Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Madhara ya kusafisha meno kwa kutumia Zebaki

$
0
0

AFYA ya kinywa ni sehemu muhimu katika ustawi wa afya ya mtu mmoja mmoja na jamii. Watanzania wengi wana magonjwa na matatizo mbalimbali katika vinywa vyao. Magonjwa ya kinywa yaliyo mengi yanaweza kuzuilika kwa kuzingatia taratibu za afya.

Magonjwa ya meno yameongezeka kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha na vyakula ambapo magonjwa ya Saratani, UKIMWI na maji yenye madini ya florini yanaathiri afya ya kinywa ya wananchi walio wengi.

Pia matumizi ya kemikali ya zebaki yanatajwa kushika kasi katika jamii ya Kitanzania, licha ya madhara ya kiafya yatokanayo na kemikali hizo kuwa makubwa.

Moja ya eneo ambalo limekuwa likitumia kemikali hizo ni katika Vituo vya kutolea huduma za afya ambapo kemikali hizo zimekuwa zikitumika kuzibia meno.

Bado matumizi ya zebaki kwenye kuziba meno yapo na yanaendelea kuwepo na kumfanya mgonjwa na wahudumu wa afya kwenye idara za kuziba meno kuathiriwa na kemikali hizo kutokana na kufanya kazi kwenye vyumba maalumu muda mwingi au muda wote.

Mmoja wa wataalamu wa afya katika Hospitali mojawapo Jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameidokeza FikraPevu kwamba wagonjwa wengi wanaathiriwa na kemikali hizo wanapokwenda kutibiwa Hospitalini lakini wakishatoka katika chumba cha matibabu ya kinywa ya meno kemikali hizo zinaendelea kuwaathiri kwenye mwili kupitia chakula wanachokula.

Ameeleza kuwa sababu kubwa ya kuathiriwa kwa njia hiyo ni baada ya pamoja na sehemu ya mabaki ya zebaki yanayoenda na chakula na wakati mwingine yanatoka kama mvuke na hivyo mwanadamu akiendelea kuhema anaendelea kuvuta sumu hiyo mwilini.

“Kutokana na hali ilivyo sasa ni vyema madaktari kuwaambia wagonjwa kwamba wakiziba meno kwa kutumia zebaki madhara yake ni yapi, na inakaa muda gani na ina faida na hasara gani” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Imeelezwa kwamba changamoto kubwa ya kutumia njia mbadala ni ile hali ya kutumia kitu kipya na madaktari wengi hawajaanza kuzizoea na ziko chache. Ingawa ingekuwa vizuri madaktari wengi wakapatiwa kozi ya kurejea matumizi ya teknolojia mpya ili kuondokana na matumizi ya zebaki katika hospitali za hapa nchini.

Kwa mujibu wa wataalamu hao wa afya, athari kubwa hutokea baada ya zebaki kuingia kwenye mwili wa binadamu na kujiunga na ngozi za mifumo ya fahamu, ngozi ya kujikinga na magonjwa, hivyo mishipa ya ndani inabaki wazi na mifumo ya fahamu inaharibika.

Wameeleza kuwa matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa zimeonyesha athari kwenye mfumo wa uzazi kutokana na ngozi ya zile chembechembe hai zinakuwa zimetoka kutokana na kuathiriwa na zebaki.

Daktari wa Afya ya Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Muhimbili ya Dar es Salaam, Dk. Rachel Mhavile, amesema taarifa sahihi juu ya tatizo hilo hazijawafikia wagonjwa na baadhi ya madaktari hazijawafikia na kwamba wengine wanazo.

Ameeleza kwamba wengi wa madaktari nchini hutumia njia mbadala wa michanganyiko ya madini ya fedha na zebaki kuzibia meno njia ambayo ni teknolojia ya zamani iliyotumika kufundishia madaktari wengi wakiwa vyuoni.

“Kubadilika na kutumia teknolojia mpya kunahitaji muda na mafunzo hivyo kinachohitajika kwa sasa ni wagonjwa wenyewe wapewe taarifa sahihi na madaktari” alieleza Dk. Rachel.

Mtu mzima anaweza kuathiriwa na kemikali hizo kwa kupoteza kumbukumbu na uwezo wa kuona unaweza kupungua na hauwezi kurejea katika hali ya kawaida.

Dalili zinazoonyesha kuwa mwanadamu ameathiriwa na hali hiyo ni pamoja na kupoteza kumbukumbu, hasira za haraka sana, kinga ya mwili kupungua na pia kutetemeka.

Hali hiyo ikishavuka kiwango baadhi ya watu hawawezi kupona, pia nywele vinakuwa nyembamba zaidi na kuwa laini kutokana, uwezo wa kuongea unakuwa mdogo na mwili kuathiriwa zaidi.

Ikiwa mtu ameathiriwa na zebaki kwa kiwango cha juu, zipo dawa anazopewa ili kuondoa dawa hizo lakini haziwezi kurudisha hali ya awali.

Uchunguzi unaonyesha kuwa ni watu wengi ambao hawana desturi ya kumwona daktari wa meno walau mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Wengi wetu huhangaika na foleni za kumwona daktari wa meno pale tu tunaposumbuliwa na maumivu ama ya jino ama kidonda kinywani ama kwa sababu ya hali zinginezo zinazotulazimisha kumwona daktari wa meno.

Kusubiri mpaka tusukumwe na maumivu ya meno/kidonda kinywani ama ajali yoyote kunatunyima fursa bora zaidi ya kuchunguzwa afya ya kinywa na meno na kusafishwa meno ili kuepusha madhara ya magonjwa ya kinywa na meno kabla hayajatokea ama kukomaa.

Aidha, kupiga mswaki kwa ufanisi walau mara mbili kwa siku huondoa ukoko unaogandamana kinywani na kusababisha kuoza kwa meno. Ukoko huu ni ute laini unaoganda kwenye sehemu mbalimbali za jino/meno huku ukiwa na mamilioni ya vimelea vya magonjwa (bakteria).

Matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss) kila siku husaidia kuondosha ukoko maeneo ambako mswaki haufiki, vile vile kuondosha ukoko huu kunasaidia kujikinga na magonjwa ya fizi.

Takriban asilimia 85 ya watu wenye harufu mbaya kinywani huwa na magonjwa ya kinywa na meno, ikiwa harufu mbaya kinywani inasababishwa na magonjwa kinywani, dawa za kusafisha kinywa (mouthwash) haziwezi kuondoa tatizo zaidi ya kulifunika kwa muda tu.

The post Madhara ya kusafisha meno kwa kutumia Zebaki appeared first on Fikra Pevu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>