AFYA za wananchi wa Kata za Igoma, Buhongwa, Busonge, Idedemia na Bukumbi, Katika Wilaya za Ilemela, Nyamagana na Misungwi mkoani Mwanza, zipo hatarini kuathirika kutokana na kutumia maji yanayodaiwa kuwa na kemikali ya sumu pamoja na walaji wa mboga za majani zinazozalishwa pembezoni mwa mifereji inayotiririsha maji hayo na kuleta hofu ya watumiaji kupatwa na magonjwa ya homa ya tumbo.
Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu mkoani humo umebaini kuwa maji hayo hutiririshwa na baadhi ya viwanda mkoani humo na kuelekezwa ndani ya Bonde la Mto Nyashishi, ambao humwaga maji hayo katika Ziwa Victoria.
Wakazi wanaozungukwa na maeneo hayo wanasema viwanda sita vilivyopo eneo la Nyakato na Igoma, vinatiririsha maji hayo yenye kemikali ndani ya Bonde hilo, ambalo ni tegemeo kwa wananchi wa kata hizo kwa shughuli za uchumi na kijamii.
Wameishangaa serikali kuzembea katika suala hilo kwa muda wa miezi mitano hadi sasa, ambapo inadaiwa kuwa Ng’ombe wanaochungwa ndani ya bonde hilo wameanza kudhoofika na Nyasi zikiwa zimekauka, jambo ambalo limeanza kuwatia hofu watu wanaotumia maji ya bonde la mto huo.
“Sisi tuna hofu ya kula nyama zinazochinjwa huko machinjioni, kwani wenye hivi viwanda wakijua tu sisi ndio tumetoa taarifa wanaweza hata wakatudhuru ingawa tumejaribu kuwashirikisha viongozi wa maeneo tunayoishi lakini wametuambia watawaona wenye viwanda ili kuwaeleza hofu yetu”
Hatari ya magonjwa ya tumbo walaji mboga za majini
Imeripotiwa kuwa walaji wa mboga za majani mkoani humo wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya kansa ya utumbo na homa ya matumbo kutokana na mazingira hatari ya uoteshaji, na baadhi ya wakulima kutumia madawa pasipo kufuata utaratibu za afya kwa lengo la kuzalisha mboga hizo kwa wingi.
Mmoja wa wananchi wa mkoa huo aliyejitambulisha kama Juliana Oppi, amesema mifereji ya maji machafu ambayo hutiririka kutoka kwenye viwanda hivyo na kuingia kwenye makazi ya watu huku pembezoni mwa mifereji hiyo shuguli za kilimo cha mbogamboga zikiendelea kufanyika na kuwa maji haya ndiyo hutumika zaidi katika umwagiliaji.
Pamoja na wataalamu wa afya kushauri ulaji wa mboga za majani kama mojawapo ya kiungo muhimu katika kukamilisha mlo kamili wa mwili wa binadamu mazingira yanayotumika katika uandaaji na utunzaji wa bustani kwa baadhi ya sehemu za jiji hilo imeelezwa kuwa bado ni hatari.
Hata hivyo, wakazi hao wamelalamikia hatua ya baadhi ya wakulima kutumia maji kutoka vyanzo visivyo salama kwa kulima kilimo cha kisasa huku wakihusishwa na matumizi holela ya dawa za kutibu zao hilo kwa lengo ya kujinufaisha kifedha
FikraPevu inaendelea na juhudi za kuwatafuta viongozi wa maeneo husika ili kutolea ufafanuzi suala hilo.