AGIZO la Serikali kutaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ishirikiane na Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) na vyombo vingine vya dola kuwasaka wanaouza dawa za Serikali katika maduka yao ili wachukuliwe hatua za kisheria, limedaiwa kupuuzwa kutokana na serikali kutoa matamko yasiyotekelezeka.
FikraPevu imebaini kuwa moja ya maagizo yaliyotolewa na viongozi wa kitaifa akiwemo, Rais Jakaya Kikwete, mwaka 2013 akiitaka Wizara hiyo kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa kuwatafuta wahudumu wa sekta hiyo wanaokuwa chanzo cha wagonjwa kukosa dawa katika hospitali za serikali hususani vijijini, halijatekelezwa.
Rais Kikwete, aliahidi kwamba serikali yake itahakikisha hospitali za umma zinapata dawa pamoja na madaktari wa kutosha ili kuimarisha kiwango cha afya nchini lakini bado tatizo hilo linazidi kuota makucha huku takwimu zikionyesha kuwa zaidi ya asilimia 20 ya dawa za serikali huchukuliwa kinyemela na watumishi wasio waaminifu na kisha kuuzwa kwenye maduka na kliniki zao binafsi.
MSD na mikakati ya kudhibiti wizi wa dawa nchini
Miezi mitatu baada ya agizo la Rais Kikwete, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kama chombo chenye jukumu la kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa, ilianzisha mkakati mpya wa kuziwekea alama dawa na vifaa tiba ili vinapokutwa mahali pasipohusika iwe rahisi kuzibaini, kwa kuweka nembo ya ‘GOT’ kwenye dawa zote ya umma, bado imeripotiwa zoezi hilo halijazaa matunda.
Mkurugenzi wa Shughuli za Kanda na Huduma kwa Wateja kutoka MSD, Edward Terry, mwezi Aprili, 2014 alisema wataendelea na mpango wa kuweka alama hizo pamoja na kubandika orodha ya dawa na vifaa tiba vinavyokabidhiwa vituoni huku tatizo hilo likionekana kutozaa matunda.
Halmashauri za takiwa kufanya ukaguzi
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, leo Jumatatu Julai 7, 2014 ameziangiza halmashauri za wilaya nchini kufanya ukaguzi katika baadhi ya maduka ya dawa yaliyopo katika maeneo yao ili kujua maduka yanayomilikiwa na baadhi ya wataalamu wa afya.
Mwanri, ameijulisha FikraPevu kwamba agizo hilo amelitoa akiwa mkoani Tanga, baada ya wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea mkoani humo kulalamikia hatua ya baadhi ya Madaktari ambao wamefungua maduka binafsi ya dawa za matumizi ya binadamu, na kuwaagiza wagonjwa sehemu ya kununulia dawa hizo kwa kisingizio cha kukosekana kwa dawa hizo hospitalini.
Amesema kuwa zipo tetesi kuwa baadhi ya wataalamu hao huiba dawa kutoka katika Hospitali za Serikali na kwenda kuuza dawa hizo katika maduka ya watu binafsi na kuisababishia serikali hasara kubwa.
Amesema amefanya ziara ya ukaguzi wa madirisha ya wazee wenye umri huo pamoja na kufahamu huduma ya dawa zinazotolewa kwa makundi hayo, kufuatia malalamiko yanayozidi kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini kuwa pamoja na sera ya taifa kuruhusu wazee wa umri huo kupata tiba bure bado wamekuwa wakinyanyasika pindi wanapohitaji huduma katika sekta ya afya nchini.
Wananchi waishangaa serikali kutoa kauli sizisotekelezeka
Baadhi ya wananchi wamelalamikia baadhi ya wamiliki wa maduka ya dawa ambao wanahusika kufanya biashara hiyo, na kuwa wamekuwa wakitumia ujanja wa kujipatia dawa hizo kutoka katika hosipitali za serikali na kuzipeleka kwenye maduka yao huku wagonjwa wakibakia bila dawa na wahudumu wengine wa afya kuwaelekeza wagonjw asehemu za kupata dawa hizo.
Kwa upande wake, Florah Chausa, mkazi wa Korogwe mkoani Tanga alisema “Serikali imekuwa ikishuhudia uhaba mkubwa wa dawa uliopo BohariKuu ya Madawa,
“Kimsingi Serikali inatumia mabilioni ya fedha kuhakikisha MSD inakuwa na dawa za kutosha ambazo zitasambazwa katika hospitali ili ziweze kuwasaidia Watanzania lakini hazidhibitiwi bado wanaendelea kupiga kelele bila kuwachukulia hatua kali,” alisema.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapaswa kufanya uchunguzi katika maduka binafsi kubaini mafisadi wa dawa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.
Watumishi wa serikali kukamatwa
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, pamoja na msako huo kutangazwa watumishi wa idara hiyo waliokamatwa kuhusika na uuzaji wa dawa hizo ni wachache mno kulingana na ukubwa wa tukio hilo.