WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepiga marufuku usafirishaji wa chumvi isiyokuwa na madini joto unaofanywa na wafanyabiashara kwa visingizio vya kupeleka kwenye viwanda vya utengenezaji wa ngozi.
Taarifa zinaeleza kwamba baadhi ya maeneo ya migodi nchini inayochimba madini hayo ni pamoja na mgodi wa Gendabi ambao unaochimbwa katika msimu wa kiangazi, kutoka Ziwa Gendabi katika Wilayani Hanang’ mkoani Manyara.
Mkurugenzi Mkuu wa Huduma na Lishe wa Wizara hiyo, Dr. Visent Assey, amesema licha ya wizara hiyo kutoa elimu ya madini joto ili kuepusha madhara 104 yanayotajwa kutokana na matumizi ya kibinadamu ya chumvi hiyo bado tatizo hilo ni kubwa nchini.
Hata hivyo, amesema ametoa marufuku hiyo baada ya wachimbaji wengi nchini kubainika kwamba hawazingatii matumizi ya masuala waliofundishwa ya madini joto kabla yake wameanza kuuza chumvi yao hadi katika baadhi ya nchi jirani na Tanzania.
Amebainisha kwamba uchunguzi wao umeonyesha kwamba chumvi hiyo nyingi inaonekana inaenda kutumiwa mitaani na watu wengine na imeenda hadi nchini Burundi ambapo mamlaka nchini humo wameripoti kwao kuhusiana na tatizo hilo.
Kufuatia hali hiyo amekaririwa na FikraPevu akisema chumvi yeyote itakayotoka ndani ya migodi hiyo nchini, inatakiwa kuwekewa madini joto na haitajalisha kama inaenda kwenye viwanda au sehemu yeyote.
Taarifa zinasema lipo tatizo kubwa la baadhi ya wafanyabiashara kukwepesha bidhaa zao kutoingia mikononi mwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wafanyakazi wa aina hiyo wapo wengi nchini, baadhi wanatoa bidhaa kutoka nje kwa bei poa.
Ofisa Mdhibiti Ubora TBS, Deusdedith Paschal, amesema viwanda vitakavyobainika kuendesha biashara bila kuongeza madini joto ndani ya chumvi kama ilivyokuwa kwa miezi ya kuanzia Oktoba, Novemba na Desemba mwaka jana, Shirika hilo liliteketeza kiasi cha tani 1.5 ya chumvi iliyozalishwa na kampuni ya Sea Salt ya Dar es Salaam, kwa kukosa madini joto na kuzalishwa katika mazingira duni.
“Ukaidi unaofanywa na viwanda vya aina hii unaweza kuangamiza watumiaji wengi, na taarifa za athari za kukosekana kwa madini husika ni kubwa, lakini wafanyabiashara wamekuwa wakikaidi maelekezo, wanachojali zaidi ni maslahi ya kibiashara kuliko kuangalia afya za wananchi” alieleza Paschal
Mjumbe wa Bodi ya Taifa na Uthibiti wa Madini Joto, Dk. Luis Mmbando, amesisitiza wananchi kuzingatia sheria bila shuruti na kuwa viwanda ambavyo vitakiuka maagizo ya kusafrisha madini joto bila kufuata taratibu watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
“Tunapaswa sisi kama Taifa tuboreshe chumvi yetu, kiafya na kibiashara, na katika kufanya hivyo kuna suala la kuweka madini joto ambalo ni suala la kisheria, sio kubembelezana” alieleza Dk. Luis.
Madini joto ni moja ya vitu muhimu sana kwenye mwili wa binadamu na iwapo kutakuwa na ukosefu wa madini hayo mtu anaweza akapata madhara kwa kupata magonjwa na madhara.
Wanawake wajawazito wakikosa madini hayo inaweza ikawa sababu kubwa kwa watoto ambao watazaliwa wakiwa na mtindio wa ubongo pamoja na kuzaliwa wakiwa na tezi la shingo.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), upungufu wa madini joto huathiri ujauzito, huathiri ukuaji wa kiakili na hupunguza ufanisi wa kazi.
Upungufu mkubwa wa wekundu wa damu unaotokana na upungufu wa madini ya chuma, unaongeza uwezekano wa kupata matatizo makubwa ya kiafya kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa na kifo kwa wajawazito.
Upungufu wa vitamini A hudhoofisha kinga ya mwili na kusababisha maambukizi, matatizo mbalimbali ya macho ikiwa ni pamoja na upofu, na kuongezeka kwa magonjwa ya watoto na vifo. Upungufu wa zinki huathiri kwa kiwango kikubwa ukuaji wa mwili, viungo vya uzazi na ubongo.
Hali ya lishe ya mama ina uhusiano wa karibu na afya ya uzazi, uhusiano kati ya magonjwa na lishe kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC),watoto wanaopata lishe duni wana kinga hafifu ya mwili, hali ambayo huongeza uwezekano wa kupata maambukizi, maradhi na kifo.
Maradhi huufanya mwili kushindwa kufyonza vyema virutubishi, kwani umetaboli huathirika pia kukosa hamu ya kula, hali ambayo husababisha ulaji duni wa chakula na ufyonzwaji duni wa virutubishi mwilini.
The post Wizara yapiga marufuku Usafirishaji wa Chumvi isiyokuwa na Madini joto appeared first on Fikra Pevu.