Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Utafiti: Ushuzi unaotokana na Kujamba, una Uwezo wa Kutibu Ugonjwa wa Saratani

$
0
0

UTOAJI wa ushuzi, katika mazingira yoyote yale, umekuwa na matokeo tofauti katika jamii yetu ya Kitanzania. Watu wanaotoa ushuzi au kujamba mbele za watu, huonekana mbele ya watu hao kama watu wasio kuwa na adabu, hivyo kudhalauliwa wakati mwingine.

Hata hivyo, taarifa za kitafiti za kisayansi, zinaweka wazi kwamba kutoa ushuzi au kujamba, ni afya. Kwa mujibu wa wataalam hao, kila mnyama kwa maana ya viumbe wote walio katika kundi la wanyama kisayansi, binadamu akiwemo, wakati fulani hujihisi tumbo kujaa gesi nyingi (kuvimbiwa), hivyo njia pekee ya ufumbuzi wake katika kuondokana na shida hiyo, ni kupunguza gesi hiyo kwa njia ya kujamba.

Kwa mujibu wa taarifa hizo za kitafiti, katika idadi yote ya viumbe hai vinavyojamba, mchwa anaongoza kuliko wanyama wengine wote. Aidha, mchwa huyo huyo anadaiwa kuchangia kupanda kwa joto la dunia (global warming) kwa kiwango kikubwa kwa kuwa huzalisha gesi ya methane kwa wingi kupitia njia hiyo ya kujamba. Kwa kawaida, gesi ya methane na hydrogen inaweza kusababisha moto.

Tafiti mbalimbali ambazo FikraPevu inazo, zimebainisha kwamba mwanadamu akijamba mfulululizo kwa kipindi cha miaka sita mfululizo akiwa ndani ya chumba kisichoruhusu hewa au gesi kutoka nje, anaweza kuzalisha nishati ya kutosha kutengeneza bomu mfano wa bomu la atomiki.

Kujamba ni tendo la kuachia hewa/gesi iliyobanwa ndani ya mwili (tumbo) kwa kutumia njia ya haja kubwa. Wakati binadamu anapokula au kunywa, hewa huingia tumboni kiasi kwamba hewa nyingine husababishwa na gesi kuingia kwenye utumbo ikitokea kwenye damu, huku baadhi ya gesi ikizalishwa na baadhi ya kemikali katika utumbo au bakteria.

Mtu anaweza kujamba akiwa katika fahamu zake zote au usingizini. Aidha, mtu anaweza kujamba pia hata baada ya kukata roho na kufariki dunia, ndani ya saa zake tatu za mwanzo. Hali hiyo ya maiti kutoa ushuzi au kujamba, husababishwa na hali ya kusinyaa kwa misuli baada ya kukata roho.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Exeter cha Uingereza, umebaini kuwa harufu ya ushuzi inaweza kutibu saratani/kansa na magonjwa mengine hatari. Kama ushuzi una nguvu za uponyaji huenda ukatumika kwa mambo mengine mengi, ingawa utafiti huu haukusema moja kwa moja.

Kwa zaidi ya wiki sasa, vyombo vingi vya habari vya Uingereza vimekuwa vikipambwa na vichwa vya habari vinavyohusiana na ushuzi kutibu hali zote za magonjwa hatari, ingawa si jambo lenye uhakika sana.

Kwa kawaida ushuzi unakuwa na asilimia 59 ya gesi ya nitrojeni, asilimia 21 ya gesi ya hydrogen, asilimia tisa ya gesi ya Carbon dioxide, asilimia saba ya methane na asilimia nne ni oksijeni.

Kwa hiyo, asilimia moja tu ya ushuzi inaweza kuwa Hydrogen Sulphide na Mercaptans, ambayo ndiyo ina Sulphur ndani yake. Kwa kawaida, Sulphur ndiyo inayofanya ushuzi utoe harufu mbaya. Ushuzi husafiri kwa mwendo wa futi 10 kwa sekunde na huchukua sekunde kati ya 10 na 15 hadi kuanza kusikika hatufu ya ushuzi baada ya mtu kujamba.

"Ingawa gesi ya Hydrogen sulphide inajulikana kuwa na harufu mbaya na hupatikana katika mayai yaliyooza pamoja na harufu ya mtu kujamba, hutengenezwa mwilini na inawezekana kuwa tiba kwa magonjwa fulani," anasema Dk. Mark Wood, Profesa wa Chuo Kikuu hicho cha Exeter.

Utafiti huo unadai kuwa kampaundi ziitwazo AP39, husababisha uzalishaji wa Hydrogen sulphide kwa wingi katika seli/chembe hai za mwili. Na kiwango kidogo tu cha Hydrogen sulphide, kimethibitika kulinda Mitochondria (Sehemu ya seli/chembehai inayotoa nguvu kwa seli yote na ambayo mara nyingi hushambuliwa na magonjwa).

Ndiyo kusema basi kwamba kama Hydrogen sulphide ina uwezo wa kulinda Mitochondria dhidi ya uharibifu wowote wa mwili wa binadamu, ni wazi kwamba Hydrogen sulphide hiyo inayokuwa kwenye ushuzi inaweza pia kuzuia kuendelea kwa magonjwa mengi yanayo shambulia mwili, mfano wa kansa.

Baadhi ya vipingamizi viliibuka na kuzuia furaha iliyoanza kusambaa. Kiukweli, utafiti ulikuwa na utata mkubwa na haukuhusisha moja kwa moja ushuzi, zaidi ya Hydrogen sulphide, gesi ambayo pia hutengenezwa na mwili ukiwa katika utendaji wake wa kawaida na kuupa ushuzi harufu mbaya.

Baadhi ya wanasayansi walidai sayansi inayohusu uvumbuzi huu ilibidi kuandikwa upya. Kwa kuwa inaaminika na wengi kwamba uvutaji wa mkusanyiko mkubwa wa Hydrogen sulphide ni hatari sana kwa afya.

Pia inaaminika kwamba kuvuta ndani ushuzi ina maana ya  sehemu ya gesi huingia kwenye mapafu na kutolewa nje tena bila kufyonzwa au kufikishwa kwenye seli/chembe hai iliyokumbwa na ugonjwa.

Wanasayansi wengi walishangazwa ni kwanini kitu hiki hakikuonekana kabla ya sasa, ikizingatiwa kwamba kwa kawaida, mtu anatoa ushuzi karibu mara 14 kwa siku, ingawa wengine huweza kutoa zaidi ya idadi hiyo, hasa wanapokuwa katika hali ya ugonjwa.

Kwa kuongezea, utafiti ulidhihirisha kwamba ni mara chache sana watu huzuiia upepo kwa watu walio wagonjwa mahututi kwa kuogopa kutokewa na kitu kibaya zaidi.

Wakati tamaduni nyingi za Kiafrika, ikiwemo Tanzania, zikichukulia tendo la kutoa ushuzi au  kujamba kuwa jambo lisilo la kistaarabu, kuna baadhi ya tamaduni hawaoni haya au aibu kujamba hadharani, huku wakifurahi tendo hilo. Kwa mfano watu wa kabila la Yanomami huko Amerika Kusini, kwao husalimiana kwa kujamba. Inasemekana hata nchini China mtu anaweza akapata ajira ya kudumu kwa kazi ya kunusa ushuzi.

Katika Roma ya zamani, Mfalme Claudius akihofia kwamba kujizuia kujamba kunaweza kuwa hatari kiafya, alipitisha sheria kwamba ni ruhusa kujamba kwenye ‘banquets’ zake, kwa maana ya hafla zinazofanyika kwenye makazi ya Mfalme au Ikulu.
Ndani ya jamii, baadhi ya watu huogopa kujamba hasa wakiwa na wenzi wao, wengine wakifikia hatua ya kushindwa kusinzia wakilala na wenzi wao wakiogopa kujamba kwa sauti wakiwa usingizini.Madaktari hawajakubaliana moja kwa moja kama kujizuia kujamba ni hatari kiafya au la.

Baadhi ya wataalamu wanafikiri kujamba ni sehemu muhimu katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula, hivyo kujizuia kujamba kunaweza kusababisha tumbo kujaa gesi na pia inaweza kusababisha kikundu.

Kikundu, ni ugonjwa wa kuvimba kwa mshipa wa damu ulio ndani ya njia ya haja kubwa na mara nyingi hutokeza nje na kumsababishia mtu maumivu makali. Hali hii, inadaiwa kusababishwa na mgandamizo mkubwa wa gesi, ambao kitaalamu hujulikana kama Hemorrhoids.

The post Utafiti: Ushuzi unaotokana na Kujamba, una Uwezo wa Kutibu Ugonjwa wa Saratani appeared first on Fikra Pevu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles