KESHO Alhamisi, Mei 12, 2016 Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anatarajiwa kusoma Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Bajeti hiyo, ambayo itajadiliwa kwa siku mbili, inasubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi, hususan walio vijijini, ili kuona kama Serikali ya Rais John Magufuli imezingatia maeneo mengi yenye changamoto kwenye sekta hiyo kama alivyoahidi wakati wa kampeni.
Ingawa mpaka sasa juhudi kubwa zimefanywa na serikali hiyo, lakini changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika zahanati za vituo vya afya vijijini bado kubwa.
Mapema mwaka huu wa 2016, Waziri Ummy Mwalimu alisema kwamba Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya kwa mwaka 2016/17 unahitaji Shs. trilioni 21 ili kutekeleza maeneo nane ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hata hivyo, kati ya maeneo nane yaliyolengwa, hakuna hata moja linalohusisha suala la uzazi wa mpango pamoja na upatikanaji wa elimu na huduma za uzazi huo, ambao ni muhimili mkubwa katika suala la kuangalia idadi ya watu nchini.
Maeneo yaliyotajwa katikia Mpango Mkakati huo ni mafunzo kwa wafanyakazi, utoaji wa kinga ya afya pamoja na elimu juu ya magonjwa mbalimbali, mgawanyo wa rasilimali fedha katika vituo vya afya ili kupata dawa na vifaa tiba, kuhamasisha uchangiaji wa huduma za afya, kuongeza watumishi kila pembe, na kadhalika.
Idadi ya watu nchini Tanzania inaongezeka kwa asilimia 2.7 kila mwaka, hali ambayo inatishia hata uchumi wa taifa kutokana na ukweli kwamba, karibu nusu ya Watanzania kwa sasa ni wategemezi na hawazilishi, hivyo mapato ya taifa ni madogo kulinganisha na mahitaji.
Suala la uzazi wa mpango, ambalo kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990 lilipata msukumo (pengine kutokana na kuwepo na fedha za msaada) kupita mpango wa Nyota ya Kijani, hivi sasa linaonekana kudorora kwani elimu haitolewi kwa kiasi cha kutosha hasa vijijini na huduma zenyewe hazipo hata kwa wale wachache ambao wanaelewa umuhimu wa kupanga uzazi.
Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 inaeleza kwamba, utekelezaji wake unakwenda sambamba na miongozo iliyomo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025 pamoja na kutambua shabaha zilizowekwa katika Malengo ya Maendeleo ya Milenia, ambayo miongoni mwa mambo mengine, yanasisitiza dhima ya soko katika kuamua mgao na matumizi ya rasilimali.
Sera hiyo inatamka kwamba, wanandoa na watu wote wana haki ya msingi ya kuamua, kwa uhuru na kwa kuwajibika, idadi na mpangilio wa watoto wao na vilevile kupata taarifa, elimu na njia za kufanya hivyo.
Kwa mukhtadha huo, idadi ya watu ni kigezo muhimu katika kupanga uchumi na maendeleo, kwani ukiwa na watu wengi wanaozalisha kuliko tegemezi maana yake uchumi utaimarika na huduma nyingine muhimu zitapatikana.
Inafahamika wazi kwamba vijenzi vikuu vya ukuaji wa idadi ya watu katika nchi yoyote ni uzazi, vifo na uhamaji, hivyo, nchini Tanzania, uzazi na vifo ni vipengele muhimu sana vinavyoathiri ukuaji wa idadi ya watu katika ngazi ya Taifa.
Kiwango cha uzazi nchini Tanzania kimepungua kidogo kutoka watoto 5.8 kwa kila mwanamke wakati wa kipindi cha umri wa kuzaa mnamo mwaka 1996 hadi watoto 5.7 kwa kila mwanamke mnamo mwaka 2004 (Utafiti wa Hali ya Afya na Uzazi Tanzania mwaka 2004-05).
Lakini mnamo 2004, Tanzania Bara ilirekodi wastani wa watoto 6.5 kwa kila mwanamke wa maeneo ya vijijini na 3.5 kwa maeneo ya mijini.
Tofauti za wastani huo zenye kuhusiana na viwango vya elimu zinaachana sana. Kiwango cha uzazi kwa wanawake wasio na elimu kilikuwa 6.9, wenye elimu ya msingi ni 5.6 na wenye kiwango cha elimu ya sekondari na elimu ya juu kilikuwa 3.2. Kwa upande wa Zanzibar, kiwango cha jumla cha uzazi kilishuka kutoka 6.9 mnamo 1996 hadi 5.3 mnamo 2004 (Utafiti wa Hali ya Afya na Uzazi Tanzania mwaka 2004-05).
Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu inakiri kwamba, kiwango cha juu cha uzazi nchini Tanzania ni matokeo ya sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuolewa mapema na kwa karibu wanawake wote.
“Umri wa wastani wa ndoa ya kwanza kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 – 49 ni miaka 18; na kufikia umri wa miaka 20, zaidi ya asilimia 69 wanakuwa wameolewa walau mara moja (Uchunguzi wa Hali ya Uzazi na Afya ya Mtoto mwaka 1999). Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inataja umri wa chini kabisa kisheria wa ndoa kuwa ni miaka 15 kwa wanawake na miaka 18 kwa wanaume.
“Kutokuwepo kanuni madhubuti za uzazi miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuzaa; na kiwango cha kuenea kwa njia za kisasa za kuzuia uzazi kinakadiriwa kuwa asilimia 16 miongoni mwa wanawake wenye umri wa miaka 15 – 49 (Uchunguzi wa Hali ya Uzazi na Afya ya Mtoto mwaka 1999),” inabainisha Sera hiyo.
Hata hivyo, inafahamika – na hata serikali inakiri – kwamba mambo yanayochangia ukuaji huo wa kasi wa idadi ya watu ni pamoja na jamii kuona kwamba thamani ya mtoto kama chanzo cha nguvukazi majumbani na mashambani na usalama wa kiuchumi na kijamii wa umri mkubwa kwa wazazi.
Lakini pia jamii nyingi kupendelea kupata mtoto wa kiume. Akikosa katika uzazi mmoja mwanamume anataka mkewe aendelee kubeba mimba tena na tena kwa matarajio ya kupata mtoto wa kiume, hatua ambayo inafanya kuwa na watoto wengi, kwani huyo wa kiume anaweza asipatikane.
Aidha, sababu nyingine ni hadhi ya chini ya kijamii na kielimu ya wanawake katika jamii inayowazuia kufanya maamuzi kuhusu uzazi na matumizi ya huduma za uzazi wa mpango na pia tofauti kubwa za umri baina ya wanandoa zinazokwamisha mawasiliano kuhusu masuala yanayohusiana na afya ya uzazi.
Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu inakiri wazi wazi kwamba kuna uhusiano wa karibu kati ya ukuaji wa idadi ya watu na maendeleo, kwani katika muda mfupi, athari za ukuaji wa idadi ya watu zinaweza kuonekana kuwa ndogo lakini zinaanzisha mchakato limbikizi, ambao athari yake hasi kwenye sura mbalimbali za maendeleo zinaweza zikawa muhimu sana katika muda wa kati na mrefu.
“Hii ni kwa sababu vigeu vya idadi ya watu vinaathiri maendeleo na ustawi wa mtu mmoja mmoja, familia, jumuiya katika ngazi ndogo na katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa zima katika ngazi ya jumla. Athari na miitikio ya shinikizo la idadi ya watu zinahusiana katika ngazi zote,” inasema Sera hiyo.
Kwa ujumla, ukuaji wa kasi wa idadi ya watu katika mazingira ya ukuaji mdogo kiuchumi huelekea kuongeza matumizi, ukiwa unaondoa rasilimali kutoka kwenye akiba ya vitegauchumi vya uzalishaji na hivyo kuelekea kupunguza kasi ya ukuaji wa uzalishaji wa taifa kupitia uundwaji mdogo wa mtaji.
Matatizo yanayosababishwa na ukuaji wa kasi wa idadi ya watu yana athari kubwa na yenye kuonekana katika bajeti za umma kwa ajili ya afya, elimu na sekta nyingine za maendeleo ya rasilimali watu, ambapo hata bajeti ya Afya inayotarajiwa kusomwa kesho inaweza kuwa na upungufu katika maeneo mengi, hususan suala la uzazi wa mpango.
Wataalamu wa masuala ya idadi ya watu wanaeleza kwamba, idadi ya watu na maendeleo yanaathiriana, ambapo athari inaweza ikawa chanya au hasi kutegemea vipengele na hali nyingine.
Kwa upande wa Tanzania, vipengele vilivyotajwa awali vya demografia vinaingiliana na kusababisha matatizo kwani ukuaji haraka wa idadi ya vijana unahitaji ongezeko la matumizi yaliyolengwa kwenye huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na makazi.
Aidha, ukuaji wa haraka wa nguvukazi unahitaji uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya rasilimali watu, na vilevile mikakati ya maendeleo inayohakikisha fursa za uundaji wa ajira katika siku zijazo.
Ieleweke pia kwamba, ukuaji wa haraka wa idadi ya watu katika muktadha wa kuondoa umaskini hupunguza uwezekano wa kufikia ukuaji endelevu wa uchumi.
Matumizi ya mbinu za kisasa za uzazi wa mpango bado ni duni (asilimia 27 tu ya wanawake ndio wanaotumia njia za kisasa).
Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu inaeleza kwamba, madhumuni yake ni kukuza mwamko wa umma kuhusu afya ya ngono na uzazi; na haki kwa vijana, wanaume na wanawake na kukuza na kupanua ubora wa huduma za afya ya uzazi; na ushauri kwa vijana, wanaume na wanawake ikiwa ni pamoja na kukuza na kupanua upeo wa utetezi wa afya ya uzazi na progamu za Taarifa, Elimu na Mawasiliano.
Kama bajeti ya kutosha itakuwepo, inawezekana mipango hiyo ya serikali itafanikiwa, vinginevyo hata kama tutakuwa na sera nzuri, lakini tusipokuwa na rasilimali fedha, bado changamoto hizi zitazidi kuathiri taifa kwani idadi ya watu inaongezeka kwa kasi.