Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Dalili za Ugonjwa wa Uvimbe wa Tezi za Uzazi kwa Wanawake na Tiba yake (2)

$
0
0

Katika makala iliyopita ambayo ni (sehemu ya kwanza) tulijadili namna wanawake wengi wanavyoteseka na tatizo la kutoshika ujauzito bila ya kujua sababu yake pia ni nini. Moja ya sababu ya kutoshika ujauzito, ni ugonjwa wa Sisti au Nziba unaopatikana kwenye Ovari za uzazi (Ovarian Cyst). Katika makala haya ya sehemu ya pili tutaangazia tena dalili na viashiria vya kwanza kabisa vya ugonjwa huu wa Sisti/Nziba.

Dalili na viashiria vya kwanza kabisa vya ugonjwa wa Sisti/Nziba kwenye Tezi za Uzazi za Mwanamke ni maumivu makali ambayo hayana mwanzo maalum na yanayochoma, ambapo maumivu hayo yanaweza yakawa yanakuja na kupotea au yakawepo moja kwa moja.

Lakini pia, mwanamke anaweza kupata usumbufu na kutojisikia vizuri kwenye maeneo ya chini ya kitovu, kwenye nyonga, uke, kwenye mapaja na mgongoni upande wa chini kiunoni.

Dalili nyingine ni maumivu ya muda mrefu kwenye nyonga wakati mwanamke anapokuwa kwenye siku zake, maumivu ambayo huweza kuhisiwa sehemu ya kiunoni. Kwa kawaida mumivu haya yanaweza kuanza muda mfupi tu baada ya kuanza hedhi, wakati wa hedhi au mwisho wa hedhi.

Maumivu ya nyonga baada ya kufanya kazi ngumu, mazoezi au baada ya kujamiiana. Kuhisi kichefuchefu, kutapika na kutokwa na matone ya damu ukeni.

Ugumba na kuhisi uchovu, mabadiliko ya haja ndogo, yaani kukojoa mara kwa mara, kujikojolea au kushindwa kutoa mkojo wote kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kupata haja ndogo.

Mabadiliko ya haja kubwa, kwa maana ya kupata haja kubwa kwa shida sana kutokana na presha kwenye maeneo ya nyonga; nywele kukua kwa kasi na kuongezeka kuota kwa nywele kwenye uso au sehemu nyingine za mwili.

kuumwa kichwa, kuongezeka uzito, maumivu ya kwenye mbavu, kutokewa na uvimbe chini ya ngozi na kuvimba mara kwa mara; maumivu kwenye matiti na kuapata hedhi isiyokuwa na mpangilio maalumu na kuhisi tumbo kuwa zito, kujaa au kuvimba.

Mwanamke mwenye dalili na viashiria hivi afanye nini?

Kwanza kabisa ni kufanyiwa kipimo cha mawimbi ya sauti ndani ya uke (Endovaginal Ultrasound). ambacho hufanywa kwa kuingiza mpira maalum kupitia ukeni na kuangalia mfuko wa uzazi na mayai ya mwanamke.

Kwa kutumia kipimo hiki, ni rahisi kwa daktari kugundua kama kuna uvimbe wowote kwenye Ovari na uvimbe huo ni wa aina gani au atajua kama ni maji tu (Fluid filled sac), au ni maji pamoja na mchanganyiko wa ute mzito, au ni ute mzito pekee.

Kipimo kingine kinachoweza kuchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi ni kipimo cha mawimbi ya sauti kutoka kwenye nyonga hadi kwenye fumbatio (Pelvic Abdominal Ultrasound) ambayo ni Ultrasound ya kawaida. Hii husaidia kujua aina ya uvimbe uliopo kwenye tezi za uzazi (Ovari) za mwanamke.

Vipimo vingine vinavyoweza kuonyesha uvimbe kwenye Ovari ni pamoja na Computerized Tomography (CT) Scan na Magnetic Resonance Imaging (MRI) Scan.

Matibabu ya Ugonjwa wa Tezi za Uzazi za Mwanamke Matibabu ya Sisti/Nziba kwenye Ovari yanategemea sana umri, aina na
ukubwa wa uvimbe pamoja na dalili anazohisi mgonjwa. Mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia vidonge vya uzazi wa mpango ili kupunguza hatari ya kupata Sisti/Nziba kwenye Ovari.

Ni muhimu kufahamu kwamba vidonge vya uzazi wa mpango, mbali na kuzuia upatikanaji wa mimba zisizokuwa na mpango, hupunguza pia hatari ya kupata Kansa au Saratani kwenye Ovari za Uzazi wa Mwanamke.

Kwa hiyo, matiba ya magonjwa haya yanaweza kuhusisha vipimo vya damu kama CA-125 ili kuangalia uvimbe huo kama ni Saratani au ni uvimbe wa kawaida tu. Uvimbe kama haupungui na unasababisha maumivu makali sana, mgonjwa anaweza kushauriwa kufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo.

Kama mgonjwa atalazimika kufanyiwa upasuaji, uvimbe uliotolewa unaweza kupelekwa kwa mtaalam wa Patholojia kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kupata bainisho la mwisho la ugonjwa (Final Diagnosis).

Endapo uchunguzi utaonyesha kwamba uvimbe huo ni wa Saratani, basi Daktari atamshauri mgonjwa kutolewa kwa viungo vyote vya uzazi (Total Hysterectomy) ili kuzuia Saratani kutosambaa kwenye viungo vingine.

The post Dalili za Ugonjwa wa Uvimbe wa Tezi za Uzazi kwa Wanawake na Tiba yake (2) appeared first on Fikra Pevu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>