Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Sheria ya Kudhibiti Uvutaji wa Sigara kwenye ofisi za umma pamoja na kwenye mikusanyiko wa watu. Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge mwaka 2003 ili pamoja na mambo mengine, ikilenga kuhakikisha kwamba watu hawapati madhara yatokanayo na moshi wa sigara au matumizi ya tumbaku kutokana.
Jina la sheria hiyo ya afya, inaitwa Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL, ya mwaka 2003. Kipengele cha 12(1) cha sheria hiyo, kinapiga marufuku matumizi ya bidhaa yoyote ya tumbakuh katika maeneo ya umma.
Kutokana na kuwepo kwa sheria hiyo, wananchi wote wanaotumia bidhaa za tumbaku, wanatakiwa kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya bidhaa hiyo, ikiwa ni pamoja na kuhimiza umuhimu wa kutolewa elimu kwa jamii nzima ili kujua madhara ya matumizi ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia uvutaji katika maeneo ya umma. Uvutaji sigara ulianza kupigwa marufuku kwa mara ya kwanza na Kanisa Katoliki mwaka 1,575, lakini katika karne ya 20 harakati dhidi ya uvutaji wa sigara zilipamba moto kwa sababu za kiafya.
Licha ya kuwepo kwa sheria hiyo nchini, utekelezaji wake kwa vitendo umeshindikana kwa kuwa ni jambo la kawaida katika mikusanyiko ya watu kukuta mvutaji wa sigara au mtumiaji wa tumbaku aina ya ugolo akifanya hivyo hadharani bila kuhojiwa na yeyote. Hata hivyo, wakati sheria hiyo ikishindikina kusimamiwa katika Tanzania, nchini China sheria hiyo imesimama kama ilivyo.
FikraPevu inaweza kuthibitisha kwamba China inaongoza ulimwenguni kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaovuta sigara. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, idadi ya wavuta sigara katika nchi hiyo inafikia milioni 300. Kwa hiyo, kutokana na madhara makubwa ya sigara yanayotokana na idadi hiyo ya wavutaji, Serikali ya nchi hiyo imeamua kutekeleza kwa vitendo sheria ya kuzuia uvutaji wa sigara kuanzia Juni Mosi, mwaka huu wa 2015.
Katika sheria hiyo mpya ya China, mtu yeyote atakayekamatwa akivuta sigara katika mikusanyiko ya watu atalazimika kulipa faini ya dola za Marekani 30, sawa na karibu Sh 60,000. Nionavyo mimi, kama Serikali ya nchi ya China imeweza kuamua kusimamia sheria hiyo kwa vitendo pamoja na kuwa na idadi kubwa hiyo ya wavutaji na watumiaji wa tumbaku, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara ya kiafya yanayotokana na bidhaa hiyo kwa wananchi wake, Tanzania tumeshindwa nini kusimamia sheria hiyo?
Takwimu kutoka nchini China zinaonyesha kwamba kila mwaka, watu zaidi ya milioni moja wanafariki dunia kutokana na magonjwa yanayotokana na uvutaji wa sigara na matumizi mengine ya tumbaku.
Aidha, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2003, zinaonyesha kuwa kila baada ya sekunde 10, mtu mmoja hufariki dunia kutokana na maradhi yatokanayo na matumizi ya tumbaku.
Kwa mujibu wa takwimu hizo za WHO, inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2025, vifo vitakavyotokana na matumizi ya tumbaku vitaongezeka kwa kiwango cha asilimia 70 kuliko ilivyokuwa mwaka 2003. Lakini pia, takwimu hizo zinaonyesha kuwa kufikia mwaka 2030, idadi ya watu milioni 10 watakuwa wakifariki dunia kila mwaka kutokana na uvutaji wa sigara ulimwenguni, huku ikitajwa kuwa asilimia 70 ya vifo hivyo vikitokwa katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwemo.
Inaonyesha pia kwamba asilimia 36 ya wavuta sigara barani Afrika ni wanaume, huku asilimia tisa tu wakiwa ni wanawake, wakati kwa upande wa Tanzania asilimia ya wanaume wanaovuta sigara ni asilimia 46, wakati wanawake inatajwa kuwa ni asilimia nne tu.
Kuna aina mbalimbali za matumizi ya tumbaku, kama vile kubwia, kunusa, kuvuta na kutafuna, ambapo wananchi wengi katika maeneo ya mijini na vijijini, wamekuwa wakitumia tumbaku kwa wingi bila kujua madhara ya kiafya ambayo yanaweza kuwapata.
Kwa mujibu wa tafiti zilizopo, matumizi makubwa ya tumbaku yamekithiri zaidi katika nchi zinazoendelea kuliko nchi zilizoendelea kutokana na juhudi za kampuni kubwa zinazozalisha bidhaa hizo kupanua wigo wao wa kibiashara kwa kuweka matangazo mbalimbali yanayotoa tahadhari juu ya madhara yasababishwayo na tumbaku. Wataalamu wa afya wanayataja magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababishwa na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kuwa ni pamoja na saratani ya ngozi, saratani ya mapafu, saratani ya kizazi, saratani ya koo, saratani ya kinywa na saratani ya kibofu.
Magonjwa na madhara meninge ni magonjwa ya moyo, kuathirika kwa mimba, mtoto anayezaliwa kuwa mlemavu wa akiri, watoto kuzaliwa na afya hafifu hivyo kuathiri ukuaji wao, kupungua kwa nguvu za kiume, vidonda vya tumbo, mtoto wa jicho, kunyonyoka nywele na kuziba kwa mishipa ya damu.
Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa za kuelimisha jamii madhara ya tumbaku ili wananchi wasihamasike kutumia bidhaa za tumbaku. Hata hivyo, pamoja na kutengwa siku maalum ya kutotumia tumbaku duniani ambayo huadhimishwa kila Mei 31 kila mwaka, bado inaonekana tatizo la matumizi ya tumbaku linaongezeka kwa kasi kubwa katika jamii.
Ni muhimu basi wakati jamii ikiishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa busara wa kutunga sheria hiyo ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya, kikiwemo Chama cha Afya ya Jamii Tanzania(TPHA), wahusika wakuu wa usimamizi wa sheria hiyo wakatimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wote wanaovuta sigara kwenye mikusanyiko ya watu na maeneo ya umma, wanachukuliwa hatua za kisheria.
Wakati China ikitajwa kuwa nchi ya mfano katika kusimamia sheria hiyo, Juni 22, 2009, Rais Barack Obama wa Marekani alisaini muswada wa sheria ya usimamizi wa tumbaku, ambao uliipatia Idara ya Usimamizi wa Chakula na Dawa katika nchi hiyo, mamlaka makubwa ya kusimamia matumizi ya tumbaku.
Kwa mujibu wa muswada huo, unaujulikana kama Sheria ya Kuzuia Uvutaji wa Sigara Majumbani na Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku, Idara ina mamlaka ya kupunguza kiwango cha nikotini kwenye bidhaa za tumbaku, kupiga marufuku uuzwaji wa sigara zenye ladha ya pipi kwa vijana, pamoja na kupiga marufuku alama za kibabaishaji kama vile kiwango cha chini cha kemikali na kuchapisha onyo la madhara ya uvutaji kwa afya.
Aidha, Oktoba 28, 2009, Serikali ya Uswisi pia iliidhinisha ratiba ya kuanza utekelezaji wa sheria ya kuzuia uvutaji sigara hadharani, ambapo ilipangwa kuanza kutumika Mei Mosi, 2010. Sheria hiyo ya Uswisi inapiga marufuku uvutaji sigara hadharani au kwenye sehemu yoyote ya kazi yenye watu zaidi ya wawili.
Desemba 8, 2009, Serikali ya Korea Kusini, kupitia Wizara ya Afya na Huduma za Jamii, ilitangaza mpango wa kupiga marufuku uvutaji sigara kwenye maeneo ya wazi, sharia iliyotakiwa kuanza kutumika mwaka 2011.
Novemba 15, Serikali ya Poland nayo ilisaini sheria hiyo. Kwa mujibu wa sheria hiyo ya nchi hiyo, watu wanaovunja sheria hiyo watalipa faini ya dola 175 za Marekani, sawa na karibu Sh 350,000. Aidha, sheria hiyo inawataka wamiliki wa maeneo ya wazi, kuweka alama zinazopiga marufuku uvutaji sigara katika maeneo yao hayo, vinginevyo wakibainika kutofanya hivyo, wanalipa faini ya hadi dola 700 za Marekani, sawa na karibu Sh milioni 1.4.
Nchi nyingine ulimwenguni ambayo imesaini sharia hiyo na kuisimamia ni Sweden. Sheria hiyo ya tangu mwaka 1993, inapiga marufuku uvutaji sigara katika sehemu zenye shughuli za watoto, huduma za matibabu na sehemu za mawasiliano ya umma.
Aidha, sheria hiyo inawataka waajiri wote nchini humo kuhakikisha wanaweka mazingira yasiyo ruhusu uvutaji sigara katika maeneo yote ya kazi, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku wauzaji wa sigara kuuza bidhaa hiyo kwa vijana wenye umri chini ya miaka 18.
Je, kama nchi zote hizo zimeweza kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa sheria za matumizi ya bidhaa za tumbaku kutokana na madhara yake kiafya, Serikali ya Tanzania na Watanzania, tumeshindwa kwanini wakati sheria tunayo?