WATAFITI wa Magonjwa ya Binadamu na Mifugo nchini, wametoa tahadhari kwa wananchi kuepuka kunywa maziwa yasiyochemshwa na nyama isiyoiva vizuri kufuatia kuibuka kwa ugonjwa wa unaosababishwa na matumizi ya vyakula hivyo.
Akizungumza na FkraPevu leo Julai 17, 2014 baada ya kumalizika kwa kikao cha kutathmini tatizo hilo mkoani Tanga, Mtaalamu wa magonjwa ya Binadamu na Wanyama nchini, Dkt Gabriel Shirima, amesema dalili za ugonjwa huo unaojulikana kwa jina la ‘Kutupa Mimba’ ni kichwa kuuma, homa kali, na mgongo pamoja na viungo vyote vya mwili na kuwa katika mtizamo wa haraka zinafanana na dalili za ugonjwa wa malaria ambao umekuwa ukisababisha vifo kutokana na kukosa tiba ya haraka.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Magonjwa ya Wanyama kwenda kwa Binadamu Dkt Andrew Chota, amesema utafiti walioufanya hivi karibuni mkoani humo, umeonyesha kuwa wilaya za Lushoto na Korogwe ndizo zinazoongoza kwa ugonjwa huo na hivyo wameunda timu ya kwenda katika wilaya hizo kufanya kampeni za kutokomeza ugonjwa huo.
Aidha, wamewataka wananchi kuchukua tahadhari hiyo na kuwataka Madaktari watakao kwenda kukagua ng'ombe hao, kuwa na vifaa maalum vya kuzuia damu ya Ng'ombe kutoingia katika mwili wa binadamu.
Hata hivyo kumekuwepo na mjadala kuhusu ugonjwa huo ulioripotiwa katika mtandao wa kijamii wa JamiiForums ambapo wachangia mada wameitaka serikali kufanya utafiti katika maeneo mengine nchini kuhusiana na ugonjwa huo.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, wataalam wa afya wanasema watu wanaopendelea kula nyama ya mifugo tofauti, wanatakiwa kuwa makini na aina ya nyama unayokula kwa kuzingatia uandaaji unakuwa mzuri pamoja na kuhakikisha kuwa imeiva ili kuepuka kupata magonjwa yatokanayo na ulaji wa nyama hizo.
Kadhalika, Wataalam wa Afya wamesema nusu ya watu duniani, wapo katika hatari ya kuambukizwa magonjwa yatokanayo na wadudu, wanapoishi katika makazi ya pamoja na mifugo katika maeneo mbalimbali duniani.