Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Kitengo cha Mazoezi ya Viungo Hospitali ya Muhimbili kipo katika hali mbaya

$
0
0

HALI ya Kitengo cha Mazoezi ya Viungo katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili ya jijini Dar es Salaam si shwari na husababisha mapungufu makubwa ya mahitahi ya wagonjwa wa viungo ambao hutibiwa hapo. Uchakavu wa majengo wa muda mrefu, ukosefu wa taa, feni na vyoo visafi ni baadhi ya mahitaji ya msingi ambayo yanabidi kuboreshwa katika kitengo cha taasisi hiyo.

FikraPevu imeshuhudia hospitalini hiyo kuwa hali mbaya ya vyoo vya wodi katika kitengo hicho na wodi nyingine mbalimbali kwenye hospitali hiyo. Vyoo hivyo nyakati za usiku haviingiliki kutokana na kukosa taa huku baadhi ya ndugu wa wagonjwa wakilalamika kuwa wanateseka kutafuta namna ya kuwasaidia wagonjwa wao kupata huduma safi ya choo. Pia, imeelezwa kwamba kwa muda mrefu hakuna maji katika wodi zenye vyoo, hali inayosababisha baadhi ya ndugu na jamaa kununua maji kutoka nje ya hospitali na kuwapelekea wagonjwa wao kwa ajili ya kujisaidia haja kubwa na ndogo.

“Kuna choo kimoja tu hicho ndio kibovu kuliko vyote, pia wagonjwa wa kike na kiume wanaogopa kujisaidia kwani mapazia yamechakaa na yanawafanya wagonjwa waonekane na mpita njia wakati wakijisaidia” alidokeza mmoja wa wagonjwa akiongea na FikraPevu.

Choo kibaya

Choo mojawapo kikiwa kinaonyesha bomba ambalo limefungwa, wala halitoi maji

Pia moja ya tatizo lingine lililopo ni eneo lile lililotengwa kwa ajili ya huduma za watoto ambalo hivi sasa linafafanishwa na eneo la kuhifadhia mizigo (Store) kwani eneo ni finyu na hakuna mfumo wa kutoa na kuingiza hewa ya kutosha.

Tatizo lingine lililolalamikiwa kuwa na hali mbaya katika kitengo hicho cha watu wanaofanya mazoezi ya viungo ndani ya hospital hiyo ni kutokuwa na hazina mashuka ya kutandika kwenye vitanda kama ilivyo kwenye hospitali nyingine na kuwalazimu wagonjwa kutandika kanga zao kwenye vitanda vya wodi hizo kwa ajili ya kujisitiri wakati wakisubira au kupata huduma na wengine kukosa kabisa cha kujifunika.

Siling bodi ya choo. 2

Mwonekano wa juu wa moja ya choo hospitalini hapo

Licha ya kubainika kua kitengo hicho kinaingiza fedha nyingi zinazoweza kukarabati jengo hilo ambalo tangu enzi za Mkoloni halijawahi kufanyiwa ukarabati wowote, taarifa zisizo rasmi zinaonyesha kumekuwepo na mvutano baina ya uongozi wa taasisi hiyo na watumishi wake baada ya kushauri maeneo yenye mapungufu hayo yarekebishwe kwa muda mrefu bila utekelezaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu kuzorota kwa huduma katika hospitali hiyo, mmoja wa madaktari (hakutaka jina lake litajwe) amesema serikali iliamua kutoshughulikia madai ya madaktari ambayo mengi yalikuwa yakitaka kuboreshwa kwa huduma hospitalini hapo kwasababu zisizowekwa wazi.

Kufuatia hali hiyo madaktari waliamua kukaa kimya na kufanya kazi katika mazingira hayo yanayowaathiri zaidi wagonjwa wasiokuwa na hali nzuri kiuchumi hali iliyohusishwa na taarifa potofu kuwa mgomo wa madaktari mwaka 2011 serikali ilipindisha ukweli kuwahadaa wananchi kwamba madaktari walikuwa wakitaka nyongeza ya mishahara.

Msemaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Algaeshi, hakupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo.

Wakati haya yanatokea siku chache zilizopita taasisi nyeti za tiba nchini ikiwemo Hospitali hiyo na nyingine nyingi zilibainika kuwa hazina dawa muhimu za kutosha baada ya Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kusitisha zoezi la kusambaza dawa katika hospitali hizo kutokana na deni la zaidi ya shilingi bilioni 90 inazoidai serikali.

Kitanda Wodi

Muonekano wa Kitanda katika wodi ya Kitengo cha Mazoezi ya Viungo

Mapema wiki hii wabunge kadhaa wakiendelea na vikao vya bunge mjini Dodoma walisimama na kuibana Serikali wakitaka suala hilo litolewe maelezo, huku baadhi wakipinga hatua ya vikao vya Bunge kuendelea kama fedha hizo hazitalipwa.

Hatua ambayo iliifanya serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu ambaye anakaimu pia nafasi ya kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Profesa Mark Mwandosya, kuahidi kuwa tamko la serikali kuhusu hali ya vifaa tiba na dawa nchini litatolewa wiki hii.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>