Quantcast
Channel: Afya – Fikra Pevu
Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Yafahamu Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, Chanzo chake na jinsi Kuishi nayo

$
0
0

Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa ni magonjwa yanayoathiri njia za hewa pamoja na sehemu nyingine zinazohusiana na mapafu, kama vile magonjwa ya Pumu, Kufungana kwa njia za pumzi (Chronic Obstructive Pulmonary Disease-COPD), ugonjwa wa mapafu unaotokana na kazi (Occupational Lung Disease), kupanda kwa shinikizo la damu kwenye Mapafu (Pulmonary Hypertension) na kadhalika.

Magonjwa haya, mara nyingi huathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa hewa na kuzuia kiasi cha hewa inayotoka na kuingia kwenye mapafu, kwa mfano ugonjwa wa Pumu. Hali hii humfanya mgonjwa apumue au kuvuta hewa kwa shida, hasa pale anapokuwa mgonjwa. Magonjwa haya huweza kusababisha kuwepo kwa makohozi katika njia ya hewa, hivyo kusababisha maambukizi mengine.

Kulingana na takwimu ambazo FikraPevu imezipata kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni 235 duniani kote wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa Pumu, huku watu milioni 64 wakitajwa kusumbuliwa na magonjwa sugu ya kufungamana kwa njia ya Pumzi (COPD). Kwa mujibu wa WHO, takriban asilimia 90 ya vifo vinavyotoakana na magonjwa hayo, hutokea katika nchi zilizo na uchumi duni na wa kati, Tanzania ikiwa mojawapo.

Watu wengi hudhani kwamba mtu anapokuwa mwembamba kupita kiasi na akawa na uzito kidogo, basi mtu huyo atakuwa na ugonjwa wa Ukimwi. Wanaodhani hivyo, hawajui kwamba magonjwa sugu ya njia ya hewa, nayo yanaweza kumsababishia mtu akakonda na kupungua uzito pia.

Hali hiyo hutokea kutokana na ukweli kuwa magonjwa hayo ya njia ya hewa, humfanya mgonjwa atumie nguvu nyingi wakati wa kupumua kuliko mtu asiyekuwa na magonjwa hayo.

Matumizi makubwa ya nguvu wakati wa kupumua, humfanya mgonjwa asiwe na nishati ya akiba ambayo huhifadhiwa mwilini, hivyo kufanya mtu kuwa mnene. Lakini pia unene uliokithiri, unaweza kusababisha magonjwa mugu ya njia ya hewa.

Ni nini chanzo cha magonjwa sugu ya njia ya hewa?

Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, mara nyingi husababishwa na kuharibika kwa njia ya hewa katika mapafu. Uharibifu huo wa njia ya hewa huweza kutokana na uvutaji wa sigara na matumizi ya ugolo; kuvuta hewa yenye sumu au vumbi kutoka viwandani, uchafuzi wa hewa ya ndani mfano kwa kutumia jiko la utambi na mafuta ya taa; uchafuzi wa hewa ya nje kutokana na vumbi au poleni ya maua na unene uliokithiri kiwango.

Anayesumbuliwa na ugonjwa sugu wa njia ya hewa azingatie nini ili aweze kuishi?

Mgonjwa wa ugonjwa sugu wa njia ya hewa anashauriwa kuzingatia ushauri wa daktari na matibabu yake, kufuata kanuni za mtindo bora wa maisha, kuepuka visababishi kama vile vumbi, barafu na harufu, kuhakikisha mazingira na nyumba anaoishi ni safi muda wote, na zaidi pia iwe na madirisha yanayoruhusu mzunguko wa hewa.

Aidha, wagonjwa wa magonjwa hayo wanashauriwa kula mlo kamili na vyakula vya aina mbalimbali ili wapate virutubishi vyote vinavyohitajika kwa afya zao. Inashauriwa kula zaidi matunda freshi, mbogamboga zenye rangi ya kijani, matunda yenye rangi ya njano kama vile ndizi, papai, embe, mapera na kadhalika.

Lakini pia, wanashauriwa kula vyakula vyenye makapi mlo kwa wingi ili kusaidia mfumo wa kusaga chakula kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa uchafu tumboni kwa urahisi. Hali hii huwasaidia kuweza kupumua kwa urahisi.

Ikumbukwe kuwa mgonjwa wa aina hiyo anatumia nguvu nyingi wakati wa kupumua, hivyo basi anahitaji kula chakula cha kutosha ili kumpatia nguvu za kutosha. Ni vizuri kula milo midogo midogo mara kwa mara, ikiwa ni pamoja nakupunguza matumizi ya chumvi ili kuepuka maji kujikusanya mwilini na kusababisha kupumua kwa shida. Ni muhimu pia kuepuka uzito uliozidi kwa sababu unene huongeza tatizo la kupumua.

Je, mgonjwa wa mugonjwa sugu wa njia ya hewa anaruhusiwa kufanya mazoezi?

Mazoezi ya mwili yana faida nyingi kiafya. Baadhi ya faida hizo ni kuimarisha mapafu na moyo. Ili kuviwezesha viungo hivyo muhimu katika mwili wa mwanadamu vifanye kazi kwa ufanisi, mazoezi ni muhimu sana. Aidha, mazoezi husaidia kuimarisha misuli ambayo hutumika wakati wa kupumua.

Kwa hiyo, mgonjwa wa magonjwa sugu ya hewa anaruhusiwa kufanya mazoezi kwa sababu mazoezi ni sehemu ya matibabu yake. Mgonjwa anapaswa kujitahidi mara kwa mara kufanya mazoezi, kwa kuanza mazoezi ya taratibu kwa kadri mwili wake unavyoweza kustahimili, na kisha kuongeza hatua kwa hatua.

Hata hivyo, inashauriwa mgonjwa anayefanya mazoezi, pindi asikiapo maumivu kifuani au kushindwa kuhimili mazoezi hayo, punguza kasi ya mazoezi hayo na fanya kwa taratibu kadri iwezekanavyo.

The post Yafahamu Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, Chanzo chake na jinsi Kuishi nayo appeared first on Fikra Pevu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 296

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>