TAKWIMU za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa nchi zilizopo Kusini Mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo, zinaongoza kuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa kiwango kikubwa, ambapo watu milioni 24.7 walikuwa wanaishi na VVU hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2013.
Kwa mujibu wa takwimu hizo za WHO, ukanda huo unabeba asilimia 70 ya maambukizi mapya ya VVU duniani na kwamba duniani kote kumekuwa na tafiti nyingi kuhusu janga hilo ili kupata suluhisho la moja kwa moja kupitia tiba mbalimbali.
Jaribio kubwa la kitafiti la kimataifa lililopewa jina la Strategic Timing of AntiRetroviral Treatment (START) limegundua kuwa watu walioambukizwa VVU wana hatari ndogo ya kupata UKIMWI au maradhi sugu nyemelezi kama Kifua Kikuu ikiwa wataanza kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU mapema wakati idadi ya CD4 ikiwa bado kubwa badala ya kusubiri idadi ya CD4 kushuka chini.
Tafiti za WHO zinaonyesha kuwa watu wanaoanza matibabu ya kupunguza makali ya VVU mapema, kunapunguza hatari ya kuambukiza VVU kwa mke, mume, au mpenzi asiye na maambukizi ambapo matokeo ya tafiti hizo yanaunga mkono kutoa matibabu kwa kila mtu aliyegundulika kuwa na VVU.
Aidha, matokeo haya mapya yametokana na utafiti mkubwa uitwao START ambao ulidai kuwa watu wote walio na maambukizi ya VVU wakianza matibabu ya kupunguza makali ya VVU watanufaika.
Taasisi ya Taifa ya Mzio na Magonjwa ya Kuambukiza inayojulikana kama The National Institute of Allergy and Infectious Diseases (NIAID) ya nchini Marekani kama moja ya taasisi za afya nchini humo ilifadhili utafiti huo, ingawa utafiti huo ulitarajiwa kukamilika 2016, bodi inayohusika na takwimu nchini humo ijulikanayo kama Data and Safety Monitoring Board (DSMB) ilipendekeza matokeo kutolewa mapema zaidi.
Mkurugenzi wa NIAID, Daktari. Anthony S. Fanci, amesema wanao uthibitisho kwamba utafiti huo ni kitu chenye manufaa makubwa kwa mtu yeyote aliyeambukizwa VVU kuanza matibabu ya kupunguza makali ya VVU mapema kuliko kuanza baadae.
"Kuanza matibabu mapema hutoa faida mara mbili zaidi, sio tu kuboresha afya za walioambukizwa lakini pia kupunguza wingi wa virusi (viral load) kitu kitakachosaidia kupunguza hatari ya kuambukizwa VVU kwa wengine. Matokeo haya ya utafiti yanaweza kubadili miongozo ya matibabu ya VVU dunia nzima", aliongezea Dk.Fanci.
Kwa upande wake Daktari, Jens Lundgren, kutoka Chuo Kikuu cha Copenhagen,mmoja wa wenyeviti wa utafiti huo alisema hatua hiyo ni muhimu katika utafiti wa VVU, “Sasa tunao ushahidi mkubwa kwamba kuanza matibabu mapema ni faida kwa mtu mwenye VVU. Matokeo haya ya utafiti yanahamasisha kutibu mtu yeyote mwenye VVU bila kujali idadi ya CD4 zake na kuanza matibabu mapema kunaleta faida kwa watu wote bila kujali unatoka katika nchi yenye kipato cha chini, cha kati au cha juu”.
Utafiti wa START uliozinduliwa rasmi Machi, 2011 na kuendeshwa na taasisi ya The International Network for Strategic Initiatives in Global HIV Trials (INSIGHT) katika vituo 215 kwenye nchi 35. Ulibaini kwamba jumla ya watu wenye VVU 4, 685, wanaume kwa wanawake kuanzia miaka 18 na zaidi, wengi wao wakiwa na miaka 36 walitumika katika jaribio. Washiriki hawakuwa kwenye matibabu ya kupunguza makali ya VVU na walikuwa na CD4 zaidi ya 500.
Kwa mujibu wa utafiti huo, walikadiria nusu ya washiriki na kuwaanzishia matibabu ya kupunguza makali ya VVU mapema na nusu waliobaki waliachwa hadi idadi ya CD4 zao zilipoteremka hadi 350 ambapo kwa wastani washiriki wa utafiti walifuatiliwa kwa miaka mitatu. Utafiti ulipima jumla ya matokeo yaliyohusisha hali mbaya zinazotokana na UKIMWI kama Kifua Kikuu na Saratani zinazohusiana na UKIMWI kama Saratani ya Seviksi (Shingo ya Kizazi) pamoja na hali mbaya zisizohusiana na UKIMWI ikiwemo magonjwa ya moyo, Ini, figo na kifo.
Kulingana na takwimu za Machi, 2015; DSMB walipata sampuli 41 zisizo na hali mbaya, zisizohusiana na UKIMWI kwa wale walioanza matibabu mapema na hali mbaya 86 kwa wale ambao hawakuanza matibabu mapema. Uchambuzi uliofanywa na DSMB wamegundua hatari ya kupata maradhi nyemelezi mabaya au kifo ambayo ilipunguzwa kwa asilimia 53 kwa wale walioanza matibabu mapema ikilinganishwa na wale waliochelewa.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa utafiti wa START ni utafiti mkubwa na wa kwanza kutoa ushahidi wa kisayansi wa kuunga mkono muongozo wa matibabu ya VVU nchini Marekani unaopendekeza watu wote wenye VVU hata wasio na dalili za VVU kuanza matibabu mapema bila kujali idadi ya CD4 zao. Muongozo wa sasa wa matibabu ya VVU wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unapendekeza kuwa watu wenye VVU waanze matibabu ya kupunguza makali ya VVU ikiwa CD4 zao zitashuka hadi 500 au chini ya hapo.
Nchini Tanzania, utafiti wa kiashirio cha VVU/UKIMWI na Malaria 2011-2012 uliojumuisha kwa kupima zaidi ya wanawake na wanaume 20,811 kwa mujibu wa utafiti huo asilimia 5.1 ya watanzania wenye umri wa miaka (15-49) wana maambukizi ya VVU/UKIMWI. Maambukizi ya VVU/UKIMWI ni ya kiwango cha juu miongoni mwa wanawake kuliko wanaume katika maeneo ya mjini na vijijin na wakazi wa mijini ni mara mbili zaidi ya wakazi wa vijijini.
Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa mkoa wa Njombe unaongoza kwa maambukizi ya VVU kwa asilimia 14.8 ambapo Iringa ina asilimia 9.1 ya watu walioathirika na VVU na Mbeya ikiwa na asilimia 9.0, kwa upande wa mikoa yenye kiwango cha chini cha maambukizi ya VVU ni Manyara na Kilimanjaro ambazo zina asilimia 2 ya maambukizi ya VVU na Pemba ikiwa ni chini ya asilimia 1 ya maambukizi ya VVU.
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2013 zinasema tayari watu milioni 1.4 wanaishi na VVU nchini Tanzania. Wakati takwimu za Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) zikiripoti kuwa kuwapatia watu waishio na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) 70, 000 tiba ya kuongeza kinga ya mwili hadi kufikia 2006. Baadhi ya vitu vinavyosababisha kuenea kwa VVU nchini ni pamoja na kufanya mapenzi bila ikiwa ni pamoja na kutotumia kondomu, matumizi ya pombe, dawa za kulevya na kuwepo kwa maradhi ya ngono ikiwemo Kisonono na Kaswende.