Jitihada za asasi zisizo za kiserikali nchini likiwemo Shirika lisilo la Kiserikali la SIKIKA kutaka kuishawishi serikali kulipa madeni inayodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) la zaidi ya shilingi bilioni 90, hadi sasa bado taarifa za ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika sehemu mbalimbali nchini zimeripotiwa ambapo imebainika kuwa bado serikali haijachukua hatua madhubuti ili kukabiliana na tatizo hilo, jambo ambalo linaweza kuchangia wagonjwa kuteseka zaidi na hata kusababisha vifo.
Limesema serikali haijataka kufanyia kazi maagizo ya Bunge kwa wakati, pindi wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walivyoanza kupigia kelele ukosefu wa dawa hizo pamoja na Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii.
Taarifa ya SIKIKA kwa vyombo vya habari, leo Novemba 27, 2017 (FikraPevu imepata nakala), kitendo cha serikali kupuuza maagizo yalitotolewa na bunge kimefanya deni hilo kuongezeka huku mikakati ya kulilipa deni hilo ikiwa haieleweki kulingana na uzito wake.
“SIKIKA ilitegemea serikali ingeangalia janga hili kwa makini zaidi na kulipa mara moja deni lote (Tshs bilioni 90), linalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) badala yake ni Tshs. bilioni 20 tu zilizotolewa mpaka sasa na nyingine Tsh bilioni 11 zilizoahidiwa kutolewa ndani ya mwezi mmoja sasa kutokana na unyeti wa suala hili ambalo linagusa maisha ya wananchi, tungependa kuona serikali ikilipa fedha zote inayodaiwa na MSD ili kuiwezesha kufanya kazi ipasavyo” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Chanzo cha deni
Kadhalika, imesema tatizo la uhaba wa dawa na vifaa tiba linaloendelea kwa sasa linasababishwa na kukua kwa deni na hivyo kuifanya MSD kushindwa kusambaza dawa na vifaa tiba kwa vituo vya kutolea huduma vyenye madeni. Hata hivyo, imeeleza kuwa tatizo la upungufu wa dawa na vifaa tiba nchini ni sugu na linapaswa kutatuliwa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa sababu kuu zinazosababisha uhaba wa dawa nchini ni bajeti ndogo inayotengwa, ucheleweshaji katika kutoa fedha zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa pamoja na takwimu zisizo sahihi juu ya mahitaji halisi ya dawa nchini na hivyo ni vyema Serikali ikatatua pia vyanzo vingine vinavyosababisha uhaba wa dawa nchini pamoja na kulipa deni kamili.
Hospitali ya Sinza Palestina
Katika hospitali ya Sinza Palestina, walikuwa wakidaiwa na MSD shilingi milioni 93 ambapo Oktoba mwaka huu, walipokea fedha kutoka Mfuko wa Afya wa pamoja (Health Basket Fund) na kuagiza MSD dawa na vifaa tiba vyenye gharama ya shilingi milioni 100. Pia walipokea mzigo wenye thamani ya shilingi milioni 25 tu kwa sababu MSD walikata deni wanalowadai la shilingi milioni 75.
“Hii imelazimisha hospitali hiyo kutumia dawa walizopokea kwa ajili ya dharura tu, kwa sababu dawa hizo haziwezi kukidhi mahitaji yao ambapo wanahudumia takribani wagonjwa 600 kwa siku, hivyo kusababisha uhaba wa dawa katika hospitali hiyo, kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na vyombo vya habari. Hali hii katika Hospitali ya Sinza Palestina inafanana na hospitali nyingi nchini”.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sikika wameitaka serikali iongeze bajeti ya dawa kufikia angalau nusu ya mahitaji ya nchi, ambayo ni Tsh. bilioni 250 kwa mwaka. Pia wameshauri kuwa Wizara ya Fedha na Uchumi (MoFEA) itoe gawio la fedha zote zinazotengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba (mwanzo wa mwaka) kwa mkupuo mmoja kwenda kwenye akaunti za vituo MSD.
Hata hivyo, wameitaka MSD kuboreshe utendaji wa kazi, uwazi na uwajibikaji kwa sababu hizo ndizo nguzo bora katika mfumo wa ununuzi na usambazaji wa dawa.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa katika siku za hivi karibuni FikraPevu ilibaini kuwepo na Taasisi nyeti za tiba nchini zikiwemo Hospitali za Wilaya za Kiteto, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Mpwapwa kuwa hazina dawa muhimu za kutosha baada ya Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kusitisha zoezi la kusambaza dawa katika hospitali hizo kutokana na deni la zaidi ya shilingi bilioni 90 inazoidai serikali.