DAKTARI feki amekamatwa katika Hospitali ya mkoa wa Morogoro baada ya kufanya kazi kwa muda wa wiki tatu akihudumia wagonjwa katika Hospitali hiyo na kufanya wagonjwa waliokuwa wanatibiwa hospitalini hapo kuingiwa na hofu ya kupata madhara ya kiafya.
Mashuhuda watukio hilo wameiambia FikraPevu kuwa Daktari huyo amegundulika akiwa amevalia koti la kidaktari ambapo imedaiwa alikuwa akihudumia katika hospitali hiyo kwa takribani wiki tatu.
“Alikuwepo hapa kwa muda mrefu lakini alikuwa hajagundulika ila baada ya Mhudumu mmoja hapo hospitalini kumtaka amsaidie moja ya kazi ambayo hatukujua ni kazi gani alisema amegundua kuwa ni Daktari feki ndipo na yeye akatoa taarifa kwa kiongozi wake” Waliidokeza FikraPevu.
Aidha, baadhi ya wananchi mkoani humo wamesema wameshtushwa na taarifa hizo na kuwa serikali inatakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika hospitali zinazotoa huduma zote ikiwemo ya afya kwa wananchi ili kuepuka kupata madhara yanayoweza kutokea.
Baadhi ya wauguzi walisema hawajui alikuwa akihudumia wagonjwa wa magonjwa gani tangu alipoanza kufanya kazi hiyo, na pia hakuwa na kitambulisho kinachomuonyesha kuwa ni mtumishi wa hospitali hiyo. Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Leonard Paul, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa bado Jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano.
Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa wa Morogoro Dakt. Rita Lyamuya, hakupatikana mara moja kuzungumzia tukio hilo, tutawaletea taarifa zaidi kadri tutakapozipokea.
Tukio hilo linatokea siku Nane tangu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini kuonya watu wanaojiita madaktari na maprofesa bila ya kuwa na sifa hizo na kudai kuwa wana uwezo wa kutibu magonjwa yasiyotibika ukiwemo ugonjwa wa Ukimwi na kisukari.
Taarifa ya Wizara hiyo ilitolewa Julai 4, 2014 jijini Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa serikali Dakt. Donnan Mmbando, na kufafanua kuwa wenye haki ya kujiita hivyo kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia tiba asili na tiba mbadala nchini Tanzania, ni wale tu wenye sifa zinazotambulika na Mamlaka mbalimbali za serikali.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, matukio ya wauguzi wasio na taaluma ‘feki’ umezidi kuzikumba Hospitali mbalimbali nchini, likiwemo tukio la hivi karibuni lililotokea katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ambapo mmoja wa wauguzi wake alimuuzia dawa 'feki' mgonjwa ambaye alielezwa kuendelea kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo hadi Mei, 2014.