitelekezwa na ndugu zake waliomfikisha katika hospitali hiyo mwaka jana mwezi Disemba, na kuwa walimhudumia kwa siku mbili baada ya hapo hawakuonekana tena ambapo alikuwa anahudumiwa na wahudumu wa hospitali hiyo.
Mmoja wa wahudumu wa hospitali hiyo ameiambia FikraPevu kuwa baada ya kumhoji mgojwa huyo; alisema alianza kutengwa na ndugu zake baada ya kuugua ugonjwa huo.
Amesema hadi sasa mgonjwa huyo hawezi kuongea vizuri kutokana na hali aliyo nayo, na kuwa amejitambulisha kuwa anatoka jijini Dar es Salaam katika eneo la Mbezi Africana.
Kwa upande wake Nkusa, amewataka ndugu zake waende kumsaidia akiwemo Baba yake, Joseph Robson Nkusa, kwa kuwa hali yake ya afya sio nzuri, kutokana na ugonjwa alionao.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kuambukiza katika hospitali ya wilaya hiyo, Dkt. Taitus Mmasi, amesema mgonjwa huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa na hali mbaya lakini baada ya kupatiwa matibabu afya yake ilianza kuboreka kwa kiwango kidogo nakuwaomba ndugu zake waweze kufika hospitalini hapo na kumchukua.
Tafiti zinaonyesha kuwa kuwa ugongwa wa kifua kikuu unaosababishwa na vimelea vidogo vidogo aina ya bakteria viitwavyo Microbacteria tuberculosis, ambapo huenezwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu ambaye anaugua na hajaanza matibabu kwa kupiga chafya, kukohoa na kutema makohozi ovyo zinatajwa kuwa ni sababu za kuweza kuambukiza watu wengine.
Dalili za kifua kikuu ni pamoja na kukohoa kwa wiki mbili au zaidi mfululizo, homa za mara kwa mara kwa wiki mbili au zaidi, kutokwa na jasho jingi hasa nyakati za usiku, kukohoa makohozi yenye damu, kupungua uzito zaidi ya kilo 3 ndani ya wiki 4 au kukonda pamoja na kukosa hamu ya kula.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa takribani wastani wa watu 176 huugua kifua kikuu kila siku nchini, na wastani wa watu 12 hufariki dunia kila siku kutokana na ugonjwa huo.