SERIKALI imeonyesha jitihada kubwa katika kupambana na ugonjwa wa malaria ambapo maambukizi yanatajwa kwamba yameshuka kutoka asilimia 18 kwa mwaka 2007/2008 hadi asilimia 10 mwaka 2011/2012.
Lakini pamoja na kupungua kwa maambukizi hayo, takwimu zinaonyesha ugonjwa huo bado ni tatizo kubwa katika vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mjini ambapo maambukizi ya maeneo ya vijijini ni asilimia 10.7 na mjini ni aslimia 3.4
Kupungua kwa maambukizi hayo kunatajwa kwamba ni kutokana na mwamko ambao wananchi wameupata wa kutumia vyandarua vyenye dawa ili kujikinga na mbu waenezao malaria, mwamko ukionekana kuwa mkubwa zaidi mijini kuliko vijijini.
Licha ya serikali kujitahidi kupeleka vyandarua vijijini, lakini baadhi ya wananchi wameshindwa kuvitumia kwa kazi hiyo, ambapo wengine walifikia hatua ya kuvitumia kuvulia dagaa pamoja na kukinga bustani zao zisiharibiwe na kuku pamoja na wadudu wengine.
Kiwango cha maambukizi nchini Tanzania kinatofautiana kati ya mkoa na mkoa, ambapo mikoa ambayo inayoongoza kwa maambukizi hayo ni Kagera (41.1%), Lindi (35.5%), Mtwara (36.6%), Mwanza (31.4%), Mara (30.3%).
Mikoa ambayo maambukizi ya malaria ni kidogo ni Manyara (1%), Kilimanjaro (1%) na Dar-es-Salaam (1.2%). Visiwani Zanzibar, maambukizi ya malaria ni kwa asilimia 0.8.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu, akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani Aprili 25, 2016 alikaririwa akisema kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha maambukizi hayo yanapungua hadi kufikia asilimia 5 mwaka huu 2016 na asilimia moja ifikapo mwaka 2020.
Hilo litawezekana tu ikiwa kila mtu anawajibika kwa nafasi yake kushiriki katika kupambana na vita dhidi ya malaria.
Wadau ambao wapo mstari wa mbele katika mapambano ya malaria ni pamoja na Mfuko wa Dunia wa kushughulikia ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kushughulikia Malaria (PMI), Shirika la Misaada la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la UNITAID,Taasisi zisizo za Kiserikali, Sekta Binafsi kupitia Mpango wa malaria Safe na Taasisi za Utafiti za NIMRI na Ifakara.
Katika kupambana na adui maradhi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Joseph Magufuli, alitoa mwongozo wa Serikali yake kupitia hotuba yake ya kufungua rasmi Bunge jipya la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,mjini Dodoma Novemba 20, 2015 ambapo alibainisha dhamira ya dhati katika masuala ya afya.
“Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini linakwenda sambamba na kuwa na wananchi wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli huu na mahitaji ya huduma bora za wananchi wetu Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya,” alisema.
Dhamira hiyo ya Serikali ni kuimarisha huduma za afya sehemu ambapo huduma hizo zipo na kuanzisha pale ambapo hazipo ikiwa na lengo la kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali ya Rufaa.
Ni dhahiri nia ya Serikali ya kuboresha huduma za afya nchini itasaidia kuongeza utaalamu katika sekta ya afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi, kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizopo nchini.
Malaria ni ugonjwa hatari ambao, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takriban watu bilioni 3.2, ambayo ni nusu ya idadi ya watu duniani, wako hatarini kuambukizwa.
Kwa mwaka 2015 pekee, karibu wagonjwa milioni 200 waliripotiwa ulimwenguni kote huku viisababisha vifo vya watu zaidi ya 400,000, wengi wao wakiwa katika Bara la Afrika, hususan kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kulikuwa na asilimia 89 ya wagonjwa wote na vifo asilimia 91.
WHO imesema lengo la kutokomeza ugonjwa huo katika nchi 35 ifikapo mwaka 2030 linaweza kufanikiwa licha ya kuwa ni la juu.
Mwaka 2015 Waziri Mkuu (mstaafu) Mizengo Pinda, aliahidi kwamba serikali ilikuwa imedhamiria kutokomeza ugonjwa wa malaria na kwamba inajenga kiwanda cha kisasa cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi wa mbu wanaosababisha malaria.
Kiwanda hicho cha viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria kimejengwa eneo la TAMCO, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
“Malaria ni ugonjwa hatari na unaongoza kwa kusababisha vifo hapa nchini. Watu karibu milioni mbili wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa huu. Tukianza kutengeneza hizi dawa zitasaidia sana kupunguza tatizo hili na kuokoa maisha ya watoto na wanawake wajawazito ambao ndiyo waathirika wakubwa,” alisema.
Akielezea utendaji kazi wa dawa hizo, Waziri Mkuu alisema: “Dawa hizi zinapotumiwa kwenye madimbwi, viluwiluwi ni lazima watakufa katika muda wa saa 24 … na mle kwenye dimbwi dawa ile inabakia ikifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja. Hii ina maana wakizaliwa viluwiluwi wengine pia wanakufa bila hata kuweka dawa nyingine.”
Kiwanda hicho ambacho kimetoa ajira za moja kwa moja 186, kilizinduliwa Juni 25, 2015 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kiwanda hicho kilichojengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya LABIOFAM SA ya Cuba, kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita za dawa ya Biolarvicides kwa mwaka.
Malaria huonekana zaidi katika Ukanda wa Tropiki. Ugonjwa huu wa malaria uligunduliwa mwaka 1880 na Charles Louis Alphonse Laveran, katika Hospitali ya Jeshi ya Constatine, Algeria, baada ya kuona vimelea vya plasmodium, kutoka kwa mgonjwa aliyefariki kwa ugonjwa huo.
Malaria ni kati ya magonjwa ya maambukizi ambao husababishwa na vimelea vya plasmodium, ambavyo humfikia binadamu kupitia kung’atwa na mmbu jike wa aina ya anopheles.
Hivi karibuni watafiti wamebaini kuwepo kwa vijidudu vya malaria ambavyo haviteketezwi na dawa za malaria zilizopo, ambavyo vimepatikana nchini Cambodia na viko tofauti na vijidudu vingine duniani. Imeelezwa kuwa vijidudu hivyo vimekuwa sugu hata kwa dawa bora dunini ya artmisinin.
Pamoja na changamoto hiyo, lakini bado jitihada zinafanyika duniani kote kukabiliana na maradhi hayo hatari, yakiathiri zaidi watoto na akinamama wajawazito.