Takwimu zinaonyesha kuwa takribani wanawake 454 kati ya vizazi hai 100,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na tatizo la uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa damu. Juhudi za serikali kwa kushirikiana na wizara ya afya inafanya jitihada mbalimbali za kutaka kupunguza idadi hiyo hadi kufikia vifo 68 katika 1,000.
Wapo akina mama wengi ambao hujifungua bila matatizo lakini haiwi hivyo nyakati zote. Kwa midingi hiyo, wazazi wenye kujali hufanya lolote wanaloweza ili kuepuka matatizo wakati wa uzazi. Kwa mfano, wao hujifunza mambo yanayosababisha matatizo wakati wa kujifungua, wanaenda kliniki ya akina mama wajawazito na wanachukua hatua rahisi za kupunguza matatizo wakati wa kujifungua. Hapa ndipo kampeni kama ya "Thamini Uhai’ (Mradi wa World Lung Foundation) iliyolenga kuongeza huduma za kiafya kwa mama wajawazito wakati wa kujifungua hua msingi katika kuongeza elimu ya afya kwa jamii.
Kama ilivyoelezwa hapo mwanzo, Damu ni moja ya hitaji la msingi katika uzazi kwa mama na mtoto. Damu ikiwa kama kiowevu katika mwili wa binadamu na pia wanyama. Inazunguka mwilini ikisukumwa na moyo ndani ya mishipa ya damu.
Damu hufanya kazi nyingi muhimu katika mwili zikiwemo; Upelekaji wa oksijeni kwenye tishu, ugavi wa virutubisho kama vile glukosi & amino asidi, uondoaji wa taka kama vile dioksaidi ya kaboni & urea, kukinga mwili, kuganda ambayo ni sehemu moja ya utaratibu wa kujirekebisha kwa mwili ambapo damu huganda wakati mtu anapokatwa ili kuziba kutoka kwa damu, usafirishaji wa homoni na udhibiti wa kiwango cha joto mwilini.
Ni wajibu wa watu wote kuhakikisha wanachangia damu ili jamii iweze kutimiza mahitaji yake kwani kunapokuwa na akiba ya damu iliyo salama kuna kuwa na uhakika wa tiba. Uchangiaji damu ni kitendo cha kutoa damu kwa hiari ili iweze kutumiwa kwa mtu mwingine kimatibabu.
Uchangiaji wa damu upo wa aina mbili, aina ya kwanza ikiwa ni 'Homologous/Allogeneic Donation' kutoa damu ili ikahifadhiwe kwenye benki ya damu na itamsaidia yeyote atakayehitaji na aina ya pili ikiwa ni 'Directed Donation' kutoa damu ikamsaidie mtu unayemfahamu mara nyingi huwa ni mshiriki wa familia.
Makundi katika jamii yanayohitaji damu mara kwa mara ni wajawazito na wanawake wenye matatizo ya uzazi, watoto wadogo hasa walio chini ya umri wa miaka mitano, watu wanaofanyiwa tiba ya upasuaji, wale wote wenye magonjwa mbalimbali yanayosababisha upungufu wa damu kama saratani ya damu na majeruhi wa ajali mbalimbali hasa ajali za barabarani.
Tabia ya kuchangia damu kwa hiari ni kitendo ambacho kitapunguza vifo vya kina mama wajawazito 363 vinavyotokea kila mwaka kutokana na tatizo la ukosefu wa damu wakati wa kujifungua. Ili kukabiliana na tatizo hili serikali kupitia wizara ya afya ilianzisha 'Mpango wa Damu Salama.'
Tangu kuanzishwa kwa mpango wa damu salama mwaka 2004 kumekuwa na ongezeko la wachangia damu kwa hiari kutoka kiasi cha chupa 5,000 kwa mwaka 2005 hadi chupa 160,000 kwa mwaka 2013, ikikadiriwa mahitaji ya damu kwa mwaka kitaifa ni wastani wa chupa 400,000 hadi 450,000 wakati damu inayopatikana kwa mwaka ni chupa 160,000 sawa na asilimia 30 pekee.
Changamoto zinazoukabili 'Mpango wa Damu Salama' ni pamoja na mahitaji makubwa kuliko upayikanaji wa damu, uelewa mdogo wa jamii juu ya suala zima la uchangiaji damu kwa hiari, uuzwaji wa damu usio halali hospitali jambo ambalo linakatisha tamaa wachangiaji damu kwa hiari na matumizi yasiyo sahihi ya damu katika hospitali.
Sifa za wanaopaswa kuchangia damu:-
Umri
Umri wa chini unaoruhusiwa kuchangia damu kwenye nchi nyingi ni miaka 18, ingawa kuna baadhi ya nchi huruhusu miaka 16-17 ikiwa amekidhi vigezo vingine vya muhimu kiafya.
Kwa kawaida umri wa juu wa kuchangia damu ni miaka 65. Kwa wale wanaotoa damu kwa mara ya kwanza ambao umri wao ni zaidi ya miaka 60 wanapaswa kutoa damu mahali palipo na daktari bingwa (Physician).
Afya
Anayetarajia kuchangia damu anapaswa kuonekana mwenye afya, asiye na utapiamlo, asiye na homa, asiyepata shida ya kupumua au mwenye kikohozi sugu, mwenye akili timamu na asiwe mlevi sugu, pia ngozi ya mwili inapaswa kuwa ya kawaida na macho yasiyo na manjano (Jaundice).
Dalili za mara kwa mara za mtoaji damu kama vile uchovu na maumivu ya mwili, homa, kuumwa kichwa, kukohoa, kuhara zinaonyesha uwepo wa ugonjwa ambao unaweza kuambukizwa kwa mtu atakayetowa damu mwenye dalili hizo. Wachangiaji damu wanapaswa kuulizwa kama hawana dalili hizo na wamepona kabisa kama waliuugua hivi karibuni, walau ziwe zimepita siku 14 tangu kumaliza matibabu.
Uzito
Kiujumla inakubalika kwamba ujazo wa damu yote itakayochangiwa isizidi asilimia 13 ya damu yote ya mchangiaji kwa mfano mtu mwenye kilo 50 anapaswa kutoa mililita 450. Ikiwa wachangiaji damu wapo chini ya uzito wa kilo 45 au 50, ujazo wa damu itakayochangiwa inapaswa kupunguzwa kama inavyostahili kuendana na vitunza damu vilivyokusanywa.
Vipimo muhimu
Msukumo wa damu kwenye mishipa (Pulse) unapaswa kuwa kati ya 60 mpaka 100 kwa dakika pia ujazo/msukumo unapaswa kuwa usiobadilikabadilika.
Joto la mwili: Mchangiaji damu mwenye homa hubainika kwa kuangalia/kupima joto la mdomoni likiwa limezidi 37.6°C. Uwepo wa homa ni kiashiria cha uwepo wa ugonjwa, hata hivyo huambatana na dalili zingine.
Shinikizo la damu (Blood Pressure): Shinikizo la damu kwa kipimo cha juu (Systolic BP) ikiwa kuanzia 120 hadi 129 mmHg na kipimo cha chini (Diastolic BP) ikiwa 80 hadi 89 mmHg, kiujumla huonekana kama kiashiria cha afya njema. Ukomo wa shinikizo la damu unaokubaliwa ni Sytolic BP kuanzia 100 hadi 140 mmHg na Diastolic BP kuanzia 60 hadi 90mmHg.
Hali ya Madini ya Chuma
Madini chuma yana faida nyingi mwilini ikiwa ni pamoja na kutengeneza chembechembe nyekundu za damu, kuimarisha kinga ya mwili, kuimarisha uwezo wa kuwa makini na huongeza uwezo wa kufanya kazi vizuri.
Hakuna njia ya haraka na nyepesi ya kutambua hali ya madini chuma kwa mchangiaji damu. Katika nchi nyingi kiwango cha chini cha damu (Haemoglobin Level) kwa mwanamke hakipaswi kuwa chini ya 12.5 g/dl na kiwango cha chini cha damu kwa mwanaume hakipaswi kuwa chini ya 13.5 g/dl. Kuna baadhi ya nchi kiwango kile kile cha damu kwa mwanamke na mwanaume hutumika. Watakao kuwa na upungufu wa damu chini ya kiwango kilichopendekezwa huonekana wenye upungufu wa damu mwilini.
Shirika la Afya Ulimwenguni hutafsiri upungufu wa damu ikiwa ni chini ya 12.0 g/dl kwa mwanamke asiye mjamzito, 11.0 g/dl au chini ya hiyo kwa mjamzito na 13.0 g/dl kwa mwanaume. Katika nchi tofauti muda toka umechangia damu mara ya mwisho ni kati ya wiki 8 na 18, kimsingi wanawake hawawezi kutoa damu zaidi ya mara moja au mbili kwa mwaka kwa kuwa hupatwa na upungufu wa madini chuma haraka kuliko wanaume, ambapo mahitaji ya madini chuma kwa wanaume ni miligramu 1.50 kwa siku wakati kwa wanawake ni miligramu 1.62 kwa siku. Utoaji wa mililita 450 za damu huondoa miligramu 200 hadi 250 za madini chuma mwilini.
Ulaji wa Chakula na unywaji wa Maji
Miongozo mingi ya uchangiaji damu hushauri wachangiaji damu waendelee kula kawaida na kunywa maji kawaida kabla ya kutoa damu ila wanapaswa kujiepusha na kula sana pamoja na vyakula vyenye mafuta vinavyosababisha damu kuwa na mafuta mengi na hupelekea damu kutupwa baada ya kukusanywa kwenye vituo vya kuchangia damu. Athari kwa wachangiaji damu waliofunga bado hazijajitokeza lakini ushahidi upo kwa walio kunywa mililita 500 za maji ya kunywa muda mfupi kabla ya kutoa damu hawakupata athari zinazotokana na kutoa damu. Hivyo inashauriwa kuwepo na maji safi na salama ya kunywa kwenye vituo vya kuchangia damu. Kwa wale wachangiaji damu wanaofunga wanapaswa kunywa maji masaa manne kabla ya kutoa damu.
Jinsia
Kwa kawaida mwanamke huhitaji miligramu 350 hadi 500 za ziada za madini chuma ili kuweka uwiano sawa wa madini chuma wakati wa ujauzito. Hivyo wanawake wajawazito, waliojifungua au walioharibu mimba ndani ya miezi 6 na wanao nyonyesha hawapaswi kuchangia damu ili kuruhusu madini chuma yarejee vizuri mwilini. Wanawake walio katika siku zao (Hedhi) wanaruhusiwa kuchangia damu ikiwa wanajisikia vizuri na wanakidhi vigezo vingine vya kutoa damu.
Vile vile damu iliyochangiwa na mwanamke aliyezaa zaidi ya mara moja inaweza kusababisha matatizo ya mapafu kwa mtu aliyeongezewa damu kuliko damu iliyochangiwa na mwanaume.
Kazi na Starehe
Wachangiaji damu wanashauriwa kutofanya kazi ngumu ndani ya masaa 24 baada ya kuchangia damu. Vile vile wale wanaofanya kazi za kutoa msaada wa dhalura (Emergency Services) au wale wanafanya kazi kwenye vilele vya milima mfano waongozaji watalii wa kupanda milima wanapaswa kutofanya kazi zao ndani ya masaa 24 baada ya kutoa damu.
Wafanya biashara za ngono (Sex Workers) wako katika hatari kubwa ya kusambaza magonjwa hivyo hawapaswi kuchangia damu. Kazi zingine ukitia ndani wahudumu wa afya, polisi na wanajeshi wako katika hatari kubwa ya kusambaza magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya damu, hivyo wanapaswa kuulizwa na kufanyiwa uchunguzi mzuri kabla hawaja changia damu.