TAASISI mbalimbali zinazohusika na kukabiliana na magonjwa ya milipuko nchini Tanzania zikiwamo hospitali kubwa za serikali nchini zinatajwa kutojizatiti katika kukabiliana na ugonjwa hatari wa ebola uliotikisa dunia hivi sasa, athari kubwa ikiwa nchi za Afrika Magharibi, FikraPevu imebaini.
Ni taasisi chache sana ambazo zimeweka utaratibu na vitendea kazi katika kujihami na ugonjwa huo hatari, ikiwamo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kwa kushirikiana na wadau wengine wa viwanja hivyo ikiwamo mashirika ya ndege, uhamiaji na maofisa wa afya.
Hata hivyo, hali bado si salama sana katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani kwa njia ya barabara na hospitali za umma zikiwamo hospitali za Rufaa katika mikoa ambayo FikraPevu iliweza kufuatilia.
Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu katika baadhi ya hospitali kubwa nchini zikiwemo za jijini Dar es Salaam na mikoa ya Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Lindi, Tanga, Kigoma na Mbeya umeonyesha kuwa hakuna utaratibu wala vifaa vinavyowekwa kwenye hospitali hizo kwa watu wote wanaoingia katika hospitali hizo kupimwa ili kujua kama yupo mmoja wapo anadalili za ugonjwa huo.
Hali hiyo inatokea pamoja na kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutoa mafunzo kwa Waganga na Wauguzi kwa jinsi ya kumhudumia mgonjwa aliyeathiriwa na virusi hivyo, lakini hakuna vifaa na maandalizi ya kutosha katika maeneo yao ya kazi.
FikraPevu imeshuhudia baadhi ya wagonjwa wakiingia katika baadhi ya hospitali hizo bila kukaguliwa kama wameathiriwa na ugonjwa huo au la na imebainika pia ya kuwa hakuna juhudi za kutosha katika maeneo ya mipakani kwa watu wanaoingia na kutoka na kuingia kwa njia ya barabara.
Baadhi ya watendaji wa hospitali za serikali na binafsi wamesema serikali haijajipanga kikamilifu kupambana na ugonjwa huo na kwamba inatakiwa kutambua jinsi Tanzania ilivyo na uhusiano wa karibu na nchi ambazo tayari zimewahi kuathiriwa na homa hiyo ikiwemo Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuwa bila kudhibitiwa kwa hali hiyo ipo hatari kwa ugonjwa huo kuingia nchini.
“Huu ugonjwa kwa sasa umekuja kwa kasi mno na biashara zinazofanyika zinaweza kuwa chanzo cha kuueneza na hofu yetu ni wale wanaotoka nje ya nchi kuingia nchi je kwanini Serikali haiweki juhudi zake katika kupambana na hili kama nchi za wenzetu? sisi tumezubaa sana kwa maana hata wanaoingia kupitia viwanja vya ndege wameanza tu juzi kusema kuwa wanawakagua lakini ukweli ni kuwa ukiingia nchini sio sisi Madaktari tu tutakao kufa ila watu tutakufa kama kuku wanavyougua ugonjwa ugonjwa wa mdondo,” anasema mmoja wa watumishi wa sekta ya afya nchini.
Mganga Mfawidhi katika moja ya hospitali zilizopo jijini Mwanza amesema, “Tusianze kulalamika kusema mipaka iko mingi nchini lakini je kwanini tulivyokuwa tunategemea kuwa serikali ingejitahidi kuchukua tahadhari zaidi ya hapa kama nchi za wenzetu?.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam, baadhi ya wakazi w ajiji hilo akiwemo Onesmo Julius, amesema fedha zilizopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa zinatakiwa kutumika kwa ajili ya kushuhulikia janga la ugonjwa wa ebola ili zitumike kuliokoa Taifa.
“Nimeingia hapo Mwananyamala mda huu hakuna hata vifaa tiba vya kumtambua mtu mwenye hivo virusi na hili naweza kusema kuwa ni uzembe kwa maana mgonjwa mmoja tu akiingia hapo ndani anaweza kuambukiza watu wengi sana kwa hiyo mimi naomba serikali kwa kweli iongeze ujudi za huu ugonjwa kwamaana wanajinadi na maeneo yaliyotengwa kuhudumia wagonjw alakini mbona watu watakufa wengi sana kama kwenye maeneo yenye mikusanyiko hayatarekebishwa,” anasema.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Ebola ni ugonjwa wa hatari unaosababishwa na virusi vijulikanavyo kwa lugha ya kitaalamu Ebola Virus, ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kitaalamu kama ‘homa za virusi’ na husambazwa na damu kutoka kwa mtu mwenye virusi hivyo kwenda kwa ambaye hana ugonjwa ambapo hali ya maambuziki huitwa Viral Haemorrhagic Fevers.
Moja ya Hospitali binafsi iliyopo jijini Dar es Salaam pekee (hadi sasa) inayokagua watu wa aina wote wanaoingia Hospitalini hapo
Hata hivyo dalili muhimu za ugonjwa huo ni mgonjwa kuwa na homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili kama ikiwemo puani, njia ya haja kubwa na ndogo, masikioni, mdomoni, machoni au anaweza kupasuka ngozi. Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika kwa kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, machozi na majimaji mengine yanayotoka katika mwili wa mtu aliyeathirika au mtu mwenye dalili za ugonjwa huu wa Ebola.
Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni lilitangaza ugonjwa huo kuwa janga la kidunia kufuatia kuua watu wengi katika nchi za Guinea ulipoanzia na kutapakaa katika nchi jirani za Sierra Leone, Liberia na nchi nyingine duniani.
Shirika la Afya Duniani lililazimika kutoa kibali kwa matumizi ya dawa ya majaribio ya kutibu wagonjwa walioathirika na virusi wa Ebola zinaweza kutumika ingawa bado hazijafanyiwa majaribio rasmi.
WHO ilisema kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo ilikuwa ni sawa kuruhusu kutumika kwa dawa hizo.nTamko hilo lilitanguliwa na kikao cha wataalam waliokutana kuzungumzia suala hilo nchini Uswisi.
Hoja hiyo ilikuja baada ya serikali ya Liberia kusema ilikuwa tayari kutumia dawa za majaribio kutoka kwa kampuni ya Zmapp kwa msaada wa serikali ya Marekani
Mpaka sasa dawa hiyo hazijafanyiwa majaribio kwa binadamu isipokuwa kwa nyani na sokwe.
Ugonjwa wa Ebola umeathiri nchi kadhaa za Afrika Magharibi na watu wanaokadiliwa kufikia 1000 wamekufa kutokana na ugonjwa huo.